Shirika
la Kimataifa la Save The Children limetoa msaada wa gari aina ya Toyota
Landcruiser katika Halmashauri ya Mji Kahama mkoa wa Shinyanga kwa
ajili ya kusaidia ufuatiliaji wa matukio ya ukatili na unyanyasaji wa
watoto.
Mbali
na kukabidhi gari hilo, Save The Children pia imekabidhi pikipiki mbili
aina ya Boxer, Kompyuta mpakato moja (Laptop) na Ipad moja kwa shirika
la KIWOHEDE linalotekeleza mradi wa kupambana na mila na desturi
kandamizi kwa watoto katika halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama.
Hafla
fupi ya makabidhiano hayo imefanyika leo Ijumaa,Desemba Mosi,2017
katika viwanja vya Halmashauri ya Kahama Mji wilayani Kahama,mkoani
Shinyanga.
Akizungumza
wakati wa kukabidhi,gari,pikipiki,laptop na Ipad, Meneja wa Shirika la
Save The Children mkoa wa Shinyanga,Benety Malima alisema vifaa hivyo
vitasaidia katika utendaji kazi kupambana na ukatili dhidi ya watoto.
“Leo ni siku ya Ukimwi duniani na sisi tumeona tushiriki katika siku hii
ili kuonesha kwamba ukatili ni njia mojawapo ya maambukizi ya Virusi
vya Ukimwi, Mradi wetu umeisha lakini mapambano dhidi ya ukatili kwa
watoto yanaendelea, kwa hiyo tunakabidhi gari hili ili mapambano
yaendelee”,alisema Malima.
“Vifaa hivi likiwemo gari hili vitakwenda kufanya kazi za mapambano
dhidi ya ukatili wa watoto,tunaomba likafanye kazi kama ilivyokusudiwa
ili kuhakikisha kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinaisha mkoani
Shinyanga”,aliongeza Malima.
Aidha alisema tangu mwaka 2014 walikuwa wanatekeleza mradi wa Ukatili
dhidi ya watotokatika halmashauri ya Mji Kahama,Manispaa ya Shinyanga na
Shinyanga Vijijini na baada ya mradi kuisha mwaka huu wametoa gari
hilo kwa halmashauri ya Kahama Mji kwani imekuwa mstari wa mbele katika
mapambano ya ukatili dhidi ya watoto.
“Tunawapongeza sana halmashauri ya Kahama Mji kwa kuwa mfano mzuri
katika vita dhidi ya ukatili wa kijinsia na watoto,wameonesha hatua za
ziada,waliamua kuubeba mradi huu na kuufanya wao,tunaamini wataendeleza
mapambano”,alisema Malima.
Hata hivyo,Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Kahama Mji,Robert Kwela
aliuhakikishia uongozi wa shirika hilo kuwa watalitunza na kulitumia
gari hilo kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Mradi wa wenzetu Save the Chidren kuisha muda wake, wamekabidhi vifaa
hivi ili shughuli za mapambano ya ukatili dhidi ya watoto
ziendelee”,alisema.
“Baada ya mradi kuisha,ili shughuli zilizokuwa zinatekelezwa ziweze
kuendelea,utaratibu huwa ni lazima mashirika husika yaendelee kuona
namna ya kujenga uwezo kwenye taasisi ambazo walikuwa wanafanya nazo
kazi ili shughuli zilizokuwa zimeanzishwa ziweze kuendelezwa”,alifafanua
Kwela.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa halmashauri ya Kahama Mji,Abel Shija
alilishukuru shirika hilo kwa ushirikiano ambao limekuwa likiwapa na
kuongeza kuwa suala la ukatili dhidi ya watoto linapaswa kufanywa kwa
vitendo kama vile Save the Children walivyoonesha kwa kutoa vifaa hivyo
vya kutendea kazi.
Naye Mratibu wa Mradi wa kupambana na mila na desturi kandamizi kwa
watoto Shirika la KIWOHEDE, Lulu Makwale alilishukuru shirika la Save
the Children kwa kuwapatia msaada wa pikipiki mbili,laptop na Ipad
vifaa ambavyo vitasaidia katika utekelezaji wa mradi huo katika
Halmashauri ya Ushetu.
Makabidhiano hayo pia yalishuhudiwa na Katibu tawala mkoa wa
Shinyanga,Albert Msovela alilishukuru shirika hilo kwa msaada wa gari na
kuongeza kuwa litasaidia katika kupunguza changamoto ya usafiri katika
halmashauri hiyo.
Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa Shinyanga,Benety Malima
akizungumza wakati akikabidhi gari katika halmashauri ya Kahama Mji na
pikipiki,laptop na Ipad kwa shirika la KIWOHEDE leo katika viwanja vya
Kahama Mji,wilayani Kahama.Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa
halmashauri ya Kahama Mji,Abel Shija. Kulia ni Mratibu wa ulinzi wa
mtoto,haki za watoto na utawala shirika la Save The Children,Alex Enock
akifuatiwa na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Kahama Mji,Robert
Kwela.
Gari na pikipiki zilizotolewa na shirika la Save The Chilren vikiwa nje ya ofisi za halmashauri ya Kahama Mji.
Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa Shinyanga, Benety Malima
(kulia) akimkabidhi funguo za gari Mwenyekiti wa halmashauri ya Kahama
Mji,Abel Shija.
Katikati ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Kahama Mji,Abel Shija akionesha
funguo za gari lililotolewa na shirika la Save the Children kwa ajili
ya kuendeleza mapambano dhidi ya ukatili wa watoto.

Post a Comment