Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.
Leo
Novemba 13, 2017 Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam,
imemuhukumu msanii maarufu wa filamu nchini, Elizabeth Michael Kimemeta
kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kupatikana na hatia
ya mauaji ya bila kukusudia ya msanii mwenzake marehemu Steven Kanumba.
Hukumu
hiyo imesomwa na Jaji Sam Rumanyika ambaye amesema, ameridhika na
ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa mashitaka na wazee wa baraza
waliotoa maoni yao kuwa kweli mshtakiwa Lulu aliuwa bila ya kukusudia.
Alisema
Aprili 12, 2012 ndio ilikuwa mara ya kwanza kwa Lulu kufikishwa
Mahakamani ambapo alifikishwa katika mahakama ya mkoa wa Dar es Salaam,
ambayo ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kujibu tuhuma za
mauaji ya marehemu Kanumba. Lakini baadae baada ya kusota rumande kwa
takribani miezi kumi, Lulu alibadilishiwa mashitaka na kushitakiwa kwa
mauaji ya bila kukusudia, shtaka lililomuwezesha kuwa nje kwa dhamana
hadi leo.
Akisoma
hukumu hiyo Jaji Rumanyika amesema, kesi hiyo imejikita katika ushahidi
wa mazingira na kwamba mshtakiwa mwenyewe alikubali kwamba yeye ndio
alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemeu Kanumba ambaye alikuwa ni mpenzi
wake kwa miezi minne . Alisema ili kuthibitisha kesi hii ni watu wawili
pekee ndio wenye uwezo huo ambao ni mshitakiwa na marehemu.
‘’Kwa
sababu hiyo, mshitakiwa anatakiwa kutoa maelezo ya kina
yanayojitosheleza na akishindwa kufanya hivyo ataonekana kwamba yeye
ndiye muuaji. Ushahidi wa mazingira unaweza kutumika kama msingi pekee
endapo utaendelea kumnyooshea kidole mshitakiwa,’’ alisema Jaji
Rumanyika.
Alisema
maelezo aliyoyatoa mshitakiwa yanakidhi viwango na vigezo kwa kuwa
alikubali kwamba walikuwa na mzozo na kupigwa. Alisema ‘’kwa maoni yangu
kuanguka au kudondoka kwa mtu mmojawapo katika ugomvi atakuwa
amesukumwa au kumkaba mwenzake.’’
Alisisitiza
kuwa mshitakiwa anajukumu la kutoa maelezo ya kutosha kuhusu tukio
lililotokea na kwamba alijikanganya wakati akitoa utetezi wake.
Alieleza
kuwa Lulu aliiambia mahakama marehemu Kanumba alikuwa amelewa na
desturi ya mlevi mara nyingine huanguka, lakini yeye alieleza kuwa
aliburuzwa na kurudishwa chumbani hivyo kama alikuwa mlevi hakueleza
kama wakati wanakimbizana alianguka.
Pia
alisema maelezo yaliyotolewa na Josephine Mushumbuzi yanaacha maswali
mengi kwa sababu hayana hadhi ya cheti cha daktari na kwamba Daktari
Paplas Kagaiga ndiye aliyethibitishwa na mshitakiwa mwenyewe pamoja na
mdogo wa marehemu, Seth kuwa ndiye daktari wa familia na kwamba ndiye
aliyepaswa kujua historia ya marehemu ikiwemo afya na maradhi. Hata
hivyo, mshitakiwa kwa kuwa alikuwa na mahusiano ya kimapenzi
alitazamiwa ajue maradhi ya marehemu lakini kwenye utetezi wake
hajaeleza.
‘’Maelezo
yake yanakinzana na hekima ya kawaida kwa sababu hata pale marehemu
alipokuwa akimpiga na kumtishia kumuua kwa panga hakuthubutu kufanya
chochote, kumsukuma wala kumrudishia bali alichukua taratibu zile za
kibiblia kwamba akupigae shavu la kulia mgeuzie na la kushoto,’’ alisema
na kuongeza;
‘’Akiwa
mtu wa mwisho kuwa na marehemu hakutoa maelezo ya kina na ya
kutosheleza ni kitu gani kilitokea hadi kukutwa na mauti,’’alisema.
Jaji
Rumanyika alisema wakati tukio linatokea mshitakiwa alikuwa mtoto wa
miaka 17, lakini alikubali kuitwa mke. Alisema mtoto wa umri kama wake
ambaye ameweza kuyafanya ya watu wazima sio mmoja wa wale watoto
waliolengwa kulindwa na sheria ya watoto hivyo kwa maoni yake, kuwa
mtoto wa umri na kuweza kufanya kama alichofanya Lulu halafu akakingwa
na sheria ya watoto basi, tutegemee watoto wengi kufanya hayo na
kujikinga na mwamvuli wa utoto.
Alifafanua
kuwa watunzi wa sheria ya watoto walikuwa na maana ya umri na sio
ukomavu kama amesherehekea sikukuu za kuzaliwa ngapi,kukua na kuzeeka ni
jambo moja na ukomavu ni jambo lingine.
‘’Kama
wanasheria na majaji wataendelea kuwa na fikra na mawazo yaliyosimama
huku jamii ikiwa inaendelea kwa kasi, basi watashindwa kuonesha kwa
vitendo utawala wa sheria nami sitaki kuwa wa kwanza,’’ alisema.
Pia alisema mahakama ikiacha kufanya yale ambayo sheria hazijaruhusu, lazima jamii isiyokuwa na maendeleo kisheria.
‘’Hivyo
ninajiridhisha kuwa kifo cha marehemu kimetokana na ugomvi ndio maana
mshitakiwa alishitakiwa kwa kosa la mauaji bila kukusudia. Mshitakiwa
alisema marehemu alikuwa na wivu uliozidi mipaka ambao haukuwa na maana
lakini hakuna mchezo usiokuwa na kanuni na katika mapenzi wivu ni moja
ya kanuni zake,’’ alisisitiza Jaji Rumanyika.
Alieleza
kuwa kama Lulu alishajiingiza katika mapenzi huku akifahamu kwamba
marehemu alikuwa na wivu kumbe hata alivyoanza kumshuku kwa simu,
alitakiwa aachane nayo ili kuepusha ugomvi lakini yeye aliamua liwalo na
liwe.
Alisema,
kuna wivu wa maendeleo ambao huzaa maendeleo lakini wivu wa mapenzi
huleta maangamizi. Kabla ya kutolewa adhabu, Wakili wa Serikali, Faraja
George alidai hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma ya Lulu, lakini kwa
vile mashitaka hayo yamehusisha uhai wa mtu, mahakama itoe adhabu
stahiki dhidi ya mshitakiwa.
Wakili
wa utetezi, Peter Kibatala alidai mshitakiwa anategemewa na familia
yake ambao ni mama na mdogo wake, pia ni balozi wataasisi mbalimbali
ambazo zinamuwezesha kiuchumi.
Pia
alisema ataangaliwa kwa macho dhihaka na jamii inayomzunguka na kwamba
Lulu amebadilika tangu tukio lilipotokea hivyo anaamini ataendelea
kubadilika endapo atapata kifungo cha nje, hivyo aliomba asipewe adhabu
kali.
Katika
kesi hiyo, ambayo Lulu anadaiwa kumuua Kanumba Aprili 7, 2012 maeneo ya
Sinza Vatican jijini Dar es Salaam, upande wa serikali uliwakilishwa na
Mawakili, Faraja, Yusuph Abood na Batilda Mushi huku upande wa utetezi
uliwakilishwa na Kibatala na Omary Msemo.



Post a Comment