Pages

September 29, 2013

MAGAZETI YA MWANANCHI NA MTANZANIA YAFUNGIWA NI BAADA YA KUDAIWA KUANDIKA HABARI ZA UCHOCHEZI.


SERIKALI imeyafungia kutochapishwa Magazeti ya MWANANCHI na MTANZANIA kuanzia 27 Septemba, 2013 kutokana na mwenendo wa magazeti hayo kuandika habari na makala za uchochezi na uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola hivyo kuhatarisha amani na mshikamano ulipo nchini. 

Gazeti la MWANANCHI limefungiwa kutochapishwa kwa siku kumi na nne (14) kuanzia 27 Septemba, 2013. Adhabu hii imetangazwa kwa Tangazo la Serikali (Government Notice ) Namba 333 la tarehe 27 septemba,2013.

Gazeti la MWANANCHI limepewa adhabu hiyo kutokana na hivi karibuni kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa amani, mfano tarehe 17 Julai, 2013 katika toleo Namba 4774 ilichapisha habari isemayo “MISHAHARA MIPYA SERIKALINI 2013” kwa kuchapisha waraka uliozuiliwa kwa matumizi ya vyombo vya habari waraka huo ulikuwa wa Siri haukupaswa kuchapishwa Magazetini.

Aidha, katika toleo la Jumamosi, tarehe 17 Agosti,2013 lilichapisha habari yenye kichwa kisemacho “WAISLAM WASALI CHINI YA ULINZI MKALI” habari hiyo ilikolezwa na picha ya mbwa mkali mwenye hasira.

Habari na picha hiyo ilitoa tafsiri ya kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka Mbwa katika maeneo ya ibada ya waumini wa dini ya kiislam. Jambo ambalo halikuwa la ukweli. 

Jeshi la Polisi katika doria siku hiyo halikupeleka mbwa katika maeneo ya Misikiti.

Serikali na jeshi la Polisi linaheshimu na kuzingatia maadili ya dini ya Kiislamu na kwa hiyo Jeshi lake haliwezi kupitisha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada.

Hivyo basi, kwa gazeti hili kuchapisha habari iliyokolezwa na picha ya mbwa ni uchochezi wa kulichonganisha Jeshi la Polisi na waumini wa dini ya kiislam mbwa ni najisi hapaswi kuingia katika maeneo ya ibada. 

Gazeti la MTANZANIA limefungiwa kutochapishwa kwa siku tisini (90) kuanzia tarehe 27 Septemba, 2013 kwa kuchapisha habari zenye uchochezi.

Gazeti hili limeonywa mara nyingi lirekebishe mtindo wake wa uandishi wa kichochezi na lizingatie maadili na Sheria na Kanuni za fani ya Habari.

Pamoja na kuonywa gazeti hili halikuonyesha kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Magazeti, mfano ;katika toleo na 7262 la 20 Machi,2013 liliandika habari yenye kichwa kisemacho “URAIS WA DAMU”,tarehe 12 Juni,2013,toleo Namba 7344 lilichapisha makala isemayo “MAPINDUZI HAYAEPUKIKI”. 

Aidha, siku ya Jumatano,tarehe 18 Septemba,2013 katika toleo Namba 73414 ukurasa wa mbele lilichapisha Kichwa cha habari kisemacho “SERIKALI YANUKA DAMU” taarifa hiyo ilikolezwa na picha zilizo unganishwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia kompyuta kutapakaza rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika.

Katika habari hiyo gazeti hilo limedai bila uthibitisho kuwa Jeshi la Polisi linahusika na wahanga waliomizwa na watu wasiojulikana kwa kumwagiwa tindikali na waliyovamiwa na kujeruhiwa vibaya. 

Vile vile gazeti hilo limeishtumu serikali kuwa goigoi katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi. Kwa ujumla wake habari hiyo ni ya kichochezi ina lengo la kuwafanya wananchi wavichukie vyombo vya ulinzi na usalama wavione kuwa haviwasaidii. 

Kutokana na makosa yalitajwa hapo juu serikali imelifungia gazeti la Mtanzania kutochapishwa kwa muda wa siku tisini (90) kwa Tangazo la Serikali Namba 332 (Government Notice No.332) la tarehe 27 septemba,2013,. Serikali inawataka wamiliki,wahariri na wanahabari kwa ujumla kuwa makini, kuzingatia weledi, miiko na madili yataaluma uandishi wa habari. 

Serikali inawataka wamiliki na hasa wahariri kuhakisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoviandaa vinazingatia taaluma, kuweka mbele maslahi ya taifa letu kwa kuwa na uzalendo wa hali ya juu. 

Serikali inavionya vyombo vya habari vinavyoutumia uhuru wa habari bila wajibu kuwa haitasita kuvichukulia hatua kali ikiwemo ya kuvifungia. Serikali haitakubali kuona vyombo vya habari kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani nchini. Imetolewa na

MKURUGENZI IDARA YA HABARI WIZARA YA HABARI,VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO 28 SEPTEMBA, 2013.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...