Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii
MKURUGENZI
Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Lauraean Bwanakunu pamoja na mafanikio
ambayo wameyapata katika kutekeleza majukumu yao ya kununua, kusambaza,
kutunza na kusambaza dawa na vifaa tiba, changamoto inayowakabili ni ya
ununuzi wa vifaa vya kitaalam toka wazalishaji.
Ametaja
baadhi ya vifaa hivyo ni vya macho, meno, moyo na figo ambapo
vinaagizwa kwa uchache na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete
(JKCI),Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH) na ORIC.
Azungumza
leo jijini Dar es Salaam mbele ya Rais John Magufuli wakati wa
uzinduzi wa magari mapya ya msaada ya kusambaza dawa ambayo yametolewa
na Global Fund kwa MSD, Bwanakunu amesema wazalishaji wa vifaa hivyo
wanaona oda ni ndogo na hivyo wamekuwa na wakati mgumu kupata.
Amemhakikishia
Rais Magufuli kuwa, MSD wamejipanga kukabiliana na changamoto hiyo na
mwezi ujao watazungumza na Shirika la IDA lililopo Denmark na wengine
ili kuwakusanyia vifaa hivyo pamoja na nchi nyingine kwa lengo la
kuwapunguzia gharama za manunuzi.
Amesema kampuni hizo hufanya manunuzi ya nchi mbalimbali ikiwemo umoja wa mataifa na hivyo wanataka kufaidika na mfumo huo.
Bwanakunu
amemueleza Rais Magufuli , changamoto ya pili wanayokabiliana nayo ni
ya maoteo kutokana na kutokuwa sahihi na kufanya suala la ununuzi kuwa
la kubahatisha.
Akizungumzia
kuongezeka kwa bajeti ya kununua dawa kutoka Sh.bilioni 31 hadi
Sh.bilioni 250, Bwanakunu amesema yale yalikuwa maajabu na kama ndoto na
kila mtu kwenye mnyororo wa ugavi alichanganyikiwa ghafla.
"Kuna
zahanati ilikuwa inapata dawa za Sh.400,000 kwa mwaka na sasa inapata
Sh.milioni 10. Furaha hii haikuwa kwa vituo vya kutolea huduma za afya ,
watumishi wa afya lakini zaidi sisi watumishi wa MSD umetuondolea kero
ya Watanzania kudhani mtu akiumwa na mbwa au nyoka basi shida ni MSD
wakati hatuna fedha za kununua dawa hizo.
"Kwa
sasa tunatembea kifua mbele .Aidha ni muhimu pia tukafahamu kuwa MSD
inanunua dawa zenye jumla ya Sh.bilioni 460 kwa fedha za Serikali na
wafadhili kila mwaka ni Sh.bilioni 28.Tena hizi ni za miaka miwili tu
ndizo zinazotumika kwa viwanda vya ndani kutokana na viwanda vya
uzalishaji wa dawa kuwa vichache na uwezo wa kuhudumia mahitaji ya
MSD,"amesema.
Amefafanua
kwa wastani wananunua dawa za Sh.bilioni 21 kwa mwezi na kutumia nafasi
hiyo kumueleza Rais ni kiasi gani cha fedha kinakwenda nje ya nchi.
Bwanakunu
amemwambia Rais Magufuli kuwa, MSD imejipanga kuhakikisha magari hayo
mapya yanaleta tija iliyokusudiwa na kueleza wamechukua hatua kadhaa
kuhakikisha magari hayo yanafanya kazi kwa ufanisi na yanakuwa katika
hali nzuri.
Kwa
upande wake Rais Magufuli akizungumzia MSD ameipongeza kwa kazi nzuri
ambayo ameifanya na kwamba anaridhishwa na utendaji kazi wao na kutumia
nafasi hiyo kumhakikishia Bwanakunu kuwa hata akitaka kupandisha
mishahara ya watumishi atakuwa tayari kukubali maombi yao.
Amesema
anakumbuka kuna wakati mkurugenzi huyo wa MSD alikuwa anapigwa madongo
lakini amemhakikishia achape kazi na yeye ndio mkurugenzi huku
akisisitiza kuelezea namna ambavyo afurahishwa na taasisi hiyo
inayofanya kazi kizalendo.
"MSD
mnafanya kazi nzuri sana, nimesema kutoka moyoni mnanifurahisha na
lazima niwapongeze.Mimi ni mgumu kupongeza hivyo ukiona natoa pongezi
mjue nimeridhishwa na mnachokifanya.
"Endeleeni
kuongeza maduka ya dawa na kama watumishi ni wachache basi ongezeni
wengine.Msikubali kuwatumia watu wa halmashauri maana nawajua kule kuna
wajanja wengi watawakwamisha.Tamisemi iko chini yangu hivyo
nawajua.Msifanye kazi na halmashauri fanyeni wenyewe kwa kutumia
watumishi wenu,"amesema Rais Magufuli.
Mkurugenzi
Mkuu wa Bohari Kuu ya Madawa, Laurean Bwanakunu akizungumza wakati wa
hafla ya kukabidhi magari 181 yatakayokuwa yakisafirisha vifaa tiba na
vitendanishi katika Mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini. Hafla hiyo
ilifanyika Jumatatu Machi 26, 2018 katika Ofisi za MSD Keko Mwanga
Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment