Senpai Esther Thomas (kushoto) akipangua chudan tzuki (ngumi ya kifua) wakati semina hiyo ikiendelea.
Anafundisha kwa mifano! Shihan Okuma akishambuliwa na Jerome Sensei kama sehemu ya maelekezo katika semina hiyo
Na Daniel Mbega
SEMINA kubwa ya Shotokan Karate kwa nchi za Afrika Mashariki,
Kati na Kusini, imeanza leo hii jijini Dar es Salaam ambapo kwa mara ya kwanza
katika historia ya mchezo huo nchini Tanzania, inaongozwa na mkufunzi mkuu,
Shihan Koichiro Okuma (6th Dan), kutoka makao makuu ya chama cha
karate cha Japan Karate Association/World Federation (JKA/WF), Tokyo, Japan.
Semina hiyo – maarufu kama JKA/WF- Tanzania Southern, Central
& East African Region Gasshuku – ambayo imeandaliwa na chama cha Japan
Karate Association/World Federation-Tanzania (JKA/WF-Tanzania) ni ya nane
kufanyika ambapo kwa mwaka huu inashirikisha makarateka 45 kutoka Zimbabwe,
Zambia, Uganda, Kenya na wenyeji Tanzania.
Kwa mujibu wa JKA/WF-Tanzania, semina hiyo ya wiki nzima
inatarajiwa kufikia tamati Jumamosi.
Makarateka ambao wameanza kushiriki leo hii, kutoka Tanzania
ni Jerome Mhagama Sensei, Justine Limwagu, Seberian Dagila, Said O. Kissailo, Lulangalila
Lyimma, Athumani Kambi, Mikidadi Kilindo Sensei, Marcus George, Khamis K.
Sambuki, Hamis Said Mkumbi, Selemani A. Mkalola, Christopher William, Eliasa
Mohammed, Adson Aroko Sensei, Nestory Federicko, Daniel Mbega, Willy Ringo
Rwezaura Sensei, na Shihan Dudley Mawala Sensei, ambaye alikuwa mgeni mwalikwa.
Makarateka wengine na nchi zao kwenya mabano ni Gibson
Sangweni (Zimbabwe), Robert Chisanga (Zambia), Thobias B. Rudhal (Kenya), George
Otieno (Kenya), Joshua Oude (Kenya), George Warambo (Kenya), George Okeyo (Kenya),
Florence Kieti (Kenya), Asana Mahmoud Ulwona (Uganda), Ofubo Issa Yahaya (Uganda),
Magezi Yasiin (Uganda), Wanyika Abdurahman (Uganda), Frederic Kilcher (Ufaransa)
na Koichiro Okuma (Japan).
Mkufunzi mkuu wa JKA/WF-Tanzania, Jerome George Mhagama Sensei
(5th Dan), amesema hata hivyo kwamba, tofauti na miaka
iliyotangulia, safari hii hakutakuwa na mashindano ili kutoa fursa kubwa kwa
Shihan Okuma kufundisha vyema na kuwapandisha madaraja makarateka mbalimbali
kuanzia ngazi ya Sho-Dan, Ni-Dan, San-Dan na Yon-Dan (1st – 4th
Dan).
“Tunataka tupate muda wa kutosha wa kufanya semina pamoja na
mitihani, kwani mbali ya kuwapandisha madaraja makarateka mbalimbali, lakini
pia kuna ambao watafanya mitihani ya ukufunzi na uamuzi wa kimataifa ili
kupanua wigo na kupata walimu na waamuzi wa kutosha katika kanda yetu,” amesema
Jerome Sensei, ambaye alipanda daraja Jumanne, Septemba 6, 2016 baada ya
kufanya vizuri na kufaulu mtihani wa 5th Dan jijini Nairobi, Kenya chini
ya Shihan Okuma.
Hata hivyo, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kesho ambapo
makarateka kutoka Zanzibar nao watahudhuria baada ya kushindwa leo kutokana na
sababu mbalimbali.
Jerome Sensei amesema kwamba, changamoto kubwa ambayo
inawakabili wao pamoja na mchezo mzima wa Karate nchini Tanzania ni kuwekwa
pembeni na wadau mbalimbali wa michezo ikilinganishwa na michezo mingine, hali
ambayo imekuwa vigumu kwao kupata udhamini.
Ameiomba Serikali na wadau wengine kuutupia macho mchezo huo,
kwani unailetea sifa kubwa Tanzania kutokana na mafanikio ya mchezaji mmoja
mmoja.
Katika kipindi cha miaka takriban 10, Tanzania imekuwa kinara
wa mchezo wa Karate katika kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini ukitoa
Afrika Kusini pekee, hatua ambayo imechangiwa na mafanikio binafsi ya Jerome
Sensei, ambaye kwa jitihada zake ameshiriki mashindano ya dunia ya Karate mwaka
2012 na kurudia raundi ya nne, mashindano ambayo yalifanyika Pataya, Thailand,
ambapo alitolewa na mtu ambaye alikuja kuwa bingwa wa dunia.
Mbali ya hivyo, ameshiriki mashindano mengine jijini Tokyo,
Japan lakini pamoja na kutotwaa ubingwa, ameweza kupanda madaraja kwa viwango
vya kimataifa na sasa ni mkufunzi, mtahini na mwamuzi wa kimataifa, ambapo
ameweka rekodi ya pekee kwa kuwa mkufunzi mwenye umri mdogo kabisa katika historia
ya JKA/WF tangu chama hicho kilipoanzishwa Mei 1947.
Kwa mujibu wa rekodi za JKA/WF, Jerome Sensei (36) ni karateka
wa pili wa Afrika Mashariki kuwa na hadhi ya Dan Tano (5th Dan)
baada ya David Mulwa Sensei wa Kenya, hivyo ameteuliwa kuwa mkufunzi mwenza
mkuu wa Afrika Mashariki.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Shihan Okuma, ambaye ametokea
Kenya ambako kulikuwa na semina wiki iliyopita, amesema kuwa ujio wake siyo wa
bahati mbaya bali umetokana na jitihada ambazo Tanzania imekuwa ikionyesha
katika maendeleo ya Karate, hususan mafanikio yasiyo na kifani ya Jerome
Sensei.
“Nimetumwa na makao makuu kuja kuiunga mkono Tanzania pamoja
na kufundisha semina hii, najua semina kama hii mara nyingi huwa inafanyika
makao makuu tu au katika kanda maalum, lakini kwa vile Tanzania imeonyesha
mafanikio makubwa, hatuna budi kuja hapa ili kuwapa fursa makarateka wengi
waweze kushiriki.
“Kuja Japan ni gharama kubwa, wengi hawawezi kumudu pamoja na
kuwa na nia na mchezo huu, ni wachache tu ambao wanapata bahati ya kuja
kuhudhuria, lakini hapa nimefurahi kuona kuna makarateka wengi wana viwango vya
juu kabisa na hii ni faraja kubwa kwangu na kwa JKA/WF,” amesema.
No comments:
Post a Comment