Pages

June 20, 2015

KWELI WA MGOMBEA URAIS NDANI YA CCM DK MUSSA MUZAMILL KALOKOLA KUPIGWA MITAMA NA WALINZI WA GREEN GUARD KATIKA MKUTANO WA HADHARA A TO Z NDIYO HII.


 
Dk Mussa Muzamill Kalokola akionyesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM baada ya kuzichukua hivi karibuni mjini Dodoma. Dk Kalokola wiki hii amekumbana na balaa baada ya kupata mkong'oto wakati akitafuta wadhamini.

Tanga\Dodoma.
Harakati za makada wa CCM wanaowania urais kusaka wadhamini mkoani zinaendelea kukumbwa na vituko baada ya wanamgambo wa chama hicho, maarufu kama Green Guards, kumshushia mkong’oto Dk Mussa Muzamill Kalokola aliyeingilia mkutano ulioandaliwa kwa ajili ya mgombea mwingine.


Tukio hilo lililotokea juzi, ni mwendelezo wa matukio kadhaa ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mchakato huo, yakiwamo ya wanachama kutaka kuchana fomu za mgombea baada ya kunyimwa ‘posho’ na kada mwingine kukosa wadhamini na kulazimika kuomba chakula cha mchana kutoka kwa mkuu wa wilaya.

Katika tukio la Tanga, Dk Kalokola, ambaye pia anadaiwa kushawishi wanachama wasimdhamini mgombea mwingine wa urais, Bernard Membe, alidaiwa kuvamia mkutano ulioandaliwa kwa ajili ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kutaka kulazimisha apewe kipaza sauti kwa ajili ya kuomba wanachama wamdhamini, kitu ambacho viongozi wa CCM wa wilaya hawakukubaliana nacho na alipoendelea kung’ang’ania ndipo Green Guards walipoamriwa wamuondoe eneo hilo.

Picha za video za tukio hilo ambazo zimesambazwa mitandaoni zinawaonyesha vijana hao wa Green Guards wakimsomba mzobemzobe mgombea huyo, kumuangusha kwa kumpiga ngwala na mkoba wake wenye stika ya fomu za mgombea urais, ukionekana kuzagaa chini.

Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu mkasa huo, Dk Kalokola alikiri kupigwa katika tukio hilo lilitokea mchana Jumatano ya Juni 17, 2015 alipofika kwenye ofisi za CCM za Wilaya ya Tanga Mjini, siku ambayo mgombea huyo anadai alipangiwa na katibu wa wilaya.

Dk Kalokola alisema baada ya kukabidhiwa fomu za kuomba kuteuliwa na CCM Julai 15 mwaka huu mkoni Dodoma, alikwenda mkoani Tanga ili kupata wadhamini.

“Tulielekezwa kuwa makatibu wa CCM wa mikoa ndiyo watakaotutafutia wadhamini siyo sisi tutafute hivyo mimi tarehe 16 nilikwenda ofisi za CCM kuripoti kwa katibu wa Mkoa,” alisema.

Hata hivyo, alisema hakuweza kuonana na Katibu huyo baada ya kuambiwa kuwa hayupo na amemwachia majukumu hayo katibu wa CCM wa Wilaya ya Tanga Mjini.

Alisema siku hiyo alikuta wagombea wawili waliofika ofisi hizo wakitaka kupewa wadhamini ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Balozi Amina Salum Ali.

“Hawakutaka hata kunisikiliza shida yangu. Mimi nikaamua kutoa taarifa makao makuu ya CCM,” alisema.

Hata hivyo, baadaye saa 12:00 jioni alipigiwa simu na katibu wa CCM wilaya hiyo ya Tanga, akielezwa kuwa aende siku inayofuata asubuhi yaani Alhamisi.

“Nilienda pale nikasaini kitabu nikawaeleza kuwa mimi jana (juzi) nilikuwa na kesi ya kupinga Katiba jijini Dar es Salaam kwa hiyo ningeomba nipate wadhamini siku hiyo hiyo ili nisafiri,”alisema Dk Kalokola ambaye amefungua kesi akitaka Mahakama Kuu itangaze kuufuta mchakato wa kupata Katiba mpya kinyume cha utashi wa chama hicho tawala ambacho kinajisifu kwa kufanikisha mchakato huo.

Dk Kalokola, ambaye wakati anachukua fomu pia aliiponda CCM akidai inaiba sera za wapinzani, alisema siku iliyofuata alikubaliwa na kutakiwa kurejea saa 6:00 mchana.

“Nilipofika nikakutana na vijana wa Green Gurd wakiwa mlangoni, wakanipiga ngwala wakiniambia huu ni mkutano wa Lowasa, nikawaambia kuwa mimi nakwenda kumuona Katibu nina ahadi naye,” alisema.

“Wakaendelea kunipiga lakini kinachonisikitisha vijana hawa wamekuwa wakija nyumbani kwangu kuniomba msaada, hata sare walizovaa niliwanunulia mimi… sasa cha kushangaza wagombea wako 37 kama kila mgombea mmoja siku moja katika kila mkoa tutamaliza lini zoezi hili?” alihoji.


Alisema kutokana na kipigo hicho, hajaweza kupata wadhamini kwenye mkoa huo ambao alipanga kuanzia kutafuta wadhamini.

“Kesho (leo) ndiyo nitaanza tena baada ya kutoka mahakamani juzi (Alhamisi). Hadi sasa sijapata wadhamini hata kwenye mkoa mmoja,”alisema.

Dk Kalokola alisema tukio hilo mbali ya kulitolea taarifa makao makuu ya CCM, pia ameliripoti kituo cha Polisi cha Chumbageni.

Lakini katibu mwenezi wa CCM wa Wilaya ya Tanga, Lupakishyo Kapange alisema kuwa alilazimika kuwaamuru Green Guard wamuondoe kwa sababu mtangazania huyo alikuwa aking’ang’ania kupewa kipaza sauti ili azungumze katika mkutano uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya Lowassa.

“Alikuja hadi nilipokuwa nikitangaza, akataka kuninyang’anya kipaza sauti, nilipomuomba afuate taratibu za kuandaliwa mkutano wake kwa sababu huu ulikuwa wa mtangazania mwingine, hakutaka kunielewa akang’ang’ania nikaamua kuwaita Green Guards wa CCM hapa Tanga wamuondoe,” alisema Kapange.

Katibu wa CCM wa wilaya, Lucia Mwilu alisema Dk Kaloloka, ambaye ni mkazi wa Tanga, alifika ofisini kwa mara ya kwanza Juni 15 wakati wa mapokezi ya Membe na alikuwa akiwazuia wanachama waliokuwa wakitaka kumdhamini mgombea huyo.

“Nilimwita na kumuomba afuate taratibu zilizopo kwenye fomu za wagombea urais, lakini nikakubaliana naye tukutane Juni 16 mchana ili anipe fomu zake hatimaye niweze kumuandalia taratibu za kudhaminiwa. Hakufanya hivyo badala yake akamvamia katibu mwenezi,” alisema Mwilu.

Alifafanua kuwa tukio la kumondoa Dk Kalokola lilitokea saa 7:50 mchana wakati wanachama wa CCM wakimsubiri Lowassa nje ya jengo la chama hicho la mkoa wa Tanga, lakini waziri huyo mkuu wa zamani na timu yake aliwasili Tanga saa 12:00 jioni.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, kamanda wa polisi wa mkoa, Zubery Mwombeji alisema Dk Kalokola alitaka kutumia jukwaa la Lowassa kuwapata wadhamni, wakati ni kinyume na taratibu za CCM.

Alisema baada ya hapo alikwenda kituo cha polisi kuomba aruhusiwe kutumia jukwaa hilo, lakini ofisa upelelezi alimtaka aende kuonana na viongozi wa CCM Kwa sababu suala hilo haliko chini ya polisi.

Watu walioshuhudia tukio hilo waliieleza Mwananchi kusitikishwa kwao na kitendo cha kada huyo kushambuliwa, lakini wamesema baadhi yao walimsihi Dk Kalokola afuate taratibu lakini hakutaka kuwasikiliza.

“Sikufurahishwa na alivyofanyiwa Dk Kalokola lakini naye kwanini avamie mikutano ya wenzake? Juzi aliwazuia wana-CCM wasidhamini Membe, leo tena kaja hapa kuleta tafrani,”alisema Mwahija Omari mkazi wa Tanga.MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...