Pages

June 3, 2015

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII,LAZARO NYALANDU AUNDA TUME YA KUCHUNGUZA WANANCHI KUNYANYASWA KARATU

Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu akizungumza na wananchi wa Kata ya Buger wilaya ya Karatu mkoa wa Arusha  katika ziara ya siku moja kuzungumza na wananchi baada ya mwananchi mmoja kuuawa kwenye msitu wa Marang unaohifadhiwa na Shirika la Hifadhi ya Taifa(Tanapa).Waziri Nyalandu ameunda Tume ya kuchunguza mgogoro huo ambayo itatoa mapendekezo serikalini kwa utekelezaji.

Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu akizungumza na mmoja  wa wananchi wa Kata ya Buger wilaya ya Karatu mkoa wa Arusha  baada ya kuhutubia wananchi hao na kuwahidi serikali kuwachukulia hatua askari waliokiuka taratibu za maadili.


Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Arusha,Cesilia Paresso akihutubia wananchi wa Kata ya Buger na kuitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuzingatia sheria na wananchi kulinda Msitu wa Marang kwaajili vizazi vijavyo.


Mkazi wa Kata ya Buger,Rehema Tango akitoa kero zake mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii.

sehemu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo ambao waliweza kutoa kero zao . 

Filbert Rweyemamu,Arusha
Waziri wa Maliasili na Utalii,Lazaro Nyalandu ameunda Tume ya kuchunguza malalamiko ya wananchi wa Kata ya Buger wilayani Karatu wanaodai kunyanyaswa na askari wanyamapori wanaolinda  Msitu wa  Marang unaohifadhiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa(Tanapa).

Akizungumza na wananchi hao baada ya kusikiliza kero zao,Nyalandu aliipa siku 14 kuanzia jana kuanza uchunguzi mara moja na kutoa mapendekezo kwa serikali njia sahihi za kuchukua ili kuhakikisha wananchi hawabughudhiwi huku msitu huo ukilindwa kwa mjibu wa sheria.

Tume hiyo itakayoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu,Omari Qangw ikakua na wajumbe sita ambao ni Afisa Usalama wa taifa wilaya,Mwakilishi wa wazee wa mila,Mwakilishi wa wanawake,Mwakilishi kutoka serikali ya Kijiji,Mkuu wa Polisi wa wilaya na Mkuu wa idara ya Ujirani mwema ya Tanapa.

“Natoa siku 14 kuanzia Tume hii ichunguze malalamiko na mashahidi wote na kuleta mapendekezo ambayo yatasaidia kuondoa kutokuaminiana kati ya askari wanyamapori  wanaolinda rasilimali zetu na wananchi ambao hawapaswi kuonewa kwa namna yeyote.”alisema Nyalandu

Tukio hilo linakuja siku chache baada ya mwananchi mmoja,Fiay Hhamu kufariki dunia baada ya kupigwa risasi na askari wanyamapori wanaolinda Msitu wa Marang wakati akilisha mifugo yake  jambo lililosababisha kuwepo na uhasama baina ya pande mbili.

Hata hivyo,Nyalandu alikemea matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na askari hao na kupiga marufuku matumizi ya silaha za moto dhidi ya wananchi wasio na silaha wala kupiga risasi mifugo inayoingia kwenye hifadhi au misitu.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Arusha,Secilia Paresso alisema kwa muda mrefu wananchi wamekua wakinyanyaswa na askari wa Tanapa na kuitaka serikali kukomesha kero hiyo mara moja kwani wananchi hao wana haki ya kunufaika na msitu huo bila kuharibu mazingira yake.

Alisema Tanapa ione umuhimu wa kuwapa mafunzo vijana kutoka maeneo yanayozunguka msitu huo ili wawe sehemu ya walinzi wa maliasili hiyo badala kutengwa wakati wa kutoa ajira.

Miongoni mwa wananchi waliotoa kero zao ni Sixbert Qamunga,Rehema Tango,Elian Bayo walisema wao wanategemea ufugaji kama njia kuu ya uchumi hivyo kuzuiliwa kulisha mifugo yao kwenye eneo ambalo wamekua wakichunga awali linarudisha nyuma maendeleo yao.

“Shughuli zetu za kiuchumi zinakwama hadi tumeshindwa kuchangia ipasavyo maabara kwasababu hatuna pesa ,kipato chetu kinatokana na kuuza mifugo kwenye minada ambayo hutupatia fedha kwaajili shughili mbalimbali,”alisema Rehema

Mwananchi mwingine, Fabian Mao alisema wakati wa vita ya Kagera mwaka 1978 na 1979 Kijiji hico kilitoa Ng’ombe 48 kwajili ya kuwawezesha askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania waliokuwa wanalinda mipaka ya nchi .

Katika hali ambayo haikutarajiwa mwananchi wa Kijiji hicho,Aminiel Axwari  wakati akianza kutoa maoni yake alimtaja Waziri wa Maliasili na Utalii kama Waziri Mkuu jambo lililozusha vicheko kabla ya kusahihisha na Mkuu wa wilaya hiyo,Omari Qawngw’ kusema kuwa hizo ni dalili njema kwa Waziri Nyalandu ambaye ni miongoni wa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)walitangaza nia ya kuwania urais .


Nyalandu alisema serikali itatoa  kiasi cha Sh 100 milioni kwaajili ya ujenzi wa Shule ya sekondari katika Kata hiyo na kiasi cha Sh 60 milioni kwaajili ya ujenzi wa Soko litakalowesha wanawake kuuza mazao yao.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...