Na Dotto Mwaibale, Missenyi Kagera
WAKULIMA
wilayani Missenyi Mkoani Kagera wametakiwa kuyatumia matunda ya tafiti
za kisayansi yanayoletwa na wataalamu kuboresha kilimo chao na kuongeza
tija kwenye mazao mbalimbali ili kuweza kuchangia malengo ya nchi
kufikia uchumi wa kati.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu,
Salumu Mustafa Kijuu wakati akizungumza na wanakikundi cha Batekaka
kwenye Kijiji cha Bunazi na kikundi cha Obumo wa Kijiji cha Kashaba
kwenye uzinduzi wa zoezi la utoaji wa Mbegu bora za zao la migomba
iliyozalishwa kwa njia ya chupa na Mihogo yenye ukinzani na magonjwa ya
batobato na michirizi ya kahawia zoezi lililofadhiliwa na Tume ya Taifa
ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa la Bioteknolojia kwa
Maendeleo ya Kilimo Tanzania (OFAB).
Alisema
Kilimo pekee ndicho kinachoweza kuwakwamua wananchi kutokana na wimbi
la umasikini lakini akasisitiza kuwa kilimo hicho lazima kizingatie
mbinu zote za kilimo bora ambacho kitamuwezesha mkulima kulima eneo dogo
na kupata mavuno makubwa na kuchana na kile cha zamani na mazoea cha
kulima bila kutumia mbinu za kisayansi.
“Tafiti
nyingi zinafanyika hapa nchini lakini zinaishia kwenye makabati na
haziwafikii wakulima ambao ndio walengwa wa tafiti hizo lakini
nawashukuru COSTECH kwa kushirikiana na watafiti wetu kwa kutuletea
mbegu hizi bora mlizozitafiti na kujihakikishia kuwa zinauwezo wa
kutatua changamoto za wakulima wetu na kuongeza tija”Alisema Mkuu huyo
wa mkoa wa Kagera.
Mkuu
huyo wa mkoa wa Kagera ameshukuru COSTECH kwa kuamua kusaidia
kuwafikishia wakulima mbegu bora za MIhogo na Migomba na kuanzisha
mashamba darasa kwenye wilaya zote za mkoa huo ambayo yatawezesha
wakulima wengi zaidi kujifunza kwa vitendo na hatimae kuweza kuinga
mbinu hizo za kisasa zilizotafitiwa na kwenda kuzitumia kwenye mashamba
yao baada ya kuona matunda yatokanayo na mshamba hayo.
Meja
Jenerali Mstaafu Kijuu pia alibainisha kuwa hivi sasa mkoa umejipanga
kuhakikisha kila wilaya inakuwa na kiwanda kimoja kikubwa cha kuchakata
zao moja na kila wilaya kuwa na zao moja la biashara hali ambayo
itasaidia katika kuwahakikishia masoko ya uhakika wa mazao ya wakulima
na hivyo kuongeza ari ya uzalishaji kwenye maeneo mengi.
Aliwataka
maofisa ugani kuwasaidia wakulima katika kutumia mbinu bora za kilimo
ili kuweza kuzalisha kwa tija na kuwataka kila mmoja kuwa na shamba lake
ambalo wakulima wataweza kuona na kujifunza kwao badala ya kuwa
wazungumzaji tuu bila wao kuonyesha mfano.
Awali
akizungumza malengo ya mpango huo wa ugawaji mbegu na malengo yake,
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Utawala na Fedha wa COSTECH, Shabani Hussein alisema kuwa mpango huo ni
moja ya utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo kwa mujibu wa sheria ya
uanzishwaji wake ya kuhakikisha matokeo mazuri ya sayansi na teknolojia
yanawanufaisha walengwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Alisema
kuwa ili kuweza kufikia adhima ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa
Tanzania ya viwanda ni lazima suala la kilimo lipewe msisitizo wa
kutosha ili kuweza kuzalisha malighafi za kutosha kulisha vwanda
vitakavyojengwa lakini bila kilimo mpango huo unaweza kukwama.
Alisema
pamoja na COSTECH kuwa mshauri mkuu wa serikali katika masuala yote
yanayohusu sayansi,teknolojia na uvumbuzi lakini pia wanashirikiana na
watafiti na vituo vya utafiti katika kusaidia kufikisha matunda hayo ya
tafiti kwa wakulima ili kusaidia kuongeza tija na kuwakwamua wakulima
katika wimbi la umasikini.
‘’Naamini
mbegu hizi tulizozileta leo na mashamba darasa haya yatakuwa chachu kwa
wakulima wengine kuona na kujifunza mbinu bora za kilimo kwenye maeneo
yao na baadae mbinu hizo kusambaa kwa wakulima wengine kwenye maeneo ya
jirani" alisistiza Hussein
Mwakilishi
huyo wa Mkurugenzi mkuu wa COSTECH alisema mbegu hizo bora za Migomba
safi isiyo na magonjwa pamoja na mbegu bora ya mihogo aina ya Kiroba
yenye ukinzani na magonjwa ya batobato kali na michirizi ya kahawia
itagaiwa kwenye vikundi kwenye wilaya zote za mkoa huo wa Kagera na
kupewa mbinu bora za kilimo kutoka kwa wataalamu.
Mkuu
wa WIlaya ya Missenyi, Luteni Kanali Denis Mwila amewapongeza COSTECH
na OFAB kwa kutimiza ahadi yao ya kuwaletea wakulima mbegu hizo na
kuwaahidi kuwa watasimamia mashamba darasa hayo vizuri hadi kuvuna ili
wakulima waweze kuona umuhimu wa sayansi na mbinu bora za kilimo kwenye
uzalishaji.
“
Tumepata bahati kubwa sana wana Missenyi uzinduzi huu kimkoa kufanyika
kwenye wilaya yetu maana zipo wilaya nyingi lakini bahati imetuangukia
sisi hivyo tuyatunze mashamba na mbegu hizi na tusiwaangushe COSTECH
waliotuletea mbegu hizi bora” alisema Mwila.
Pia
ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kutoa ruzuku za pembejeo mara
mbili kwa mwaka kwenye mkoa wa Kagera kutokana na kuwa na misimu miwili
ya kilimo badala ya kuwapatia pembejeo msimu mmoja pekee sawa na mikoa
mingine yenye msimu mmoja.
Ameahidi
kushirikiana na COSTECH na wataalamu katika kila aina ya teknolojia na
mbinu bora inayowafaa wakulima wa wilaya yake ili kuwawezesha kuzalisha
chakula kingi na mazao ya biashara ambayo wananchi watauza na kujipatia
kipato.
Kwa
upande wao wakulima kwenye vikundi hivyo wameahidi kuyatunza na
kuyalinda mashamba hayo na mbegu hizo ili kuzizalisha kwa wingi na
kuweza kuwasambazia wakulima wengine kwenye maeneo yao ili
kujihakikishia usalama wa chakula kwa kulima zao bora la muhogo na
kulima migombo bora iliyozalishwa kwa njia ya chupa baada a migomba yao
kushambuliwa sana na ugonjwa hatari wa mnyauko.
Pia
wakapaza sauti zao kwa serikali kuhakikisha wanawapelekea mbegu bora za
mahindi na mazao mengine kwa wakati kupitia mpango wa serikali wa kutoa
ruzuku ya pembejeo maana kilimo mbili za mbegu bora ya mahindi
wananunua kwa wastani wa shilingi 15 bei ambayo ni kubwa kwa wakulima
wengi.
Mkuu
wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu (wa tatu kulia),
akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa mashamba darasa ya kilimo
bora cha mihogo na migomba iliyozalishwa kwa njia ya chupa (tissue
culture), kwa ufadhili wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia (OFAB) katika
vijiji vya Bunazi na Kashaba wilayani Missenyi mkoani humo leo. Shamba
hilo litasimamiwa na Kikundi cha Ushirika cha Batekaka. Kutoka kulia ni
Mkuu wa Wilaya hiyo, Luteni Kanali, Denis Mwila, Mwenyekiti wa Kikundi
hicho, Belington Kyokwete, Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya
Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa
Utawala na Fedha, Shaban Hussein na Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya
ya Missenyi, Projestus Tegamaisho.
Miche ya migomba ikiwa tayari kupandwa.
Ofisa Ugani wa Kata ya Kasambya, Hakika Ibrahim, akizungumza kataika uzinduzi huo.
Mwakilishi
wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein,
akizungumza katika uzinduzi huo.
Mtafiti kutoka OFAB, Dk. Beatrice Lyimo akizungumza katika uzinduzi huo.
Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti cha ARI-Maruku akielezea mbegu hiyo mpya ya migomba.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu (wa tatu kulia), Mwakilishi
wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein na
Mkuu wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Luteni Kanali, Denis Mwila (kulia), pamoja na Mwenyekiti wa Kikundi cha Ushirika cha Batekaka, Belington Kyokwete, wakiwa wameshika mmoja wa mche wa mgomba katika uzinduzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu , akipanda mche wa mgomba kwenye shamba darasa katika Kijiji cha Bunazi.
Mwakilishi
wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein,
akipanda mgomba kwenye shamba darasa hilo.
Mkuu
wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu , akiwahutubia
wananchi wa Kijiji cha Kashaba kabla ya kuzindua shamba darasa la zao la
mhogo.
Usikivu katika uzinduzi huo. Kutoka kulia ni Mtafiti kutoka OFAB, Dk. Beatrice Lyimo, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Adam Swai na Mwakilishi
wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein,
akipanda mgomba kwenye shamba darasa hilo.
Wananchi wa Kijiji cha Kashaba wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Mkuu
wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu , akimpongeza
kijana, Shafii Idrisa wa Kijiji cha Kashaba ambaye ameamua
kujishughulisha na kilimo kijijini hapo badala ya kukimbilia mjini na
kuendesha bodaboda kama walivyofanya wenzake.
Mtafiti
wa mazao ya jamii ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti cha ARI-Maruku,
Jasmeck Kilangi, akimueleza Mkuu wa Mkoa namna ya upandaji wa zao la
mihogo.
Mkuu
wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu, akipanda mbegu ya
mhogo katika shamba darasa katika Kijiji cha Kashaba.
Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Missenyi, Projestus Tegamaisho, akitoa shukurani baada ya uzinduzi huo.
No comments:
Post a Comment