Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitembelea harakati
za ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung uliopo Mpirani Kikwajuni
Mjini Zanzibar. Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Hbari, Utamaduni, Utalii na Michezo Rashid Ali Juma.
Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Omar Hassan Omar
akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hayupo
pichani ramani ya Uwanja wa Mao Tse Tung utakavyokuwa baada ya
kukamilika kwake.
Balozi
Seif katika picha ya pamoja na Uongozi wa ngzi ya juu wa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo pamoja na wahandisi wa nujenzi wa
uwanja wa michezo wa Mao Tse Tung.
Balozi
Seif akiagana na Mshauri wa Rais wa Zanzibar katika masuala ya
Utamaduni Chimbeni Kheir baada ya kuangalia harakati za ujenzi wa uwanja
wa michezo wa Mao hapo Mpirani Kikwajuni Mjini Zanzibar. Picha na – OMPR – ZNZ.
Harakati
za ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung uliopo Mpirani Kikwajuni
Mjini Zanzibar zinaendelea karibu Miezi Miwili sasa chini ya Wahandisi
wa Kampuni ya Kimataifa ya Zhengtai Group ya Jamuhuri ya Watu wa China.
Ujenzi
huo unafuatia msada mkubwa ulioidhinishwa na Serikali ya Jamuhuri ya
Watu wa China kwa Serikali ya Zanzibar katika azma ya kuimarisha
uhusiano wa muda mrefu wa pande hizo mbili ukizingatia heshima uliopewa
Uwanja huo wa kuitwa jina la Muasisiwa Taifa la China Hayati Mao Tse
Tung.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa ya
kutembelea Uwanja huo kujionea harakati za ujenzi huo kazi ambayo
inaonyesha mafanikio mazuri.
Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Omar Hassan Omar
alisema eneo hilo litakuwa na Viwanja Viwili Vikubwa vya chezo wa Soka,
viwanja vyengine vidogo vya Michezo ya ndani pamoja na eneo maalum la
Mazoezi.
Hassan
alimueleza Balozi Seif kwamba Moja ya Viwanja hivyo utajumuisha
Majukwaa Mawili ya watazamaji ambapo mipango ya baadae Wizara
inayosimamia Michezo itafikiria kuweka Vibaraza ili kuwapa fursa nzuri
watu kutazama michezo kwa utulivu zaidi.
Alieleza
kwamba Uwanja huo utakaokuwa wa Kijamii zaidi tofauti na viwanja
vyengine vinavyotoza viingilio vikubwa unatarajiwa kugharimu Dola za
Kimarekani Milino Tano sawa na Shilingi Bilioni 12 za Kitanzania.
Naye
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Rashid Ali Juma alisema
Serikali imezingatia mambo muhimu yaliyohitajika kufanywa kabla ya
kuanza kwa ujenzi huo ili kuwaondoshea usumbufu wajenzi wa Mradi huo.
Waziri
Rashid alisema mahitaji hayo muhimu ilikuwa ni pamoja na huduma za
maji, huduma za umema pamoja na ulinzi wa vifaa na mali za Kampuni
inayojenga Uwanja huo ya Zhengtai Group.
Naye
kwa upande wake Mkuu wa Wahandisi wa ujenzi wa Uwanja wa MaoTse Tung
kutoka Kampuni ya Zhengtai Group ya Nchini Bwana Ligen Zhang
alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kazi hiyo
itaendelea kutekelezwa ili imalizike kwa wakati ulipangwa.
Hata
hivyo Bwana Ligen alisema licha ya changamoto chache zilizojichomoza
ikiwemo rasilmali ya mchanga lakini juhudi zitachukuliwa katika kuona
mradi huo unakwenda vyema bila ya kuathiri ratiba nzima iliyowekwa.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
aliipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa misaada inayotowa
kwa Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo.
Balozi
Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake
itajitahidi kushirikiana na wahandisi wa Ujenzi huo wa uwanja ili kuona
Mradi huo unakamilika katika kipindi kilichokusudiwa.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaonya Wananchi kuacha tabia ya wizi wa
vifaa vilivyotengwa kwa ajili ya kazi hiyo kwani kufanya hivyo ni aibu
kwa vile jamii ya Kimataifa itashangaa kuona miradi iliyotengwa
kuwanufaisha Wananchi inafanyiwa hujuma.
Aliagiza
vyombo vinavyohusika na ulinzi kuwachukulia hatua kali za kisheria na
kinidhamu wale wote wanaofanya vitendo viovu vya kutaka kuiba vifaa vya
ujenzi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/7/2017.
No comments:
Post a Comment