Pages

May 23, 2015

MEMBE, LOWASSA NA SUMAYE WATOKA KIFUNGONI NDANI YA CCM DODOMA.


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye (katikati) akifurahia jambo na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Stephen Wasira kabla ya kuanza kwa kikao cha CC, makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma jana. kushoto ni Mjumbe wa Kamati hiyo, Adam Kimbisa Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. 
Mpambano mkali wa kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM sasa umeanza rasmi baada ya Kamati Kuu ya chama hicho tawala kuwaweka huru makada sita waliokuwa wamefungiwa kwa takriban miezi 17 kwa makosa ya kukiuka kanuni za uchaguzi. 


Kufunguliwa kwa makada hao, ambao baadhi yao wanapewa nafasi kubwa ya kupitishwa na chama hicho, kumekuja wakati CCM ikikabiliwa na tishio la kutokea mgawanyiko mkubwa, hasa kutokana na baadhi ya kambi kuituhumu sekretarieti kuwa inabagua baadhi ya wagombea.

Makada waliofungiwa tangu Februari, 2014 kwa kosa la kuanza kampeni mapema ni mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, ambaye kwa sasa ni mbunge wa Monduli.

Wengine ni Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Steven Wasira (Waziri wa Kilimo na Chakula), January Makamba (Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia), na mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Baadhi ya wanachama wa CCM, hasa wajumbe wa Halmashauri Kuu, walianza kumiminika nyumbani kwa makada hao mara baada ya kupata taarifa za kuondolewa kwa adhabu hiyo, wengi wakionekana kwenda kumpongeza Lowassa.

Kufunguliwa kwa makada hao ni mwanzo wa kinyang’anyiro kikali cha kuwania kumrithi Jakaya Mrisho Kikwete kwenye nafasi ya urais na mwenyekiti wa chama hicho kikongwe na dalili zote za kuwapo kwa vita kali zilianza mara moja jana baada ya kutangazwa kwa uamuzi huo.

Makamba: Safari ya ushindi 
“Nimefurahishwa na uamuzi wa Kamati Kuu. Safari ya ushindi sasa inaanza,” alisema Makamba alipohojiwa kuhusu tamko hilo la Kamati Kuu.

“Sijashangaa hata kidogo (kusikia uamuzi huo) kwa kuwa sijawahi kukiuka maadili ya chama. Sasa nasubiri muda wa kampeni kutangazwa ili nianze kufanya hivyo kwa kuzingatia kanuni za chama kwa sababu najua wakati wa mchujo wa wagombea, CCM itaangalia tena jambo hili.”

Ngeleja: Nasubiri muda 
Ngeleja, ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini, aliishukuru Kamati Kuu kwa kufikia uamuzi huo akisema imezingatia misingi yote ya haki na kwamba kilichobaki ni kusubiri muda wa kampeni.

“Hatua inayofuata ni kuhakikisha kwamba nafuata kanuni, taratibu na miongozo ya chama katika kugombea nafasi nitakayoiomba,” alisema mbunge huyo wa Sengerema.

Lowassa: Safari ya matumaini
Hali ya kusubiri filimbi ya kampeni ipulizwe pia ilionekana kwa Lowassa ambaye alijitetea kuwa ni muadilifu na anayeipenda CCM kwa dhati.

“Sasa ninaanza safari ya matumaini. Niliianzisha mwaka juzi kule Arusha, nilisema niungane na watu katika safari hii nashukuru wameniunga mkono,” alisema waziri huyo mkuu wa zamani.

“Ninachotaka tuungane zaidi, tutaianza rasmi safari yetu niliyosema ya miba, mabonde, misukosuko na sasa tumefikia mahali… Mei 30 nitatangaza rasmi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid,” aliongeza Lowassa.

Membe: Idumu CCM 
Naye Membe alipotafutwa kwa simu kuhusu hatua hiyo ya Kamati Kuu ya CCM, simu yake iliita bila kupokewa lakini alipotumiwa ujumbe mfupi, alijibu: “Kidumu Chama cha Mapinduzi.”

Sumaye: Tunasubiri maelezo
Sumaye, ambaye alikuwa waziri mkuu wa Serikali ya awamu ya tatu kwa kipindi chote cha miaka 10, alisema kimsingi kifungo kilikwisha tangu Februari mwaka huu, lakini anashukuru kwamba CCM imekaa na kufikia uamuzi huo hivyo anasubiri kupata taarifa rasmi na taratibu za kufuata kwa wagombea wote wa chama hicho.

“Nimeona tu kwenye vyombo vya habari lakini naamini kutakuwa na maelekezo kwa wagombea wote wa urais kwa maana sasa tupo kundi moja,” alisema Sumaye.

Aliongeza kwamba kwa kuwa wamefunguliwa ikiwa imebaki miezi mitano kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, itabidi wagombea wanaodhani wamechelewa kujinadi kwa wananchi watumie nguvu ya ziada.

Uamuzi ulivyokuwa 
Jana, akitangaza uamuzi wa Kamati Kuu mbele ya waandishi wa habari, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema chombo hicho kimeridhia mapendekezo ya Kamati ya Maadili ya kumalizika kwa kipindi cha adhabu kwa makada hao.

“Kamati Kuu imeridhia mapendekezo ya Kamati ya Maadili ya kumalizika kwa kipindi cha adhabu na kuwataka kuendelea na shughuli zao,” alisema Nape saa moja baada ya kuanza kikao cha CC kwenye ukumbi wa White House mjini hapa.

Alisema Kamati Kuu ya CCM imewataka makada hao na wengine kusoma, kuheshimu, kuzingatia kanuni ili wasikumbwe tena na adhabu.

“Hawa na wengine watakaoingia katika uchaguzi taarifa zao zitatumika wakati wa kuchuja wagombea, kupima na kuamua kama wanafaa katika nafasi zao walizoomba,” alisema Nape.

Akijibu taarifa zilizoandikwa katika mitandao ya jamii, kuwa makada hao wamepewa barua ya onyo, Nape alisema taarifa hizo ni za uongo.

“Huko nje kuna presha kubwa ya makambi, taarifa nyingi mtadanganywa mtafute source (vyanzo) zilizo sahihi,” alisema.

Awali kabla ya kuanza kwa kikao hicho kulikuwa na taarifa kuwa Kamati ya Maadili ilitangaza makada wengine wenye nia ya kugombea urais waongezwe kwenye kundi la adhabu kutokana na kukiuka kanuni na taratibu za chama.

Habari zilizopatikana awali zinasema kuwa Kamati Kuu ilizingatia masuala mengi kabla ya kufikia uamuzi huo, hasa uwezekano wa chama kugawanyika iwapo wangeendelea kuwadhibiti baadhi ya makada.

Nape asema mkutano huo ni mgumu. 
“Mkutano huu utakuwa ni mgumu kutokana na una tension (hofu) kubwa iliyopo ndani na nje,” alisema Nape kabla ya Kamati Kuu kuanza kikao.

Nape alisema anafahamu kuwa watu walioko nje wanataka kufahamu kuhusu ratiba ya zoezi la uchukuaji fomu na hatma ya makada sita walio chini ya uangalizi kwa tuhuma za kuanza kukiuka kanuni.

Mambo yalivyokuwa
Tangu Jumatatu kumekuwa na mfululizo wa vikao, kuanzia kikao cha sekretarieti kilichokutana kwa siku mbili, na kufuatiwa na kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili ambayo mwenyekiti wake ni Makamu Mwenyekiti wa Chama, Philip Mangula, kilichofanyika kwa siku mbili Jumatano na Alhamisi. Kamati hiyo inafanya kazi na Tume ya Udhibiti na Nidhamu ambayo zamani ilikuwa ikiitwa Kamati ya Usalama na Maadili.

Alhamisi jioni Kamati ya Maadili, ambayo ni kubwa iko chini ya mwenyekiti wa CCM, ilikutana juzi jioni na kuendelea hadi usiku wa kuamkia jana.

Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa, sintofahamu kuhusu adhabu ya makada sita iliendelea kuisumbua jana asubuhi na Kamati Ndogo ya Maadili ililazimika kukaa tena na baadaye saa 6:00 hadi saa 7:00 mchana kukawa na kikao kilichoelezwa cha dharura cha Kamati ya Maadili chini ya Mwenyekiti Kikwete.


Taarifa za ndani kwenye kikao cha maadili zinadai kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka makada wengine waongezwe kwenye adhabu. Hoja nyingine ilikuwa ya kutaka makada sita adhabu yao iendelee iliyodaiwa kutolewa na makamu mwenyekiti, lakini alipingwa na Katibu Mkuu Abdulrahmani Kinana.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wetu, Kinana alisema kufanya hivyo ni kama vile chama kinataka kumuumiza mtu mmoja bila ya kumtaja. Ilidaiwa hoja ya Kinana iliungwa mkono na Kikwete aliyesema makada hao sita wote wapelekewe kwenye kura wakapambane wote.

Nje ya ukumbi 
Kwakuwa vikao hivyo ni vya ndani na vinahusu wajumbe wachache, hakukuwa na makundi makubwa ya makada ndani ya uzio wa jengo la CCM. Nje ya uzio kulikuwa na watu wachache kwa kuwa wajumbe wengi walikuwa hawajaanza kufika.

Nyumbani kwa Lowassa 
Baada ya taarifa za kufunguliwa makada sita, baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu na wana-CCM walianza kumiminika nyumbani kwa Lowassa kumpa mkono wa hongera kwa kutoka ‘kifungoni’.

Waliokwenda kwa Lowassa ni Nazir Karamagi, Daniel Nsanzugwako, Peter Serukamba, Salum Mbuzi, Khamis Mbeto, Kilumbe Ng’enda na Robert Lowassa.

Kabla ya CC 
Akizungumzia kuhusu kubadilika kwa ratiba hiyo, Nape alisema kumetokana na kuwepo kwa kikao cha Kamati ya Maadili.

“Kikao kitaanza muda mfupi baada ya kumalizika kikao cha kamati ya maadili,”alisema Nape. Hata hivyo, kikao hicho kilichoanza saa 6:00 mchana kilichukua zaidi ya saa moja na kilipomalizika waliahirisha hadi saa 10.00 jioni. Wajumbe 29 kati ya 32 ndio walihudhuria kikao hicho.MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...