Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen-Kijo Bisimba amepata ajali ya gari na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake, ajali hiyo ilitokea jana asubuhi katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Akiwa katika Hospitali ya Aga Khan alikolazwa majeruhi huyo, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa LHRC, Ezekiel Masanja alisema Dk Bisimba alipata ajali katika barabara hiyo alipokuwa akitokea kanisani.
“Gari alilopanda liligongwa sehemu ya ubavuni na kuzunguka mara nne. Dereva wake anaendelea vizuri lakini Dk Bisimba aliwahishwa moja kwa moja katika chumba cha dharura,” alisema Masanja.
Hata hivyo, Masanja hakuwa tayari kubainisha zaidi sehemu zipi za mwili alizopata majeraha Dk Bisimba, badala yake alisema wanasubiri ripoti kutoka kwa daktari ndipo watoe taarifa.
Baadaye mchana jana, Dk Bisimba alitolewa kwenye chumba cha dharura na kuhamishiwa wodini kuendelea na matibabu zaidi.
Akizungumza jana jioni, Mkurugenzi wa Utetezi wa kituo hicho, Harold Sungusia alisema kuwa bosi wake anaendelea na matibabu na kuna dalili za kufanyiwa upasuaji wa mguu wa kushoto.
Alisema kuwa kwa sasa wanasubiri maelekezo zaidi kutoka kwa madaktari.
No comments:
Post a Comment