Mkuu
wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo(katikati) na viongozi wa Kanisa la
Waadventista wa Sabato katika picha ya pamoja.
Viongozi wa dini
nchini wameombwa kuhamasisha waumini wao kufanya kazi kwa bidii na kulipa kodi
ili kuongeza kasi ya kuleta maendeleo katika Taifa la Tanzania na pia
wametakiwa kuhamasisha waumini wao kuhakikisha wanadai risiti kila wanapoenda
kununua bidhaa au kupata huduma
mbalimbali.
Kauli hiyo ilitolewa
jana mjini hapa na Mkuu wa Mkoa wa
Arusha Mrisho Mashaka Gambo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dr John Joseph Pombe Magufuli aliyekuwa mgeni rasmi katika
Maadhimisho ya miaka 50 ya Utume wa Kanisa la Waadventista wa Sabato.
Akizungumza na
waumini na viongozi wa Kanisa hilo lililopo Burka mjini hapa, Mkuu wa Mkoa
Arusha Gambo alisema, Watanzania wanalojukumu la kufanya kazi kwani hata Vitabu vya Dini vimeelekeza kuwa mtu
asiyefanya kazi na asile na mafundisho hayo ya dini yanaendana na falsafa ya hapa
kazi tu.
Mhe. Gambo
aliendelea kusisitiza kwamba kutokana na maelekezo hayo ya vitabu vya dini ni
wazi kwamba kila mtu anatakiwa kufanya kazi kwa kadiri ya uwezo aliopewa na
Muumba ili apate riziki hatua itakayowezesha pia kupunguza wategemezi katika
Taifa letu.
Akizungumza katika
maadhimisho hayo RC Gambo kwa niaba ya Rais Magufuli alisisitiza kuwa ni vyema
kwa kila mmoja wetu kufanya kazi na kulipa Kodi.
"Kwa yule
ambaye hatalipa Kodi ajue kwamba anaikosesha nchi yake mapato ambayo yangeweza
kutumika kuendesha shughuli mbalimbali za maendeleo, pia tutambue kwamba huduma
zote ni gharama na zinatokana na kodi tunazolipa.
Hivyo katika Serikali ya
Awamu ya Tano asiyefanya kazi na asile na zaidi ya hapo asiyelipa kodi ni vyema
akafahamau kwamba analirudisha taifa lake nyuma. Niwaombeni sana viongozi wa
Dini muhamasishe waumini walipe kodi kwa mustakabali wa Taifa letu"
Kwa upande wake
Makamu Mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni Mch. Geofrey
Mbwana akitoa somo fupi wakati wa maadhimisho hayo alisema amefurahishwa sana
na uteuzi wa Mhe. Gambo na ana imani na vijana kwa sababu vijana wakati wao ni sasa
na pia ni taifa la leo hivyo wakipewa nafasi kama hii hudhihirisha vipawa
vilivyomo ndani yao na bila shaka Mkoa wa Arusha utakua Mkoa kielelezo kwa
Taifa hili.
Kanisa hili la
Sabato katika Tanzania lilianzishwa Katika kijiji cha Giti kilichopo Mamba Miamba
huko Same mnamo mwaka 1903 na kuendelea kukua katika Mji wa Shirati Mara na
kisha kufika Arusha na kuanzisha Kanisa la Burka mwaka 1966 likiwa na Jengo
moja dogo na waumini nane tu.
Hivi sasa Kanisa
hili lina majimbo mawili na waumini zaidi ya 500,000 Tanzania. Kanisa hili pia
wanamiliko Chuo Kikuu kimoja, Shule za Sekondari 17, Msingi 11 na shule za
awali 11. Pia Kanisa hili lina Hospital moja, Kituo cha Afya kimoja na Zahanati
28.
RC Gambo aliendelea
kuwaomba viongozi mbalimbali wa dini wazidi kumuombea na kumtia Moyo Mhe. Rais
katika kazi yake ngumu na kubwa anayoifanya kwa maslahi ya Taifa haswa kusaidia
wanyonge ambao kwa muda mrefu hawakuwa sehemu ya Agenda kubwa ya Serikali. Pia
waendelee kuwasisitiza wanasiasa watambue kuwa wakati wa Siasa umekwisha ni vyema Mhe. Rais akapewa nafasi
ya kuwatumikia watanzania kwa yale aliyoyaahidi kupitia utekelezaji wa ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI na
watakutana tena kwenye siasa mwaka 2019 - 2020.
|
No comments:
Post a Comment