.jpeg)
SHIRIKISHO la Viwanda Tanzania (CTI) limetangaza kuwa Tuzo za Rais za Wazalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA) kwa mara ya 19, jukwaa kubwa nchini Tanzania la kutambua mafanikio ya viwanda, litafanyika Agosti 24 mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CTI, Hussein Sufian, alisema kaulimbiu ya mwaka huu, “Green Elegance — Celebrating Sustainable Manufacturing Practices,” inaonesha mabadiliko katika kile ambacho PMAYA inatambua; si tu uzalishaji wa viwanda, bali pia uendelevu, uwajibikaji na ustahimilivu unaosimamia uzalishaji huo.
Alisema jioni hiyo itashuhudia zulia la kwanza la kijani (Green Carpet) nchini Tanzania, likichukua nafasi ya zulia la kawaida jekundu, ikiwa ni ishara ya dhamira ya pamoja ya sekta kuelekea ukuaji endelevu wa viwanda.
“Kwa miaka kumi na tisa, PMAYA imekuwa ikieleza hadithi ya viwanda vya Tanzania katika hali yake bora zaidi. Mwaka huu, tunaeleza hadithi kamili zaidi, inayotambua si tu kile wazalishaji wetu wanachozalisha, bali pia jinsi wanavyozalisha kwa uwajibikaji. Green Elegance si kaulimbiu tuliyoikopa; ni mwelekeo ambao sekta hii tayari inaufuata, na PMAYA ipo kutambua uongozi huo,” alisema.
Pia kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 19 ya PMAYA, mbali na washindi wa kategoria za tuzo, PMAYA itatangaza Mabalozi sita wa ESG (ESG Ambassadors), ambao wameainishwa kupitia tathmini ya CTI kama viongozi katika utekelezaji wa masuala ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora.
Alisema mabalozi hao wameainishwa kupitia tathmini ya moja kwa moja ya utendaji wao viwandani na watatumika kama mabalozi wa sekta kwa muda wa miezi 12. Kundi hilo litakuwa msingi wa kuanzishwa kwa tuzo mpya ya kudumu ya Mzalishaji Bora wa Mazingira wa Mwaka (Green Manufacturer of the Year), itakayoanza kutolewa katika PMAYA ya 20.
Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Mhandisi Leodegar Tenga, alisema kupitia mradi wa ESG, timu ya CTI ilitembelea viwanda mbalimbali nchini na kushuhudia utekelezaji wa masuala hayo kwa vitendo.
“Balozi sita wa ESG tutakaowatangaza waliainishwa kupitia mchakato huo. Huu ni mwanzo wa njia ya kudumu ya kutambua uzalishaji endelevu viwandani hapa Tanzania, na tunatarajia kushiriki hadithi zao tarehe 24 Agosti,” alisema.
Alisema PMAYA ya 19 inaungwa mkono na wazalishaji na kampuni mashuhuri za Tanzania, ikiwemo Tanzania Cigarette Company (TCC), Tanzania Breweries Limited (TBL), Chemi Cotex Limited na Africab Group (Kilimanjaro Cables).
CTI imezihimiza kampuni nyingine zenye nia ya kushirikiana katika PMAYA ya 19 kuwasiliana na Sekretarieti ya CTI kwa maelezo zaidi kuhusu udhamini.
Tenga alisema tuzo hizo zilitokana na mashindano kati ya wazalishaji yaliyoanzishwa mwaka 2005 na kuandaliwa na CTI kwa lengo la kutambua, kutathmini na kuenzi umuhimu na mchango wa sekta ya viwanda katika maendeleo ya nchi.
“Siku hii ni ya muhimu sana kwetu kwa sababu ni fursa ya pekee tunayoipata mara moja kwa mwaka, kwa pamoja, ili kutambua, kutathmini na kuenzi umuhimu na mchango wa Sekta ya Viwanda katika maendeleo ya uchumi wa Taifa letu,” alisema.
Alisema katika miaka 19 tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo, maboresho mbalimbali yamefanyika, ikiwemo kuongeza wigo wa washiriki kwa kuhusisha sekta za uzalishaji 26, ili kujumuisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.
Aidha, alisema washindi wa tuzo hizo hupatikana kwa kuzingatia mchango wa mzalishaji katika uchumi, maendeleo na uwekezaji katika teknolojia ya kisasa inayojali na kutunza mazingira, mauzo ya nje, afya na usalama wa mazingira ya kazi, pamoja na mchango katika kuendeleza jamii inayowazunguka (Corporate Social Responsibility) na vigezo vingine.
Tuzo hizo zinaendelea kuwa jukwaa kuu la Tanzania katika utambuzi wa viwanda, uhamasishaji wa uwekezaji na majadiliano baina ya sekta binafsi na Serikali.


Post a Comment