Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia mradi wa Kilimo, Chakula na Lishe (FoodLand) umebaini kuwa wakazi wengi wa vijijini hawatumii mayai wala maziwa katika lishe yao, licha ya kufuga kuku, ng’ombe, na mbuzi.
Profesa Susan Nchimbi, mmoja wa watafiti wa mradi huo, alitangaza matokeo ya utafiti huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, akieleza kuwa utafiti ulifanyika katika Wilaya za Kilombero na Mvomero, hasa katika kijiji cha Kinda.
Amesema Utafiti huo ulifanywa kwa njia mbalimbali, ikiwemo madodoso, na umebaini kuwa wananchi wengi wanauza mayai kwa ajili ya kipato badala ya kuyatumia kwa lishe.
Zaidi ya hayo, imegundulika kuwa wananchi wa vijijini hawanywi maziwa kwa sababu wengi hawafugi ng’ombe au mbuzi wa maziwa. Utafiti huu pia umechunguza mbegu bora za maharage zenye madini muhimu, mbinu za ufugaji wa samaki, na uhifadhi wa mazao kama maparachichi, huku ukilenga pia kuboresha elimu ya lishe kwa jamii.
Alisema kuwa katika utafiti walioufanya katika kijiji cha Kinda walibaini kuwa wananchi wa kijiji hicho wanalima Kwa wingi maharage hivyo kupitia utafiti huo wameweza kuja na aina nne za mbegu za maharage ambazo zimeongezewa madini ya chuma na zinki.
Alitaja aina za mbegu hizo maharage ni PIC 130, Nuha 629, Nuha 660 na Mashamba na tayari aina hizi zote zipo kwenye hatua mbalimbali za kufanyiwa majaribio kwenye Mamlaka mbalimbali ikiwemo TOSCI," amesema Prof. Nchimbi.
Profesa Nchimbi alisema utafiti ulilenga pia kwenye ufugaji wa samaki Kwa kuangalia chakula bora cha samaki wa kufungwa lakini pia namna bora ya kuhifadhi mazao hasa matunda mbalimbali yakiwemo maparachichi.
Awali akitoa taarifa ya utafiti huo mmoja wa washiriki wa utafiti huo Prof. Dismas Mwaseba alisema utafiti huo ilianza mwaka 2020 na unafanywa kwenye nchi sita ambazo ni Morocco, Tunisia, Ethiopia, Kenya, Uganda na Tanzania ambapo Kwa Tanzania utafiti huo umefanyika katika mkoa wa Morogoro wilaya ya Kilombero na Mvomero lakini pia katika mkoa wa Dar es Salaam.
Profesa Mwaseba alisema mradi huo umelenga kwenye masuala ya kilimo, elimu, afya na lishe ambapo kwenye upande wa elimu wamebaini kuwa vijana wengi wa kwenye kijiji cha Kinda hawajui kusoma hali ambayo inawafanya washindwe kusoma vipeperushi na majarida mbalimbali yanayoeleza masuala ya lishe na hivyo kujikuta wakishindwa kuzingatia masuala ya lishe.
Post a Comment