Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akivipongeza
Vituo vya Mafuta vya Puma na Total kwa kuonesha mfano wa kufunga mashine
za EFDs katika Pampu zote za mafuta kwenye vituo vyao, wakati
akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Jijini Dar es Salaam.(Picha: Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini-WFM)
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akiwaomba
wananchi kulipa kodi ya Majengo mapema kwa mwaka wa Fedha 2017/18 ili
kuepuka usumbufu wa msongamano, alipofanya Mkutano na Waandishi wa
habari katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akitoa
agizo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha kuwa mashine za
kutolea risiti za kielektroniki (EFDs) zinatumika ipasavyo na
kutengenezwa mara moja zinapoharibika na kwamba zisipotengenezwa ndani
ya saa 48 zifungwe na wamiliki wake watozwe faini, alipozungumza na
wanahabari, Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Waandishi
wa Habari Jijini Dar es Salaam wakiwa katika Mkutano na Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) ambapo
Waziri huyo aliwashukuru wananchi kwa kulipa kodi ya Majengo kiasi cha
Sh. Bilioni 32.5 kufikia Julai 15, 2017, katika Ukumbi wa Wizara ya
Fedha Jijini Dar es Salaam.
………………………………………………………………..
Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Serikali
kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh bilioni 32.5 ya
kodi ya majengo, kwa mwaka wa fedha 2016/17 kutoka katika Majiji, Miji
na Manispaa 30 nchini.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) amewaambia waandishi wa
habari Jijini Dar es Salaam kwamba makusanyo hayo ni sawa na asilimia 56
ya lengo lililowekwa Mwaka wa Fedha uliopita la kukusanya shilingi
bilioni 58.
Alisema
kuwa hatua niyo ni mafanikio makubwa tangu TRA ipewe jukumu la
kukusanya kodi hiyo ambapo mwaka wa fedha 2015/2016 katika maeneo hayo,
Halmashauri zilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 28.3 wakati TRA
imekusanya kiasi hicho cha shilingi bilioni 32.5 tangu ianze kukusanya
kodi hiyo mwezi Oktoba mwaka wa fedha 2016/2017.
“Mpaka
kufikia tarehe 15 Julai mwaka huu TRA imekusanya sh. bil 32.5 kipindi
ambacho ni kifupi, na kwamba mapato hayo yanatarajiwa kuongezeka
kutokana na mwitio mkubwa wa wananchi kulipa kodi ya majengo”Alisema
Dkt. Mpango.
Dkt.
Mpango aliwapongeza wananchi kwa mwitio wao mkubwa wa kulipa kodi ya
majengo na kwamba wameonesha uzalendo wa kweli na ndio maana Serikali
imeamua kuongeza muda wa kulipa kodi hiyo bila adhabu hadi Julai 30
mwaka huu, hali anayoamini itapandisha zaidi mapato hayo.
Katika
hatua nyingine Dkt, Philip Mpango aliwapongeza wamiliki wa vituo vya
mafuta waliotii maagizo ya Serikali, kwa kufunga mashine stahiki za
EFDs, akitolea mfano vituo vya PUMA na TOTAL ambavyo vimefunga mashine
hizo kwenye pampu zao zote.
Aliwaonya
wamiliki wote wa vituo vya mafuta ambao hawatafunga mashine hizo za
EFDs ndani ya siku 14 kama agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli linavyoelekeza na kwamba yeye kama Waziri mwenye dhamana
atahakikisha analisimamia kikamilifu na kwamba baada ya muda huo mtu
asijekuilaumu Serikali baada ya kuanza kuchukua hatua kali za kisheria.
Aliwataka
wamiliki wa vituo hivyo kupitia chama chao cha wamiliki wa vituo vya
mafuta TAPSOA kuheshimu maelekezo ya Serikali na kuacha majibizano
yasiyo na tija kuhusu amri hiyo ya Rais kwenye vyombo vya habari kwa
kuwa huo ni utovu wa nidhamu.
Aliwageukia
wenye maduka ya vifaa vya ujenzi, vileo na maduka makubwa ‘supermarket’
nao watumie mashine hizo za kukusanyia mapato ya Serikali (EFDs)
kikamilifu na kutoa risiti kwa wateja wao huku akiwaasa wateja nao kudai
risiti wanapofanya manunuzi kulingana na kiwango halisi cha bidhaa
wanazonunua.
Alipiga
marufuku wafanyabiashara wanaosingizia mashine za EFDs kuwa mbovu na
kuwaonesha wateja wao makaratasi waliyotoa taarifa TRA kwamba mashine
zao zilikuwa mbovu kwa kipindi kifrefu na kuaigiza Mamlaka ya Mapato
Tanzania-TRA, kusimamia jambo hilo ili kuhakikisha kuwa linakoma kabisa.
“TRA
mtimize majukumu yenu mliyodhaminiwa na Serikali na kuhakikisha kuwa
wafanyabiashara ambao mashine zitakuwa hazitumiki ndani ya saa 48 kwa
kisingizio cha kuharibika zifungiwe na wamiliki watozwe faini na kulipa
kodi ya Serikali ipasavyo” aliagiza Dkt. Mpango.
“Serikali
ya Awamu ya Tano haijaribiwi, tumeazimia tutafanya kazi kwa niaba ya
wanyonge ili nchi yetu iende mbele na kwa hili watusamehe.” Alisisitiza
Dkt. Mpango
Dkt
Mpango alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli kwa kujitoa kwake kuwatumikia wananchi na
kuongoza mapambano ya uchumi yatakayo ifikisha nchi kwenye uchumi wa
kati ambao hata watu wa kawaida watajisikia kuwa unakua kwa kutatua
changamoto zao za maisha.
Alisitiza
watanzania wafanye kazi kwa bidii kujenge nchi ili kila Mtanzania apate
huduma bora, barabara bora, tiba nzuri, maji, yote haya hayawezi
kufanyika bila mapato yakutosha na kwamba Tanzania itajengwa na
Watanzania wenyewe.
No comments:
Post a Comment