Pages

March 22, 2015

BUNGE: ZITTO KULIPWA MAFAO YAKE YOTE

Ikiwa ni siku moja tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kutangaza kung’atuka katika nafasi yake ya ubunge, Bunge limeeleza kuwa mbunge huyo atapata mafao yake yote kama wabunge wengine.
Zitto ambaye alitangaza juzi bungeni kuwa anaondoka baada ya kuvuliwa unanachama wa Chadema aliahidi kuwa ‘Mungu akipenda’ atakuwa tena ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria Novemba mwaka huu baada ya uchaguzi mkuu.Kuondoka kwa mbunge huyo pia kunaifanya nafasi ya uenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali(PAC) kuwa wazi kwa kuwa ndiye aliyekuwa akiishikilia hadi alipotangaza rasmi juzi kuachia ubunge.
Akizungumzia uamuzi wa Zitto na juu ya mafao yake baada ya kuamua kuondoka mwenyewe, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema kuwa mbunge huyo atalipwa mafao yake yote.
“Unajua Chadema wametangaza kumvua uanachama Zitto lakini hawajampa barua, sasa yeye ameona kuwa kuliko kuendelea na ubunge wake ni vyema akakaa kando. Kutokana na suala hilo atalipwa tu mafao yake yote,”alisema Joel.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa PAC wamesikitishwa na kuondoka kwa Zitto kabla ya muda wa Bunge la 10 kumalizika huku wakimwelezea ni kiongozi aliyeweza kuwaunganisha katika kamati bila kujali itikadi za vyama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wajumbe hao walisema aliwafanya wajumbe wa kamati hiyo kuwa familia na aliwaamini na kuwaheshimu wote.
“Ni mtu aliyekuwa na ushirikiano na aliweza kutuunganisha bila kujali itikadi.
"Alitufanya kama familia na alituamini na kutuheshimu. Tunamtakia kila la kheri katika mipango yake ijayo,”alisema Ismail Aden Rage (Tabora Mjini).
Mbunge wa Mkwamtipura, Kheir Ali Khamis alisema kujiuzulu kwa Zitto ni suala la Kikatiba asingeweza kuendelea kushika nafasi hiyo.
“Hili ni suala la Kikatiba haki ya kuwa mbunge inaondolewa ukishakuwa si mwanachama wa chama cha siasa,”alisema.
Alisema kutojiondoa mwenyewe kungeleta mgogoro kati yake na chama chake kwa kuwa tayari walishamvua uanachama.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy alisema kuondoka kwa Zitto kunalenga katika kujipanga upya katika chama chake kipya cha siasa.
“Yeye ni mwanasiasa atakaa hivi hivi? Na kwenye chama chake ameshafukuzwa anaenda kukijenga chama chake cha ACT ili katika uchaguzi ujao apate madiwani na wabunge,”alisema Keissy.
Mbunge wa Ludewa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Deo Filikunjombe alisema, “Zitto alikuwa kama baba ndani ya kamati na kuondoka kwake kutaifanya kamati kuyumba.”
Filikunjombe ambaye ni rafiki wa karibu wa Zitto alisema kamati hiyo itayaenzi mazuri yake na kwamba kazi alizozifanya ndani ya Bunge zitaendelea kukumbukwa.
Hata hivyo, Filikunjombe alisema,“Zitto bado hajafukuzwa kwa sababu hajapewa barua rasmi ila yeye mwenyewe ameamua kukaa pembeni kutokana na maneno yanayoendelea kusemwa pamoja na ukimya wa chama chake.”

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...