WAKATI Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), akisema kuwa serikali yoyote yenye dalili za kuelekea kubaya huanza kufungia au kudhuru vyombo vya habari halafu binadamu, Muungano wa Mabaza ya Habari Duniani (WAPC) na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ) wamelaani kitendo hicho.
Kauli hizo zimekuja zikiwa zimepita siku chache tangu serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi kwa siku 14 na Mtanzania siku 90, kwa kile kinachodaiwa ni kuchapisha habari za uchochezi.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Lembeli ambaye kitaaluma ni mwandishi, alisema kuwa serikali yoyote inayotumia mabavu kama hayo, hapo kuna madhara, na kwamba ni dalili mbaya kwamba inakoelekea siko.
Alisema kuwa amesikitishwa na hatua hiyo ya serikali kuyafungia magazeti hayo kwa kutumia sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976, wakati vyombo vya habari siku zote ndivyo vimekuwa watetezi wa wanyonge.
Lembeli alifafanua kuwa sababu kama hizo wakati mwingine ndizo zinawafanya wananchi kukosa imani na serikali yao, hivyo hata wanahabari wanapodhuriwa wanaihusisha serikali na matukio hayo.
Alisema kuwa kufungia vyombo vya habari si suluhisho la kutofichua maovu, kwani siku hizi nchi ipo katika teknolojia ya kisasa na kwamba ukifungia gazeti wanatumia mitandao.
“Ukifungia mitandao ya online, wanatumia kuhabarishana kwa njia za simu. Ukianza kumuona baba anaziba midomo ya mtoto wake anayehoji na kudadisi, basi hiyo nyumba ni lazima iwe na matatizo.
“Suluhisho hapo ni kujibu hoja na si kufungia, na kama kuna kosa, basi baba anatakiwa kuwa wa kwanza kumkanya mtoto kwa njia sahihi badala ya kufunga mdomo,” alisema.
Kwa mujibu wa Lembeli, sheria ya magazeti ya mwaka 1976, imepitwa na wakati huku akishangaa sababu za serikali kushindwa kupeleka muswada bungeni kuifanyia marekebisho.
WAPC, IFJ wacharuka
Muungano wa Mabaraza ya Habari Duniani (WAPC) umeungana na wadau wengine wa Tanzania na Afrika kupaza sauti kutaka uhuru wa habari na haki za binadamu kwa kulaani serikali kuyafungia kibabe magazeti mawili ya kila siku.
Taarifa ya WAPC kupitia kwa Katibu Mkuu Chris Conybeare, ilisema kuwa matendo hayo ni ya kuchukiza na kwa wale wanaotafuta umaarufu wa kidemokrasia au kisiasa, watambue kuwa hayo hayawezekani bila kuwapo na uhuru wa vyombo vya habari na jamii huru.
Alisema kuwa Watanzania wamejitahidi kwa muda mrefu kuwa na jamii iliyokomaa kidemokrasia. Kwamba huu ni muda mwafaka wa serikali kufanyia marekebisho au kuondoa sheria ya kibabe ya magazeti ya mwaka 1976 na ile ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970.
“Sheria hizo zinazuia uhuru wa mawazo unaokuza demokrasia. Uhuru wa habari ni muhimu kwa demokrasia na katika haki za binadamu kama ilivyotangazwa na kifungu cha 19 cha Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu,” alisema.
Alisema kuwa kuyafungia magazeti hayo ni kukiuka haki za binadamu na uamuzi huo unapaswa kuondolewa haraka.
Nalo Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ) limeeleza kuhusu wasiwasi mkubwa katika hali ya kuzorota kwa uhuru wa habari nchini kufuatia uamuzi wa serikali kuyafungia magazeti mawili.
“Tuna wasiwasi na umakini wa Serikali ya Tanzania kwa uamuzi wa kuyafungia magazeti. Kufungia magazeti maana yake ni kuwazuia waandishi wa habari wasitoe taarifa kwa umma.
“Huu ni ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa habari ambao haupaswi kufikiriwa kuwa umetokea kwa bahati mbaya,” alisema Gabriel Baglo, Mkurugenzi Mkuu wa shirikisho hilo, akisema Tanzania ni lazima iyafungulie magazeti hayo.
Alisema kuwa IFJ inaamini kuwa waandishi wa Tanzania wamekomaa kimaadili, hivyo hawawezi kuandika kinyume cha maadili ya kazi zao za kila siku.
“IFJ linaona kuwa serikali haiwezi kuficha kitu chochote kutokana na kujiingiza katika mijadala na waandishi wa habari ili kutengeneza jamii ya pamoja inayowajibika,” alisema.
Aliongeza kuwa ukweli ni kuwa Tanzania inaendelea kukandamiza uhuru wa habari wakati nchi nyingine katika Afrika zinajitahidi kutafuta uhuru wa habari na uhuru wa kutoa mawazo.
CHADEMA yang’aka
Nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeeleza kusikitishwa na adhabu hiyo ya kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasilinao ya chama hicho iliyosainiwa na John Mnyika, ilisema kuwa serikali imeendelea kutumia sheria mbaya na madaraka vibaya kufanya uamuzi mbaya, kila inapokosa hoja na uwezo wa kukabiliana na sauti mbadala au maoni kinzani.
“Suala hili limekuwa dhahiri zaidi baada ya serikali kuamua hata kuanza kuingilia uhuru wa habari na maoni kwenye mitandao ya kompyuta (online), pia kutishia kulifungia gazeti la Rai, linalotolewa na Kampuni ya New Habari (2006) Limited, kwa sababu limeanza kuchapishwa kila siku,” alisema Mnyika katika taarifa hiyo.
Mnyika alisema serikali inajichanganya. Kwamba hiyo ni dalili ya wazi kuwa uamuzi wake huo ni mwendelezo wa uamuzi wa kibabe, usiofanywa kwa masilahi ya Watanzania.
“CHADEMA inapinga na itaendelea kupinga kwa kauli na vitendo, hatua hii ya serikali yenye lengo ovu dhidi ya umma wa Watanzania. Ni suala linalohitaji tafakuri yetu sote, kwa nini serikali imeamua kuchukua hatua hii wakati huu ambapo nchi nzima iko kwenye mjadala wa Katiba Mpya?” alihoji.
Kwa mujibu wa Mnyika, kufungia vyombo vya habari sasa hivi ni jaribio la kuleta hofu vyombo hivyo visiripoti kwa uhuru mchakato wa katiba mpya, hasa habari zenye mwelekeo wa kusema ukweli dhidi ya serikali au watawala wanaotaka kukwamisha na kuharibu mchakato huo.
CHANZO.Tanzania Daima
|
No comments:
Post a Comment