Pages

April 1, 2015

JESHI LA POLISI LAMWACHIA HURU ASKOFU WA KANISA LA UFUFUO JOSEPHAT GWAJIMA BAADA YA KUTOKA HOSPITALINI DAR ES SALAAM.

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, akisaidiwa kusukumwa katika baiskeli ya miguu mitatu alipowasili katika Kituo cha Polisi cha Osterbay, jijini Dar es Salaam jana baada ya kutoka hospitali alikokuwa amelazwa ili kumalizia mahojiano na Jeshi la Polisi. PICHA: HALIMA KAMBI

Askofu wa Kanisa la Ufunuo na Uzima, Josephat Gwajima (pichani), ametolewa hospitali na Jeshi la Polisi kumwachia bila masharti yoyote. 

Askofu Gwajima, ambaye alilazwa katika Hospitali ya TMJ kwa siku nne baada ya kuugua ghafla wakati akihojiwa na polisi, alitolewa katika hospitali hiyo jana saa 6:15 mchana na maofisa wa jeshi hilo waliovalia nguo za kiraia. 

Maofisa hao waliofika saa 6:15 mchana wakiwa kwenye magari mawili na kuingia moja kwa moja hadi chumba alichokuwa amelazwa muda mfupi baadaye,walitoka wakiwa na Askofu Gwajima aliyekuwa amebebwa kwenye machela akisaidiwa na wafuasi wake kuisukuma. 

Askofu Gwajima aliingizwa katika moja ya magari ya polisi lililofika katika hospitali hiyo kumchukua. 

Dakika chache baadaye, alipakiwa kwenye gari hilo na kuondoka hadi katika kituo cha polisi cha Oysterbay, ambako waliwasili saa 6: 50 mchana. 
Alipofikishwa katika kituo hicho, aliingizwa katika Kitengo cha Upelelezi Mkoa wa Kinondoni akiwa kwenye machela, huku akifuatana na Wakili wake, John Mallya, na kuruhusiwa huku akielezwa kuripoti kesho katika Kituo cha Polisi cha Kati. 

Hata hivyo, ilichukua muda wa takriban saa moja na nusu kukamilisha taratibu huku waandishi wa habari na wafuasi wake wakiwa nje wakimsubiri. 

Baada ya kuruhusiwa akiwa ndani ya gari lake akizongwa na umati wa watu, alisema afya yake imeimarika. 

Alisema wachungaji wanapaswa kuheshimiwa kutokana na kauli wanazozitoa. 

Askofu Gwajima alisema kwa sasa anaenda kupumzika, hivyo akalitaka jeshi hilo kutotumia nguvu katika kupata mwafaka. 

Nje ya kituo cha polisi Oysterbay, mamia ya waumini wa Askofu Gwajima walifurika wakisubiri kujua hatima ya kiongozi wao.Wafuasi hao waliokuwa wamevalia mavazi ya kiuchungaji, walionekana wakirandaranda nje ya viwanja vya kituo hicho. 

Baada ya kuruhusiwa, wafuasi hao waliruka ruka kwa furaha, huku wakiimba nyimbo za kumtukuza Yesu Kristo na kulisukuma gari lililombeba. 

Baadhi ya waumini waliamua kutembea kwa miguu kutoka kituo hicho hadi kanisani kwenye viwanja vya Tanganyika Pakers, huku wakiwa wanaimba na kushikilia matawi ya mti. 

Katika kituo kikuu cha polisi, waumini hao walipiga kambi na walianza kumiminika saa 3.00 asubuhi na kusababisha eneo hilo kufurika watu. 
Ulinzi ulikuwa umeimarishwa katika eneo hilo na baadhi yao waliondolewa, hivyo kulazimika kusambaa maeneo yaliyo karibu na kituo hicho, huku wachache wakiruhusiwa kuingia eneo la kituo. 

Kumiminika kwa wafuasi hao katika kituo hicho kulitokana na taarifa zilizoeleza kwamba Askofu Gwajima angefikishwa katika kituo hicho kwa ajili ya hatua nyingine za kipolisi. 

Majira ya saa 6:35 mchana, walipata taarifa kwamba anapelekwa Osterbay, hali iliyoulazimisha umati wa waumini hao kukodi magari kuelekea huko. 

Awali, maaskofu wa makanisa ya Kipentekoste walikuwa wamepanga kwenda kuonana na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, kuzungumzia suala la Askofu Gwajima. 

Hata hivyo, walishindwa kumuona IGP, huku baadhi yao wakianzia katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, ambaye hata hivyo hawakufanikiwa kumuona kutokana na kuwa nje ya ofisi. 

Wakili wake, Mallya, alisema aliruhusiwa bila masharti. 

Imeandikwa na Gwamaka Alipipi, Elizabeth Zaya na Enles Mbegalo. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...