Pages

March 11, 2015

MGOGORO WA CHUO KIKUU CHA ST JOSEPH ARUSHA CAMPUS WAPATA SURA MPYA

Aliyekua Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St Joseph tawi la Arusha ,Irmia Edara akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ,Kisongo mkoa wa Arusha juu ukiukwaji wa taratibu za mikataba ya ajira na uongozi.

Baadhi ya wanafunzi waliohudhuria mkutano na waandishi wa habari ,Kisongo mkoa wa Arusha ambao pamoja na mambo mengine walilaumu Menejimenti ya Chuo juu ukiukwaji wa taratibu za taaluma na upungufu wa vifaa vya maabara

 
Mwandishi Wetu,Arusha
Mgogoro wa muda mrefu uliokikumba  Chuo Kikuu cha St Joseph tawi la Arusha ambao umekua kati ya wanafunzi na uongozi wa Chuo hicho  sasa umechukua sura mpya baada ya  mmoja wa Waadhiri wake kutoka nchini India kufukuzwa kazi ghafla.

Katika mkutano na waandishi wa habari  jijini hapa,Mhadhiri huyo,Irmia Edara alisema taasisi ya St Joseph ambayo makao yake makuu yapo nchini India imekua ikitumia udanganyifu kukusanya fedha kwa kisingizio cha kuwasaidia waafrika lakini imekua ikijinufaisha.

Alidai katika makubaliano ya awali akiwa na wafanyakazi wenzake 45 kutoka India walikubaliana kufanyakazi nchini Zambia kwenye taasisi hiyo kwa malipo ya dola za kimarekani 2,000 sawa na Sh 3.6 milioni  lakini waliamua kuwabadilishia mikataba yao kuja Tanzania kama wafanyakazi wa kujitolea.

“Tunasikitishwa na kitendo kinachofanywa na uongozi wa St Joseph,haujali haki za binadamu wala taaluma wanayoipata  wanafunzi kwa kuwaweka Waadhiri katika mazingira magumu na vitisho bila sababu za msingi huku haki zetu zikikiukwa,”alisema Irmia

Alisema walilazimishwa kusaini mikataba mipya ya kujitolea kwakua taasisi hiyo ni kidini na kuanza kulipwa chini ya asilimia 50 ya malipo ya mkataba wa awali jambo ambalo limeyafanya maisha yao kuwa magumu hapa nchini.

Hata hiyo alidai pamoja na udanganyifu unaofanywa na Chuo hicho  kuwatoza fedha zaidi za kuwapatia vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini pia wapo raia wa kigeni wanaoishi bila vibali licha ya taarifa  kufikishwa kwenye Idara ya Uhamiaji mkoa wa Arusha .

Akijibu madai hayo,Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Arusha,Danson Mwakipesile alisema ofisi yake imepata malalamiko kutoka kwa waadhiri  hao ya kukiukwa kwa malipo kulingana na mikataba yao na kuwaagiza kwenda Idara ya Kazi kwaajili ya kulitafutia suluhu suala hilo.

“Kuhusu kuwepo wafanyakazi wasio na vibali katika Chuo hicho bado sijapata taarifa rasmi lakini nikuhakikishie nitalifuatlia,taarifa nilizonazo ni malalamiko ya kukiukwa kwa masharti ya ajira zao na tumewalekeza mahali sahihi,”alisema Mwakipesile

Uongozi wa taasisi hiyo unalaumiwa  na wanafunzi kwa kuendesha Chuo bila mitaala inayotambulika na mamkala ya Vyuo Vikuu nchini(TCU) huku wakiwa na Waadhiri wasiokidhi sifa zinazotakiwa na kuwafukuza wanafunzi bila kusikilizwa.

Wanafunzi wa mwaka pili,Thadeus Thomas na Mathayo Abas walisema wanashangazwa na ukimya wa serikali kuchukua hatua zinazofaa na kuacha Chuo kizalishe wahitimu wasio na sifa katika soko la ajira.
Uongozi wa St Joseph haukuweza kupatikana mara moja kutokana na simu zao kutokupokelewa.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...