Waandishi wakishuhudia gari lililokuwa linatumiwa na majambazi hao. Picha zote na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha. |
Wakutwa
na AK 47 mbili, SMG moja, bastola tatu na Radio “call” mbili za Polisi
Na
Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Watu wanne wanaosadikiwa kuwa
ni majambazi waliuawa na askari Polisi wakati wa mapambano ya majibizano ya
risasi usiku wa tarehe 17.09.2015 saa 3:30 maeneo ya Chekereni mpakani mwa
wilaya ya Arumeru na halmashauri ya Jiji la Arusha.
Hayo yalisemwa na Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Arusha alipokuwa anaongea na waandishi wa habari ofisini kwake
leo asubuhi. Akielezea mazingira ya tukio hilo Kamanda Sabas alisema Jeshi hilo
lilipokea taarifa za Kiintelejensia juu ya kuwepo kwa kundi la majambazi
lililotaka kufanya uvamizi na uporaji ndani ya jiji la Arusha.
“Tulipata taarifa toka tarehe
19.08.2015 mwezi mmoja nyuma juu ya uwepo wa kundi la majambazi toka nchini Kenya
ambao wangeshirikiana na wengine wa hapa nchini kwa nia ya kufanya uhalifu
kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo taasisi za fedha”. Alisema Kamanda sabas.
“Baada ya taarifa hizo
tukaendelea na ufuatiliaji na kufanikiwa kumkamata mtu aitwaye Sixtus Alfredy
Ngowi (51) Mtanzania, Mkazi wa Ngulelo jijini hapa ambapo baada ya mahojiano
alikiri kwamba huwa anashirikiana na majambazi wenzake toka nchini Kenya katika
kufanya matukio mbalimbali ya kiuhalifu hapa nchini”. Alifafanua Kamanda Sabas.
Baadhi ya matukio ambayo
ameyafanya ni pamoja na tukio la uporaji wa fedha zaidi ya dola 2,000,000
lilitokea jijini Dar es salaam mwaka 2005 kwenye Kampuni ya Security Group 4 na
kisha kufikishwa Mahakamani.
Mbali na tukio hilo pia mwaka
2002 alihusika na tukio la uvamizi wa Benki ya NBC tawi la Moshi mkoani
Kilimanjaro. Mwaka 2014 jambazi huyo amewahi kushtakiwa nchini Kenya kwa
matukio ya uhalifu katika Mahakama ya Mlimani Law Court iliyopo jijini Nairobi lakini
baadae aliachiwa huru.
Alizidi kukiri kuhusika katika
matukio ya ujambazi huku akishirikiana na wenzake katika matukio ya unyang’anyi
wa kutumia silaha katika jiji la Arusha ambalo lilikuwa linawalenga
wafanyabiashara wakubwa wa Madini ya Tanzanite na Hoteli za Kitalii. Miongoni
mwa tukio walilolifanya ni kumjeruhi mfanyabiashara wa madini aitwaye Mathius
Manga ambaye alipigwa kwa risasi kwenye ubavu wa kulia.
Kamanda Sabas alisema kwamba
mara baada ya kuridhishwa na mahojiano baadae jambazi huyo alikubali
kushirikiana na Polisi ili aweze kufanikisha juu ya upatikanaji wa wenzake
ambao siku ya jana walipanga kuvamia katika duka la kubadilishia fedha liitwalo
Sanya lililopo jijini Arusha.
Walipokuwa wanaelekea kwenye
eneo la tukio akiwa anaongozana na askari Polisi kwa nia ya kufanikisha
kuwapata majamabzi wengine, mara tu baada ya kufika kabla hawajawakamata
majambazi hao ambao walikuwa kwenye gari aina ya Noah rangi ya silver yenye
namba za usajili T. 981 AVK walishtuka na kuanza kulishambulia gari lililokuwa
na askari Polisi na kumjeruhi mwenzao Sixtus Alfedy Ngowi ambaye alifariki muda
mfupi wakati akiwa njiani kupelekwa hospitali.
Mara baada ya kuona hivyo,
Polisi nao walijibu mapigo na kufanikiwa kuwaua majambazi watatu huku wengine
wakifanikiwa kukimbia. Katika upekuzi kila mmoja alikutwa na bastola pamoja na
risasi. Pia walikuta mabegi matatu meusi ambapo ndani yake kulikuwa na bunduki
mbili aina ya AK 47 zenye namba 83 LG 3953 56-1 na nyingine yenye maandishi ya
kirusi pamoja na SMG moja yenye namba 56-1 28038394.
Bastola ambazo zilikutwa toka
kwa majambazi hao zilikuwa na namba CZ 75 Compact Luger-9mm namba A. 269206, CZ
85 B Luger 9mm namba 051967 na Chines Pistol namba 967741. Pia zilipatikana
magazine nne tupu za SMG, risasi 85 za SMG/AK 47 na risasi 28 za bastola.
Mbali na silaha hizo pia
walikutwa na Radio “Call” mbili aina ya Kenwood zilizokuwa hewani na wimbi la
Polisi Arusha, bullet proof moja, vifaa vya kusafishia bunduki, mifuko mitatu
ya kubebea pesa na vifaa vingine.
Majambazi hao ambao kwa sasa
miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya Mount Meru walikutwa pia na
vitambulisho mbalimbali vya Jamhuri ya Kenya pamoja na simu tano aina ya Nokia,
Tecno na Samsung. Kamanda Sabas alisema kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na
upelelezi juu ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwatafuta watuhumiwa wengine
waliofanikiwa kukimbia na kubaini mtandao mzima wa kundi hilo.
Kamanda Sabas alimalizia kwa
kuwashukuru wananchi wa Arusha kwa kushirikiana na Jeshi hilo juu ya utoaji wa
taarifa za uhalifu na wahalifu na kuonya yoyote ambaye atajiingiza katika
matukio ya kufanya uhalifu Jeshi hilo litamkamata na kumfikisha kwenye vyombo
vya sheria.
No comments:
Post a Comment