Mahakama mkoani Dodoma imefuta dhamana ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja kutokana na kukiuka masharti ya
dhamana aliyopewa ikiwemo ya kutowazuia wafanyabiashara kufunga maduka
yao wakati kesi yake ikiendelea mahakamani
Akitoa taarifa mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa wa Dodoma,
Rebecca Mbilu, Mwendesha mashtaka wa serikali Rose Shio amesema kuwa
upelelezi dhidi ya kesi hiyo umeshakamilika na kuiomba mahakama kutengua
dhamana ya mshtakiwa kutokana na kukiuka masharti ya dhamana aliyopewa.
Amesema kuwa pamoja na hilo Mwenyekiti huyo amekuwa akiendelea
kufanya mikutano na wafanyabiashara kwa ajili ya kuwahamasisha
wasiendelee kulipa kodi kwa kutumia mashine za kielektroniki za efds
kitenda alichosema kuwa ni kukiuka masharti ya dhamana aliyopewa.
Hata hivyo wakili wa mshtakiwa, Godfrey Wasonga ameiambia mahakama
kuwa tangu mteja wake apewe dhamana ahajawahi kuitisha mikutano na
wafanyabiashara kwani hata juzi hakuwa na mkutano bali wafanyabiashara
waliokuja mjini Dodoma kusikiliza kesi ya mwenyekiti huyo, waliposikia
kuwa yupo Dodoma walikwenda kumsalimia baada ya kupata taarifa kuwa yuko
katika hoteli ya Image Hill.
Na kuhusu suala la kufunga maduka mwenyekiti huyo hakuwashawishi
wafanyabiashara nchini kufunga maduka yao bali ni wafanyabishara wenyewe
ndo walioamua kufunga maduka yao kwa ajili ya kwenda kusikiliza kesi ya
mwenyekiti wao.
Hata hivyo hakimu Mbilu amesema kuwa ameridhika na hoja za upande wa
mashtaka na hivyo akatengua dhamana ya Minja na kumtaka kubaki rumande
hadi April Mosi mwaka huu ambapo kesi yake itatajwa tena.
Amesema kuwa kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa maelezo ya awali April 9 mwaka huu kutokana na ushahidi wa kesi hiyo kukamilika.
Mpekuzi blog
No comments:
Post a Comment