Pages

March 26, 2015

WAZIRI WA ARDHI MHE. WILLIAM LUKUVI AWASILI MKOANI RUKWA , AAHIDI SULUHU YA MGOGORO WA MUDA MREFU WA SHAMBA LA SKAUNGU

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiwasili katika uwanja wa ndege wa Mjini Sumbawanga leo tarehe 25/03/2013 kwa ajili ya ziara ya siku mbili Mkoani Rukwa moja ikiwa kufuatilia migogoro sugu ya ardhi ukiwemo wa shamba la Skaungu ambapo ameonana na wananchi na viongozi wa vijiji kumi vinavyolizunguka shamba hilo ambalo lina mgogoro wa muda mrefu kati ya Mmiliki Ephata Ministry na wananchi hao. Lengo la pili la ziara yake ni kuweka jiwe la msingi katika nyumba za makazi zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katikati ya Mji wa Sumbawanga.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya (kulia) akimtambulisha Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi kwa viongozi wa Serikali na Chama Mkoa wa Rukwa muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Sumbawanga.
Katika msafara wake Mhe. Waziri aliongozana na Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini Mhe. Aeshi Hillal (Pichani na Mdau Juddy Ngonyani wa Channel Ten), Mbunge wa Jimbo la Kwela Mhe. Ignas Malocha na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya. 
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akizungumza na viongozi wa Vijiji kumi vya kata za Mollo na Msandamuungano vinavyozunguka sahamba la Skaungu lenye Mgogoro wa muda mrefu kati ya muwekezaji Ephata Ministry na wananchi wa vijiji hivyo. Mhe. Waziri amesema lengo la kufika kwake Mkoani Rukwa ni kuona maeneo ya mgogoro huo pamoja na kuwasikiliza wananchi na baadae kuonana na muwekezaji huyo kabla ya Serikali kufanya uamuzi wa hatma ya shamba hilo ambalo linadaiwa na wananchi kumega maeneo ya vijiji na hivyo kukosa maeneo ya kulima kutokana na ongezeko la watu. Alieleza kuwa taarifa zote kuhusu shamba hilo zimeshaifikia ofisi yake na kilichobaki ni kutoa uamuzi wa Serikali wa kumaliza Mgogogoro huo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi alipofika katika Kijiji cha Skaungu kuongea na wananchi alipokelewa na mabango yenye ujumbe mbalimbali unaolenga kuiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa ardhi yao ambayo ipo ndani ya shamba la Muwekezaji Ephata Ministry. Mhe. Lukuvi amewatoa hofu wananchi hao kuwa mgogoro huo utapata ufumbuzi kabla ya Serikali ya awamu ya nne haijamaliza muda wake.
 Ujumbe mwingine uliokuwa kwenye mabango hayo.
Ujumbe mwingine ukinyesha kuwa toka Kijiji hicho kianzishwe mwaka 2008 na kupewa hati wananchi hao wamekuwa hawana haki na sehemu ya ardhi yao ambayo ipo ndani ya shamba la Muwekezaji huyo. 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Skaungu muda mfupi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi kuzungumzia lengo la ziara yake katika Kijiji hicho, alisema ni muda sasa kumaliza mgogoro huo.  

 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi (kulia) akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Skaungu leo tarehe 25/03/2015. Alisema kuwa mgogoro huo unawanyima usingizi viongozi wa Serikali na imefika wakati sasa kuumaliza. Aliongeza kuwa iwapo Serikali itaamua sehemu ya shamba hilo irudi kwa wananchi basi halitagawiwa kiholela na badala yake utatumika utaratibu maalum kwa kushirikisha Halmashauri na Serikali ya Kijiji kwa kuanza kuwatambua wale wenye hitajio kubwa la ardhi na baadae kuwaangalia wananchi wengine wenye haki ya kupatiwa maeneo hayo.
 Wadau wa Habari Mkoa wa Rukwa wakitoka kuchukua matukio katika Kijiji cha Skaungu, Kutoka kulia ni Juddy Ngonyani (Channel Ten), Nswima Errrrrnest (TBC), Joshua Joel (ITV), Peti Siame (Habari Leo/Daily News), Gurian Adolph Ndingala FM na Mussa Mwangoka (Mwananchi).
 Bi. Anna Msafiri Mwananchi wa Kijiji cha Mawenzusi akitoa kero yake kwa Mhe. Waziri wa Ardhi.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Mawenzusi ambao pia walipata fursa ya kupaza sauti zao kwa Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi.
(Na Hamza Temba - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa@Rukwareview.blogspot.com)

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...