Pages

April 4, 2018

KUELEKEA MTIHANI WA TAIFA MEI 2018 WANAFUNZI 1003 KIDATO CHA SITA SIMIYU WAPIGA KAMBI YA KITAALUMA


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wanafunz wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 za Mkoa huo wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani Maswa.
Baadhi ya Wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 za Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani Maswa.
Baadhi ya walimu mahiri 40 waliochaguliwa kufundisha na kuwaandaa wanafunzi wa kidato cha sita (kutoka shule 11 mkoani Simiyu) na Mtihani wa Taifa utakaofanyika mwezi Mei mwaka huu, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Kambi ya  Kitaaluma kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani Maswa.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe.Dkt.Seif Shekalaghe akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 za Mkoa wa Simiyu wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani humo. 
Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl.Julius Nestory akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 za Mkoa huo wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani Maswa.




Na Stella Kalinga, Simiyu

Takribani wanafunzi 1003 wa Kidato cha sita kutoka shule za Sekondri 11 zenye kidato cha tano na sita Mkoani Simiyu, wamepiga kambi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa na Shule ya Sekondari Binza, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa ambao unatarajia kufanyika mapema mwezi Mei mwaka huu.

Akifungua kambi hiyo Aprili 03 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa wilayani Maswa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema ili mkoa huo uweze kushindana na kufanya mageuzi katika Uchumi ni lazima kuwekeza katika elimu.

“Kama wanafunzi wetu wanakaa makambi ya michezo ngazi ya kata, wilaya, mkoa na Taifa kwa nini wanafunzi hao hao wasikae kambi kwa ajili ya maendeleo ya taaluma; tukitaka kufanya mageuzi ya Mkoa huu ni lazima tuweke nguvu kwenye elimu, maeneo yenye uchumi mzuri wamewekeza sana  kwenye elimu” alisema Mtaka. Aidha, Mtaka awataka wanafunzi wote wa kidato cha sita kuwasikiliza walimu watakaokuwa wakiwafundisha na kuwaelekeza na akawataka kujiamini wakati wa mtihani wao wa mwisho.

Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwl. Julius Nestory amesema Mkoa huo una mpango wa kuondoa daraja la nne na sifuri katika matokeo ya Mitihani ya Taifa, hivyo wanayo matumaini makubwa kuwa, kupitia makambi hayo ya kitaaluma Mkoa utaweza kufikia lengo hilo kwa matokeo ya kidato cha sita mwaka 2018.

“ Tumeamua kuwaleta pamoja wanafunzi ili waweze kunyanyuka kama kundi moja la mama mmoja (Simiyu) na kuweza kupandisha ufaulu, tumewaleta hapa ili kuweza kunyanyua morali wa kazi kuwaleta pamoja anayeweza na asiyeweza ili tuweze kunyanyuka pamoja kama kundi” alisema Mwl.Nestory.

Amesema katika siku 10 za kambi wanafunzi wa kidato cha sita watapitishwa katika miiko ya watahiniwa wakati wa mitihani kwa kuwa mkoa wa Simiyu unapinga suala la udanganyifu kwenye mitihani, watapitishwa katika maswali na mada ambazo baada ya tathmini ilionekana hawakufanya vizuri katika mtihani wa kanda na mtihani wa Mkoa.

Akizungumza kwa niaba ya walimu mahiri 40 ambao watakuwa wakiwafundisha na kuwasaidia wanafunzi hao, Mwl.Majaliwa Chibona wa Shule ya Sekondari Mwandoya wilayani Meatu amesema, wamejipanga kuwasaidia wanafunzi katika kuwapa mbinu na mikakati mbalimbali itakayowasaidia kujiandaa na mitihani wao wa mwisho ili waweze kufaulu.

Nao baadhi ya wanafunzi wamesema kambi hiyo itawasaidia sana katika kuwajengea hali ya kujiamini kwa kuwa watasaidiwa na walimu katika maeneo yote yanayoonekana magumu kwao, watasaidiana wa kwa wao kupitia makundi na watapewa mbinu zitakazowasaidia kujiandaa vema na hatimaye kufanya vizuri.

No comments:

Post a Comment