NA ESTOM SANGA-TASAF.
Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- na wadau wa maendeleo wameanza mkutano wa
kutathimini utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo kupitia Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini kwa kipindi cha miezi SITA iliyopita.
Mkutano
huo unaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za TASAF mjini Dar
es salaam pia unawajumuisha maafisa wa serikali kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar,pamoja na mambo mengine umefahamishwa juu ya mafanikio na
changamoto zilizopatikana katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru kaya
maskini kwa kipindi cha kuishia mwezi Marchi mwaka huu.
Katika
mawasilisho ya shughuli zilizotekelezwa na TASAF katika kipindi
kilichopita, imeonyeshwa kuwa zaidi ya kaya milioni MOJA za walengwa
zimeendelea kunufaika na Mpango kupitia ruzuku na utekelezaji wa miradi
mbalimbali iliyoibuliwa na walengwa kupitia utaratibu wa ajira ya muda
ambapo hulipwa ujira baada ya kutekeleza kazi hizo.
Aidha
taarifa hiyo imeonyesha kuwa kumekuwa na mwitikio chanya wa walengwa
katika kuanzisha shughuli za kiuchumi kwa kutumia fedha zinazotolewa na
TASAF chini ya utaratibu wa uhawilishaji fedha, na hivyo kusaidia kwa
kiwango kikubwa ongezeko la kipato kwa kaya zilizoandikishwa kwenye
Mpango.
Mafanikio
mengine yaliyoonyeshwa ni ongezeko la mahudhurio ya watoto wenye umri
wa chini ya miaka mitano kutoka katika kaya za walengwa kupata huduma za
kliniki kwa lengo la kuboresha afya na makuzi yao pamoja na kuongezeka
kwa mahudhurio shuleni kwa watoto wanaotoka kwenye kaya za walengwa wa
Mpango wa kunusuru kaya maskini.
Katika
kuboresha zaidi huduma kwa walengwa, TASAF kwa kushirikiana na idara
nyingine za serikali imeandaa utaratibu wa kuanza kutoa ruzuku ya fedha
kwa njia ya kielektroniki ambapo majaribio yataanza katika baadhi ya
maeneo ya Utekelezaji wa Mpango huo.
Wadau
hao wa Maendeleo baada ya kuhudhuria mkutano huo wa siku moja watapata
fursa ya kutembelea maeneo ya utekelezaji wa Mpango huko
Zanzibar,Itirima,Magu,Lindi Longido ambako watawatembelea walengwa wa
Mpango kuona namna wanaoendelea kunufaika na fedha zinazotolewa katika
jitihada za serikali kupitia TASAF katika kuwaondolea wananchi kero ya
umaskini.
Zifuatazo
ni picha za washiriki wa mkutano huo wa wadau wa maendeleo ,baadhi ya
maafisa wa serikali na watumishi wa TASAF unaofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano wa Mfuko huo wa Maendeleo ya Jamii jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akifungua mkutano wa wadau wa maendeleo kwenye ukumbi wa mikutano wa Mfuko huo jijini Dar es salaam.

Msimamizi wa shughuli za TASAF (Benki ya Dunia) Bwana Muderis Mohamed (aliyesimama) akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa maendeleo na TASAF .

Baadhi ya wadau wa Maendeleo na Maafisa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF – wakiwa katika ukumbi wa mikutano wa Mfuko huo katika mkutano wa kujadili utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya maskini.


Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Wadau wa maendeleo na TASAF (picha ya juu na chini ) wakiwa kwenye mkutano ulioanza leo kujadili utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya masikini.


Post a Comment