Pages

September 17, 2013

LOWASSA AMWAGIWA SIFA KWA KUFANIKISHA UPATIKANAJI WA MAJI KATIKA WILAYA YA KAHAMA NA SHINYANGA KUPITIA MRADI WA MAJI KUTOKA ZIWA VICTORIA.

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja amempongeza Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa jinsi alivyofanikisha utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Kahama na Shinyanga.


Alisema Lowassa pia alifanikisha ujenzi wa shule za sekondari za kata ambazo kwa kiasi kikubwa zimewezesha idadi kubwa ya watoto wanaomaliza elimu ya msingi kuendelea na masomo ya sekondari ingawa awali zilibezwa na kuchekwa na watu wasiopenda maendeleo.

Mgeja alitoa pongezi hizo juzi katika harambee iliyoongozwa na Lowassa kuchangia ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, jengo la utawala, nyumba mbili za walimu na choo katika Kanisa la African Inland Tanzania (AICT) wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga.

Lowassa katika harambee hiyo iliyokuwa na lengo la kuchangia Sh milioni 150 aliwezesha kupatikana Sh milioni 212 na kuvuka lengo.

Fedha taslimu zilizokusanywa ni Sh milioni 106, ahadi Sh milioni 85 na mifuko ya saruji 980 ikiwa na thamani ya Sh milioni 17.

Mgeja alisema bila juhudi za Lowassa ni wazi wakazi wa Mkoa wa Shinyanga wangekuwa wanaendelea kuhangaikia suala la upatikanaji wa maji safi na salama huku maji hayo yakiwanufaisha na kuwaendeleza watu wa mataifa mengine.

“Sisi watu wa Shinyanga tunakupongeza sana Mheshimiwa Lowassa kwa ujasiri uliouonyesha ulipokuwa waziri mkuu.

“Ulisimama kidete kwa kusema liwalo na liwe lazima watu wa Shinyanga na Kahama tupate maji kutoka Ziwa Victoria na kweli tuliyapata. Tunakushukuru sana na pia uliendesha kampeni kubwa ya ujenzi wa sekondari za kata.

“Wapo waliokuwa wakikubeza katika suala la sekondari za kata, leo hii hawana la kusema na hata hawa wanaobeza juhudi zako za kuendesha harambee mbalimbali za maendeleo wanahangaika bure, hawawezi kukuzuia maana wewe sasa unafanana na kasi ya maji ya mto Ruvu ambayo hayazuiliki,” alisema Mgeja. MTANZANIA

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...