Pages

September 18, 2013

SHAHIDI WA KWANZA ATOA USHAHIDI HUKU USONI IKIWA IMEFUNIKWA NA KITAMBAA DHIDI YA MASHTAKA YANAYOMKABILI NAIBU RAIS WA KENYA KATIKA MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA ICC NCHI UHOLANZI.

 


Naibu Rais William Ruto alisindikizwa ICC na kikundi cha wabunge wa chama chake.
SHAHIDI wa kwanza kutoka upande wa mashtaka, amefika mbele ya mahakama ya kimataifa ICC kutoa ushahidi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya, William Ruto.

Mahakama inamlinda shahidi huyo kwa kutoonyesha sura yake.

Shahidi alianza kwa kuahidi kusema ukweli. Alielezea ambavyo familia yake ilijiunga na mamia ya watu wa kabila la Kikuyu wakiwa na magodoro yao pamoja na blanketi.

Walikuwa wanatafuta hifadhi katika kanisa la Assemblies of God Church katika kijiji cha Kiambaa karibu na mji wa Eldoret ambalo liliteketezwa na kusababisha vifo vya zaidi ya watu thelathini waliokuwa wamekimbilia usalama wao.

Hii ilikuwa baada ya wenyeji wa kabila la Kalenjin kuwaonya kuwa wangeadhibiwa vikali ikiwa wangekosa kupigia kura chama cha kisiasa cha ODM kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.

Shahidi huyo anatoa ushahidi wake akiwa nyuma ya kitambaa cha dirisha ndani ya mahakama huku kwenye TV sura yake ikiwa imezuiwa kuonekana ili kulinda usalama wake.

Naibu Rais William Ruto naye alitizama kutoka upande wa kushoto lakini sura yake imebanwa kabisa, hawezi kuonekana,.

Ushahidi wake unagusia siku ya tarehe mosi mwezi Januari. Aliambia mahakama kuwa maelfu ya watu walikuwa wanakuja kuizingira kanisa hiyo wakiimba huku wakiwa wamefunika nyuso zao kwa matope, wengi walikuwa wanavalia vitambaa kwenye vichwa vyao.

Alisema kuwa walikuwa wamejihami kwa mapanga na silaha zengine za kijadi , panga , shoka na viboko huku akisema kuwa aliweza kumtambua mwanasiasa mmoja miongoni mwa vijana hao kutoka chama cha ODM.

Ruto anakabiliwa na tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007-2008

Kesi dhidi ya Ruto na mshtakiwa mwenzake Joshua Arap Sang, ilianza tarehe 10 mwezi Septemba, baada ya wawili hao kutuhumiwa kuhusika na ghasia hizo, kwa njia ya kuzipanga na kutekeleza.

Kumekuwa na wasiwasi kuhusu mashahidi kujiondoa kwenye kesi hiyo wakihofia usalama wao. Mwishoni mwa wiki, mashahidi wanne walijiondoa katika kesi hiyo baada ya kuelezea wasiwasi kuhusu usalama wao ikiwa watatoa ushahidi mbele ya mahakama hiyo.

Wiki jana jaji mkuu kwenye kesi hiyo, aliiakhirisha kesi kwa sababu mashahidi hawakuwa wamefika kwenye mahakama hiyo kutoa ushahidi wao.

Rais Uhuru Kenyatta, anatarajiwa kufika mbele ya mahakama hiyo mwezi Novmba kwa mashtaka sawa na hayo. BBC.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...