Mkurugenzi wa Teknolojia ya Nyuklia na Huduma za Ufundi wa TAEC,Dk.Remigius Kawala alifafanua jambo kwa waandishi wa habari.
Tume ya Nguvu za Atomu nchini (TAEC) kwa kushirikiana na Shirika la
Kimataifa la Nishati ya Nyuklia (IAEA), wamezindua mkakati wa kiusalama
unaolenga kudhibiti nyenzo za nyuklia na vifaa vyenye mionzi visitumike kwa
madhumuni ya kihalifu wakati wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON)
itakayofanyika nchini mwaka 2027.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Najat Kassim
Mohammed wakati wa ufunguzi wa warsha ya kitaifa ya siku tano inayolenga
kuandaa na kutekeleza hatua za usalama wa nyuklia kwa matukio makubwa ya umma.
Profesa
Najat amesema kuwa ingawa uwezekano wa kutokea kwa dharura au shambulio la
kiusalama linalohusisha nyuklia ni mdogo, madhara yake yanapotokea huwa ni
makubwa mno yakiwemo hofu kubwa kwa umma, kuvurugika kwa huduma za kijamii
pamoja na mdororo mkubwa wa kiuchumi.
Ameongeza
kuwa michuano hiyo ya AFCON 2027 itakayofanyika hapa nchini na nchi za Kenya na
Uganda itawaleta pamoja wachezaji,
viongozi, mashabiki na waandishi wa habari duniani, jambo linalohitaji mipango
thabiti ya usalama inayozingatia tathmini ya kina ya viashiria vya hatari.
"Usalama wa nyuklia kwenye matukio makubwa kama hili hauwezi kuwa
jukumu la taasisi moja pekee. Unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Jeshi la
Polisi, mamlaka za forodha, uhamiaji, zimamoto, sekta ya afya na uongozi wa
viwanja vya michezo," amesema Profesa Najat.
Tanzania imeelezwa kupiga hatua kubwa kwa kuweka vifaa vya kisasa vya
kugundua mionzi kwenye mipaka na maeneo ya kimkakati pamoja na kutoa mafunzo
kwa maafisa wa mipakani, hata hivyo, mapungufu madogo yaliyopo yatafanyiwa kazi
ili kuendana na vigezo vya kimataifa vya IAEA.
Kwa upande wake, Mtaalamu kutoka IAEA, Lacina Saro amesema kuwa maandalizi
ya usalama wa nyuklia ya kiwango hiki yanapaswa kufanywa kwa umakini mkubwa,
kufanyiwa majaribio ya kutosha na kutekelezwa kwa kujiamini na timu za kitaifa
zilizofundishwa vizuri.
Saro aliongeza kuwa warsha hiyo ni muendelezo wa msaada wa IAEA ambapo
mnamo Aprili 2025 watalaamu kutoka shirika hilo walifanya tathmini ya mahitaji
ya Tanzania na Julai mwaka jana ujumbe wa wataalamu wa Tanzania ulitembelea
nchi ya Morocco kujifunza kwa vitendo namna mifumo hiyo inavyofanya kazi.
Alifafanua kuwa katika kipindi cha mafunzo hayo,washiriki hawatasikiliza
mihadhara tu, bali wataingia viwanjani kufanya mazoezi ya vitendo ya ugunduzi
wa mionzi, upekuzi, utambuzi wa kengele za hatari na jinsi ya kukabili vifaa hatarishi kwenye
uwanja wa michezo.
Warsha hiyo inatarajiwa kuhitimishwa kwa zoezi kubwa la uwanjani
litakalofuatiwa na uandaaji wa mpango kazi wa kitaifa wa utekelezaji
utakaokabidhiwa kwa serikali ya Tanzania kwa usimamizi wa karibu wa Mkurugenzi
wa Kitengo cha Usalama wa Nyuklia cha IAEA, Elena Bubo.
Naye Mkurugenzi wa Teknolojia ya Nyuklia na Huduma za Ufundi wa
TAEC,Dk.Remigius Kawala amesema kitaalamu teknolojia ya nyuklia ina uwezo wa
kutumika kwa manufaa makubwa sana lakini pia inaweza kutumika katika njia
zisizo za manufaa na kusababisha hatari,hofu na kutishia usalama.
‘Hivyo shirikisho la soka duniani (FIFA) na shirikisho la soka barani
Afrika (CAF) wameweka sehemu ya mionzi kama takwa la kiusalama wakitutaka
tuzingatie shughuli zetu zote zinazohusu matukio ya umma ikiwemo michezo yote
yazingatie usalama wa mionzi na nyuklia,”amesema Dk.Kawala
Washiriki wa warsha hiyo wanatoka Ofisi ya Rais wa Tanzania,Ofisi ya Rais
wa Zanzibar,Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ),Jeshi la Polisi,Jeshi la
Zimamoto na watumishi wa Taec .
Post a Comment