Ujenzi
wa Daraja la Kavuu lenye urefu wa Mita 89 linalounganisha Halmashauri
ya Wilaya ya Mlele na Halmashauri ya Wilaya ya Mpwimbwe Mkoani Katavi
ujenzi wake umekamilika na litaanza kutumika ifikapo mwishoni mwa mwezi
Julai mwaka huu.
Akizungumza
mara baada ya kukagua ujenzi wa Daraja hilo Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amesema kukamilika kwa
ujenzi huo kutarahisisha usafirishaji wa abiria na Mizigo kutoka Mkoa wa
katavi kwenda mikoa ya jirani.
“Serikali
iliona kero kubwa wanazozipata wananchi wa mkoa huu hasa kwenye
usafirishaji wa abiria na mizigo kwenye kipindi cha mavuno, hivyo baada
ya kukamilisha Daraja hili wananchi wataweza kupita vipindi vyote vya
Mwaka,” alisema Naibu Waziri Eng. Ngonyani.
Aidha,
Eng. Ngonyani amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa
wa Katavi Eng. Abdon Maregesi Kuhakikisha Mzani unaohamishika unawekwa
ili kudhibiti magari yatakayozidisha Tani 36.
Kwa
upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Katavi Eng. Abdon
Maregesi amemuhakikisha Naibu Waziri, Eng. Ngonyani kuwa wakala utaweka
mzani huo ili kutoruhusu magari yaliyozidisha Uzito wa Mzigo kupita
kwenye Daraja hilo.
Wakati
huo huo, Naibu Waziri Eng. Ngonyani amekagua ujenzi wa Nyumba za
Viongozi Mkoani humo na kuuagiza Wakala wa Majengo nchini (TBA),
kuhakikisha ujenzi wa nyumba hizo unakamilika ifikapo Novemba mwaka huu.
“Serikali
imeshatoa fedha za kukamilisha ujenzi wa nyumba hizi, ujenzi huu
ulisimama kwa takribani miezi minne kwa sasa hakuna sababu ya ujenzi
kusuasua wakati fedha zipo, ninakuhakikishia Mkuu wa Wilaya nyumba hizi
zitakamilika kwa wakati ili zianze kutumika,” alisisitiza Naibu Waziri
Eng. Ngonyani.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri Eng. Nyonyani amekagua ujenzi wa Barabara
ya Sitalike-Mpanda yenye urefu wa kilomita 36.9 ambao ujenzi wake
umekamilika kwa asilimia 99, barabara hii ni sehemu ya barabara kuu
inayoanzia Tunduma kupitia Sumbawanga, Mpanda, Uvinza, Kibondo,
Nyakanazazi hadi Mutukula.
Naibu
Waziri Eng. Ngonyani yupo katika Ziara ya kukagua Miundombinu ya
barabara, Viwanja vya Ndege, Ujenzi wa Nyumba za viongozi na Madaraja
katika Mkoa wa Katavi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Naibu
Waziri Wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Wa
kwanza kushoto), akikagua ujenzi wa Nyumba za viongozi zinazojengwa na
Wakala Wa Majengo nchini (TBA) Mkoani Katavi, Kulia kwake ni Mkuu wa
Wilaya ya Mlele Bi. Rachel Kassanda.
Meneja
Wa Wakala Wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Abdon Maregesi (kulia),
akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng.
Edwin Ngonyani (Katikati) juu ya hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Daraja
la Kivuu wakati Naibu Waziri huyo alipokagua, Mkoani Katavi.
Naibu
Waziri Wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akiongea
na wananchi wa kata ya MajiMoto Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi mara baada
ya kukagua Daraja la Kavuu ambalo ujenzi wake umekamilika na
linatarajiwa kuanza kutumika mwishoni mwa mwezi huu..
Naibu
Waziri Wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani
akisalimiana na wakazi wa kata ya MajiMoto Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi
mara baada ya kuongea nao.
Naibu
Waziri Wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Kulia)
akiongea na Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi Mhe. Omary Yahya
Massare (Kulia), Wakati Waziri Ngonyani alipotembelea Jimboni kwake
mwishoni mwa wiki.
Muonekano
wa Daraja la Kavuu lenye urefu wa Mita 89 linalounganisha Halmashauri
ya Wilaya ya Mlele na Halmashauri ya Wilaya ya Mpwimbwe Mkoani Katavi
ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99.
Muonekano
wa Barabara ya Sitalike-Mpanda yenye urefu wa kilomita 36.9 ambapo
ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99, barabara hii ni sehemu ya
barabara kuu inayoanzia Tunduma kupitia Sumbawanga, Mpanda, Uvinza,
Kibondo, Nyakanazazi hadi Mutukula.
No comments:
Post a Comment