MWANANCHI
Mfanyabiashara wa Moshi Mjini, Lenana Marealle
amejikuta matatani baada ya kuwekwa mahabusi kwa saa tatu kwa amri ya
jaji baada ya kuvuta sigara eneo la Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.
Moshi wa sigara unadaiwa kuingia kwenye vyumba vya mahakama na kusababisha Jaji Mfawidhi, Aishiel Sumari, mawakili na karani wa mahakama kuanza kukohoa mfululizo.
Hili linaweza kuwa tukio la kwanza kwa
mhimili wa Dola kutumia mamlaka yake kuzuia uvutaji wa sigara kwenye
maeneo ya wazi ya umma licha ya Sheria inayosimamizi bidhaa za tumbaku
ya mwaka 2003 kuharamisha.
Tukio hilo limekuja miezi minne tangu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid kutoa agizo la kuzuia uvutaji wa sigara hadharani ikiwamo katika ofisi za umma.
Kwa mujibu wa Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu, Benard Mpepo, Marealle aliwekwa mahabusu iliyopo mahakamani hapo
kuanzia saa tano asubuhi hadi saa nane mchana.
Mpepo alisema Marealle aliwekwa mahabusi
kwa kosa la kuidharau mahakama chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu
kifungu 114 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Bunge mwaka 2002.
Mpepo alisema adhabu ya kosa hilo ni
kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh500, lakini ilionekana
adhabu ya kukaa mahabusi kwa muda huo inatosha kuwa fundisho kwake.
MWANANCHI
Mkurugenzi mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Hassy Kitine, ametangaza nia ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM, akisema “nipeni miaka mitano niirudishe Tanzania ya Mwalimu (Julius) Nyerere”.
Kitine alitangaza nia hiyo jana mjini
Dodoma akitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kutoa mifano ya utendaji wa
muasisi huyo wa Taifa, huku akiwaponda waliotangaza nia wengine na
kujisifu kuwa hakuna mwenye sifa za kumfikia, hasa katika elimu.
“Ninataka
kuirudisha Tanzania ya Mwalimu Nyerere… sikuwahi kutangaza wala
kuonyesha dalili zaidi ya kukaa na kutafakari katika nafsi… najua
sitaweza kufanya kama alivyokuwa Mwalimu, lakini nitasimamia katika
misingi ya utendaji ya Mwalimu Nyerere,” alisema waziri huyo wa zamani.
Alisema kuwa enzi za uhai wa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema “Ikulu si pa kukimbilia, Ikulu ni shida, Ikulu ni matatizo”, akisisitiza kuwa ofisi hiyo ya mkuu wa nchi ni matatizo na hata yeye anaiogopa.
“Mwalimu
alisema ‘ukiona mtu anakimbilia Ikulu kwa namna yoyote ile, na hasa kwa
mapesa, mapesa siyo fedha, mapesa, mapesa, mapesa mpaka yanatisha. Huyu
mtu akienda Ikulu lazima azirudishe, na (Ikulu) si pa biashara. Sasa
anakwenda kufanya biashara gani?’
“Huyu
ni wa kuogopa kama ukoma…mimi ninaijua Ikulu kuliko mgombea mwingine
yeyote. Nilikuwa Ikulu kama kiongozi, kila mlango wa chumba Ikulu
naujua, hata alipolala Baba wa Taifa. Ikulu si pa kukimbilia.
“Nimefanya
kazi Ikulu kwa muda mrefu sana, Ikulu ni shida… ninazijua Ikulu zote
Tanzania, si pa kukimbilia, Ikulu ni matatizo, matatizo, matatizo. Sasa
pamoja na matatizo hayo, nimewiwa kuchukua fomu kwa kuwa sikuona hata
anayefaa kati ya waliochukua,” Kitine.
“Wanahangaika
kwenda Ikulu, wanahangaika kwelikweli. Wapo waliotangaza nia na kujaza
viwanja vya mpira, wanajaza watu, wanafanya mbwembwe. Sasa nikaangalia
hivi kweli hawa wanataka kulitumikia Taifa kwa mbwembwe zote hizi au
wanataka kurudisha fedha zao?
“Ndiyo
maana nikaogopa sana na nimejitokeza mwishomwisho kwa kuwa Ikulu
napafahamu sana, si kidogo, sikukimbilia. Naona tabu hata nikichaguliwa,
naogopa kwelikweli, kwa sababu najua kuna matatizo sana.”
Alisema akiwa Ikulu na akiwa na miaka 30
aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, alikataa lakini Nyerere
alimlazimisha, hivyo akamwambia waendelee na watasaidiana.
NIPASHE
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema
sheria tatu za makosa ya jinai zilizo mbioni kupitishwa na serikali,
zimelenga kuwanyamazisha wapinzani kwenye uchaguzi mkuu ujao, ili
wasiweze kuanika madudu ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika taarifa yake iliyopatikana jana
jijini Dar es Salaam, Mbowe alizitaja sheria hizo ambazo ama zimesainiwa
au zinasubiri saini ya rais kuwa ni pamoja na ile ya Muswada wa Vyombo
vya Habari wa Mwaka 2015, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 na
Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015.
Alisema kuna nia moja tu inayoweza
ikaeleza ni kwa nini sheria hizi zimepelekwa mbio mbio, nayo ni kutokana
na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
“Uwingi
wa sheria hizo mpya kwa pamoja kunaweza kunyamazisha ukosoaji wa
kukosekana kwa utawala bora, na kukandamiza kile ambacho kimekuwa ni
utamaduni wa vyombo vya habari wa kuchunguza na kuripoti ufisadi, ndani
ya serikali,” alisema.
Mbowe alifafanua kwamba, Muswada wa
Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015, utawazuia waandishi wote na vyombo vya
habari kujiendesha, kuwa na baraza lao la habari, isipokuwa waandishi
wenye leseni tu.
Aidha alisema muswada huo unalenga
kudhibiti machapisho hadi majarida madogo na blogs, na kutoa adhabu kali
kwa watakaopatikana na makosa, pamoja na kuyafungia magazeti.
Kwa upande wa Sheria ya Makosa ya
Mtandao ya Mwaka 2015, alisema itaharamisha machapisho ya mtandaoni
yanayoonekana na serikali kuwa na habari za kupotosha, udanganyifu au
uongo.
Aidha, alisema sheria hiyo inatoa
mamlaka kwa polisi ya kukagua nyumba za watuhumiwa, kukamata kompyuta
zao na kutaka takwimu zao kutoka kwa watoa huduma wa mitandaoni
“Itakuwa
ni kosa la jinai kutuma barua pepe au mawasiliano mengine ya
kielektroniki bila ya idhini,” alisema. Kwa upande wa Sheria ya Takwimu
ya Mwaka 2015, Mbowe alisema inaharamisha uchapishaji wa takwimu ambazo
kwa maoni ya serikali zitakuwa ni za uongo, na adhabu yake itakuwa faini
ya Dola 6,000, au hukumu ya miaka mitatu jela.
“Mtafiti au mwandishi anaweza kwenda jela kwa kuchapisha takwimu ambazo serikali haikubaliani nazo,” alisema.
Mbowe alizitaka nchi washirika katika
maendeleo na jumuiya ya kimataifa kumsisitiza Rais Jakaya Kikwete
kutozisaini sheria hizo, na kuzirudisha tena bungeni ili mambo yote
yaliyolenga kuvisambaratisha vyombo vya habari na kukandamiza uhuru wa
kujieleza yaweze kuondolewa.
NIPASHE
Wabunge wa vyama vya upinzani mkoani
Kilimanjaro wameukoleza mgogoro unaohusu madai kuwa Mkuu wa mkoa huo,
Leonidas Gama, anahusika katika uporaji wa ardhi ya wananchi wa Rombo na
Vunjo pamoja na kushirikiana na matapeli kutoa hati ya kiwanja cha
Mawenzi, baada ya kuamua kuungana na kumwomba Rais Jakaya Kikwete amfute
kazi au kumstaafisha kwa manufaa ya umma.
Mbunge wa Vunjo (TLP), Dk. Augustine Mrema,
alisema ili kuunusuru mkoa huo kuingia katika mgogoro, anamuomba Rais
Kikwete kuingilia kati na kumfuta kazi Gama au kumstaafisha kwa manufaa
ya umma kwa madai kuwa ni dalali na mlanguzi anayefanya biashara akiwa
mtumishi wa umma.
“Namuomba
Rais Kikwete amuondoe Gama Kilimanjaro kwa sababu ya heshima yake na
serikali yake. Ni vizuri akamstaafisha kwa manufaa ya umma,” Mrema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini,
alisema wanachotaka kwa sasa mkuu wa mkoa huo arejeshe Sh. milioni 168
za halmashauri ya wilaya hiyo kwa madai zilitumika kufanya shughuli
binafsi wakati wananchi wa Rombo hawakunufaika na shughuli hiyo.
“Lakini
pamoja na kumuomba Rais Kikwete amwajibishe mara moja kiongozi huyu
(Gama) kwa kutumia madaraka yake vibaya na kujiingiza kwenye biashara
chafu; Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imchunguze
sambamba na watendaji wote wa serikali waliotumia vibaya madaraka yao
kwa kutumia fedha za umma katika kuanzisha kampuni binafsi,” Selasini.
Jumatatu iliyopita, Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Mendeleo ya Makazi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Halima Mdee,
alimlipua Gama ikimtuhumu kushiriki katika uporaji Ardhi ya wananchi wa
Rombo na Vunjo huku akishirikiana pia na matapeli katika kutoa hati ya
kiwanja cha Mawenzi mjini Moshi.
Gama anadaiwa kushirikiana na matapeli
hao kwa kutoa hati ya kiwanja cha Mawenzi chenye hati namba C.T 056035
licha ya kumilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa zaidi ya
miaka 33.
Hata hivyo, Gama jana alikaririwa na
vyombo vya habari akikanusha madai yaliyodaiwa na Kambi Rasmi ya
Upinzani kwamba anashiriki vitendo vya uporaji wa Ardhi, akisema suala
la kuwekeza kwenye ardhi ya Rombo kwa kampuni binafsi ya Jun Yu
Investment Internation Company Ltd lilipitishwa kihalali na kikao cha
ushauri cha mkoa (RCC) kwa ajili ya kujenga kiwanda cha saruji.
“Kambi
ya upinzani ifanye uchunguzi wa madai hayo na kuyatafutia ukweli.
Sijawahi kwenda nchini China kwa lengo la kuwatafuta wawekezaji hao,
kama inavyodaiwa, hivyo kambi hiyo itafute ukweli juu ya tuhuma
wanazozitoa,” Gama.
Alisema mtoto wake, Mayunga Gama,
alimweleza kuwa kuna marafiki zake wawili raia wa China wanataka
kuwekeza kiwanda cha saruji mkoa wa Dar es Salaam au Bagamoyo.
NIPASHE
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema asilimia 65 ya wanafunzi kwa sasa wanakaa katika madawati huku asilimia iliyobaki wakitarajiwa kumaliziwa tatizo hilo.
Pinda akizungumza jijini Mwanza jana
alisema serikali imefanikisha kuwaondoa wanafunzi kukaa mavumbini hadi
katika madawati kwa asilimia 65, huku 35 iliyobaki ikitarajiwa kumalizwa
wakati wowote.
“Lengo letu ni kutaka kuboresha elimu nchini na kuhakikisha kila shule inakuwa na madawati tofauti na miaka ya nyuma,” alisema.
Aidha, alizitaka halmashauri nchini
kuhakikisha kila mwaka zinatenga pesa kwa ajili ya kununulia madawati
ili wanafunzi waondokane na kukaa chini ya matofauri ama sakafuni.
Waziri Pinda alisema katika suala la
ujenzi wa maabara, lazima ziwe zimekamilika kabla ya Juni 30, mwaka huu
kama agizo la Rais Jakaya Kikwete lilivyosema.
Alisema kila halmashauri inatakiwa
kuhakikisha shule zote zinamaliza ujenzi wa maabara tatu kabla ya Juni
30 mwaka huu, ili zifanye kazi kuanzia Julai, mwaka huu.
“Kwa
sasa serikali imeashaanza kusambaza vifaa kwa halmashauri 75 nchini kwa
ajili ya maabara za sayansi katika shule hizo zinazomilikiwa na
serikali,” Pinda.
Pia aliziagiza halmashauri za wilaya
zote kuhakikisha zinapima maeneo ya shule pamoja na viwanja vyake ili
kuepukana na migogoro ya ardhi inayotokea mara kwa mara.
MTANZANIA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
amesema endapo Kamati Kuu ya CCM haitalipitisha jina lake kuwania urais
mwaka huu, kura yake ataipeleka kwa kada wa chama hicho, Profesa Mark
Mwandosya.
Amesema atafikia uamuzi huo kwa kile
alichodai kuwa yeye na Profesa Mwandosya ndio wanakidhi vigezo 13
vilivyowekwa na CCM kumpata mgombea urais.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini Mbeya, alipokuwa akitafuta wadhamini, ambapo alisema Profesa Mwandosya amebahatika kuwa na sifa zote za kiuongozi.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini Mbeya, alipokuwa akitafuta wadhamini, ambapo alisema Profesa Mwandosya amebahatika kuwa na sifa zote za kiuongozi.
“Sina
wasiwasi na mtu huyu, hata kama chama kikiliondoa jina langu, basi kura
yangu naipeleka kwake kwani yeye ndiye mwanamume aliyekidhi vigezo vyote
vilivyopitishwa na kuhalalishwa na chama,” alisema Membe huku akishangiliwa.
Aliwataka wakazi wa Mkoa wa Mbeya
kuhakikisha wanayapitisha majina mawili ya wagombea wa nafasi za urais –
jina lake na la Profesa Mwondosya.
Hata hivyo, Membe alionyesha kushangazwa
na tabia za baadhi ya watangaza nia kuwa na uchu wa madaraka kwa kutaka
nafasi zote mbili za urais na ubunge, hivyo kuwataka wananchi kuwakataa
mapema kabla jogoo halijawika.
MTANZANIA
Mkuu wa Operesheni Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Simon Siro ametoa ushahidi katika kesi inayowakabili Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba na wafuasi wake 30 na kudai mkutano huo ulipigwa marufuku kutokana na taarifa za intelijensia za kuwapo kwa tishio la ugaidi.
Siro aliyaeleza hayo jana mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Cyprian Mkeha, akiwa shahidi wa upande wa mashtaka.
Alidai Januari 23 mwaka huu walipokea
barua ya CUF ikiiarifu polisi kuwa Januari 27 mwaka huu wangefanya
mkutano na maandamano yenye lengo la kukumbuka watu waliouawa Pemba na
kulaani mauaji hayo.
Siro alisema barua hiyo ya CUF ilidai
kuwa chama hicho kimekuwa na tabia ya kuwakumbuka watu waliouawa na
kuyalaani mauaji hayo kila mwaka, Januari 27.
“Tuliipokea
barua hiyo ya CUF Januari 23, 2015 na Januari 24 na 25, timu ya
intelejensia ilifanya kazi kuona kama yanaweza kufanyika na kumalizika
kwa usalama,” Siro.
Siro alidai pia kuwa kwa kipindi kile yalikuwapo matukio ya unyang’anyi
wa silaha katika vituo mbalimbali vya polisi na kwa sababu hiyo jeshi la
polisi liliyazuia maandamano na mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika,
kwa mujibu wa sheria inayoruhusu kufanya hivyo.
Alidai polisi hawakuyaruhusu maandamano
hayo ya Januari 27, 2001 na yalikuwa haramu na hata waliouawa hawakuwa
wanachama wa CUF pekee bali hata polisi walikuwamo.
Alidai jeshi hilo liliandika barua ya
kuyapinga yasifanyike na kumkabidhi Abdul Kambaya kwa niaba ya Katibu wa
CUF na walikubaliana kuwa maandamano na mkutano hautakuwapo.
“Niliamini kuwa makubalino tuliyofanya
Januari 26 yangetekelezwa lakini Januari 27 majira ya saa 8.00
nilipigiwa simu na Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Kamishna
Zakaria ambaye aliniambia kuwa walikuwapo watu wengi wenye mabango
katika ofisi ya CUF wilaya ya Temeke.
Tukio la viongozi hao kukamatwa
lilitokea Januri 27 mwaka huu wakati Profesa Lipumba na viongozi wenzake
walipokamatwa kwa kuitisha mkutano wa hadhara kuadhimisha miaka 14
tangu wafuasi wa chama hicho kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati
wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar mwaka 2001.
Maandamano hayo ya Januari 27, mwaka huu yalianzia katika ofisi za CUF
Temeke yakiongozwa na Lipumba kuelekea viwanja vya Zakhem kwa ajili ya
mkutano wa hadhara.
HABARILEO
Leo ni siku ya Bajeti Kuu. Masikio ya
Watanzania yataelekezwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma
wakati Serikali itakapowasilisha Bajeti Kuu ya mwaka 2015/16.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya
atasoma hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa kubainisha namna ambavyo
Serikali itaweza kukusanya na kutumia kiasi cha Sh trilioni 22.480,
ambazo zimeongezeka kutoka zaidi ya Sh trilioni 19 za bajeti ya mwaka
jana, ikiwa ni ongezeko la asilimia 13.24.
Kwa siku mbili mfululizo, waziri na
maofisa wa wizara ya fedha wamejifungia ndani na Kamati ya Bunge ya
Bajeti wakichambua na kupitia kwa kina bajeti hiyo kabla ya kusomwa leo
bungeni.
Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima amewataka Watanzania waondoe hofu na kwamba bajeti itakayosomwa leo itakuwa nzuri na kwa manufaa ya wananchi wote.
“Watanzania
wategemee bajeti nzuri, tunaweka misingi kwa serikali ijayo kwa kuwa
uchui imara zaidi na maisha bora kwa watanzania wote,” alisema.
Aprili 30, mwaka huu, Mkuya alitoa
mwelekeo wa bajeti ukiwa ni zaidi ya Sh trilioni 23, huku utegemezi wa
fedha za kigeni ukipungua kutoka asilimia 14.8 ya mwaka wa fedha
uliopita hadi asilimia 8.4 kwa mwaka ujao wa fedha.
Bajeti ya mwaka 2015/16 inalenga zaidi
kupeleka umeme na huduma za maji vijijini, kumalizia miradi ambayo
haijakamilika na kutenga fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Alisema katika fedha hizo, Sh trilioni
16.71 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh trilioni 5.77
ambayo ni asilimia 25.9 zitatumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Alisema serikali inalenga kukusanya
mapato ya kodi ya jumla ya Sh trilioni 13.35 sawa na asilimia 90.1 ya
mapato ya ndani huku mapato yasiyo ya kodi ni Sh bilioni 949.2 na yale
yatokanayo na vyanzo vya halmashauri yanatarajia kuwa Sh bilioni 521.9.
Mkuya alisema Serikali inategemea kukopa
kiasi cha Sh trilioni 5.77 kutoka vyanzo vyenye masharti ya kibiashara
huku washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 1.89 sawa
na asilimia 8.4 ya bajeti, ikilinganishwa na asilimia 14.8 ya bajeti ya
mwaka 2014/15 ambazo sehemu kubwa ni mikopo ya masharti nafuu.
No comments:
Post a Comment