Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu kamishna (DCP) Charles Mkumbo
|
Na Rashid Nchimbi
wa Jeshi la Polisi Arusha
Wakuu wa vituo vidogo, Wakaguzi wa Tarafa pamoja na Polisi
kata wameambiwa kwamba wanatakiwa kuwa karibu na wananchi hasa kwa kushiriki
shughuli za kijamii kama vile misiba na matatizo mbalimbali hali ambayo
itasaidia kupata taarifa nyingi za uhalifu.
Akizungumza katika kikao hicho kilichowahusisha pia watendaji
wa kata mbalimbali za halmashauri ya jiji la Arusha kilichofanyika mwishoni mwa
wiki katika ukumbi wa bwalo la Polisi lililopo mjini hapa, kamanda wa polisi
mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema kutatua matatizo ya
kihalifu yanayowakabili wananchi si njia pekee ya kuwa karibu na wananchi bali
pia askari hao wanatakiwa kushiriki kwa namna moja au nyingine katika shughuli
za kijamii katika maeneo yao.
Alisema kitendo hicho cha askari hao kuishi vizuri na
wananchi nje ya kazi yao ya Upolisi kitasabaisha wananchi wajione wapo karibu
na askari kwa kila jambo hali ambayo itasaidia kupata taarifa zaidi za kihalifu
ambazo hatimaye watazifanyia kazi.
”Ushirikiano wenu pia ujikite kushiriki katika masuala ya
kijamii kama vile misiba, lakini pia kuna matatizo mengine kama ya kukatika kwa
umeme Polisi kata unapaswa uwasiliane na Tanesco ili kujua tatizo lipo wapi na kisha
kuwajulisha wananchi wa kata yako”. Alisema Kamanda Mkumbo.
Aidha Kamanda Mkumbo alisisitiza kudumishwa kwa ushirikiano
baina ya askari hao na viongozi wa mitaa pamoja na kata ili kujenga umoja imara
utakaosaidia katika kupambana na uhalifu na kuwaeleza watendaji nao wanatakiwa
kuwaambia mabalozi wawe na madaftari la usajili wa wageni katika maeneo yao yatayowawezesha
kujua tarehe ya kuingia na kuondoka hali ambayo itasaidia kuimarisha usalama.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa kata ya Ngarenaro Bw.
Brayson Nassari aliendelea kuhimiza ushirikiano katika utendaji wa kazi baina
ya Polisi kata na watendaji hali ambayo itasaidia kuimarisha utulivu na amani
ndani ya jiji la Arusha.
Naye Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi (SSP)
Emmanuel Tille alizidi kuwasisitiza Polisi kata wawe na vikao vya mara kwa mara
na wananchi hali itakayowasaidia kutoa elimu ya ulinzi shirikishi na kupata
taarifa lakini pia aliwaeleza watendaji wa kata waendelee kutoa taarifa na
kufichua sehemu zenye viashiria vya uhalifu ili zifanyiwe kazi kwa haraka.
Kuwepo kwa mahusiano ya karibu baina ya Jeshi la Polisi mkoa
wa Arusha na wananchi kumesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya
uhalifu ambapo takwimu za hivi karibu zilizotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa
Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo zinaonyesha kwamba kwa kipindi cha
miezi sita toka Januari hadi Juni mwaka huu 2017 uhalifu umepungua kwa 24.4%
ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana 2016.
No comments:
Post a Comment