Na Felix Mwagara (MOHA)
Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelitaka Jeshi
la Magereza kumchukulia hatua kali Mkandarasi wa mradi mkubwa wa
umwagiliaji wa Gereza la Kilimo Idete wilayani Kilombero endapo
atabainika alifanya makosa kwa kuutelekeza mradi huo.
Mradi
huo ambao ungesaidia kuendeleza kilimo cha mpunga na mahindi kwa zaidi
ya ekari 1000, unathamani ya zaidi ya Bilioni 2.5 ambapo ulianza
kujengwa mwaka 2013 mara bada ya Serikali kumpa Mkandarasi huyo wa
Kampuni ya Tanzania Building Works ya Dar es Salaam, zaidi ya Bilioni 1
ili kuufanikisha mradi huo katika hatua ya awali.
Akizungumza
mara baada ya kuukagua mradi huo uliopo Idete mkoani Morogoro, Masauni
alisema Serikali ya Awamu ya Tano haitakubali uzembe huo kwa fedha za
Serikali kuchezewa huku mradi huo haujakamilika.
Masauni
alilitaka Jeshi la Magereza kuhakikisha Mkandarasi huyo ambaye fedha
alizopewa haziendani na ukubwa wa kazi alizozifanya, achunguzwe haraka
iwezekanavyo na endapo ikibainika amefanya makosa hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi yake.
“Fedha
ni nyingi alizopewa, zaidi ya bilioni moja za Serikali zimetolewa, na
ukiangalia ukubwa wa kazi aliyoifanya haiendani na thamani ya fedha
hizo, hivyo hatuwezi kuvumilia na kuona fedha za Serikali zikichezewa,
nahitaji huyu mkandarasi achunguzwe na ikithibitika amefanya makosa
hatua za kisheria zichukuliwe,” alisema Masauni na kuongeza;
“Fedha
zilizotumika ni nyingi halafu mkandarasi huyo eti anaondoka kwasababu
ambayo inayojulikana akisingizia kuwa ukosefu wa fedha, Serikali haiwezi
ikachezewa, tendo la kuchelewa kwa mradi huu ameitia hasara kubwa
Serikali.”
Akizungumzia
suala hilo, Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Morogoro, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Mzee Nyamka alisema Mkandarasi huyo
aliondoka mwaka jana kwa kuhamisha vifaa vyake na kuutelekeza mradi
huo. “Endapo
mradi huu ungekamilika kwa wakati hakika mavuno ya mpunga yangeongezeka
kwa kasi kubwa kutokana ukubwa wa mradi huu,” alisema Nyamka.
Akitoa
taarifa yake kwa Naibu Waziri, Karani wa Mradi huo, Mkaguzi wa Jeshi
hilo, katika Gereza la Kilimo Idete, Juma Mtega alisema kazi alizotakiwa
Mkandarasi huyo kuzifanya ni kujenga jengo la ofisi litakalo tumika na
mkandarasi na mhandisi mshauri, jengo la stoo ya kuhifadhia vifaa vya
ujenzi na kujenga banio.
Pia
alipaswa kujenga mfereji mkubwa wa kusafirisha maji kwenda mashambani
umbali wa mita 2450, na kujenga mfereji mdogo wa kusafirishia maji
mashambani umbali wa mita 3450. Hata hivyo, Mtega alisema mpaka mwaka
jana alivyoondoka, kazi alizozifanya ni kujenga jengo la ofisi lenye
vyumba vitatu ambalo bado halijakamilika, amejenga banio ambalo
limekamilika kwa asilimia 95.
“Pia
alifanikiwa kujenga mfereji mkubwa wa kusafirisha maji kwa umbali wa
mita 2450 hadi 3250, hii inatokana na njia iliyotakiwa kupita mfereji
ambapo awali ilibadilishwa. Pia amejenga mfereji mdogo wa kusafirishia
maji umbali wa mita 150,” alisema Mtega.


Post a Comment