EAC YAJIPANGA KUDHIBITI MAGONJWA YA MLIPUKO NA YANAYOAMBUKIZA

Arusha.Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) kwa kushirikiana na shirika la maendeleo la kimataifa la Ujerumani(GIZ) kupitia mradi wa kudhibiti na kupambana na magojwa ya mlipuko utawakutanisha wadau na wataalamu wa afya kujifunza mikakati ya kukabiliana na magonjwa hayo baada ya uzoefu walioupata kwenye nchi za Afrika Magharibi.

Watalaamu mbalimbali 500 kutoka nchi za Afrika Mashariki mwaka 2014 na 2016 walienda katika nchi za Afrika Magharibi kusaidiana na watalaamu wa afya kupambana na ugonjwa hatari wa Ebora ambao ulisababisha vifo vya watu na kuacha makovu.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Mawasiliano wa EAC,Richard Owora ilisema tangu wataalamu hao tangu warejee kwenye nchi zao utaalamu,maarifa na uzoefu walioyapata haujawekewa mfumo maalumu wa kuuweka kwenye maandishi kwaajili ya kuutumia pindi milipuko hiyo itakapotokea kwenye nchi za EAC.

"Kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ambao ni GIZ na benki ya maendeleo ya Ujerumani(KfW) Novemba 6 hadi 8 mwaka huu tutawakutanisha watalamu hao nchini Kenya kuona namna tunavyoweza kutumia maarifa ya wenzetu waliojitoa mhanga kwenda kuokoa maisha ya ndugu zetu kuona namna tunavyoweza kuyatumia wakati ujao," ilisema taarifa hiyo

Mkutano huo utasaidia kuhakikisha nchi za Afrika Mashariki zinakua na uwezo wa kujiandaa kukabiliana na magonjwa ya milipuko na yanayoambukizwa ili kulifanya eneo zima la EAC kuwa salama.

Mwaka 2014 hadi 2016 nchi za Liberia,Guinea na Siera Leone zilishambuliwa na ugonjwa wa Ebola ambao ulisababisha vifo vya watu na kuathiri mfumo wa kiuchumi wa nchi hizo.

Mganga Mkuu wa Jiji la Arusha,Dk Simon Chacha alisema mkutano huo utazisaidia nchi za Afrika Mashariki kujenga uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na yanayoambukiza ili kuhakikisha nchi zote zinakua tayari kukabiliana magonjwa hayo.

Post a Comment

Previous Post Next Post