Rais Barack Obama.
Kauli ya Rais Barack Obama ya kuwataka Wakristo kujua kuwa Uislamu si
dini pekee inayohusishwa na vurugu na mauaji, imezua kizaazaa duniani na
baadhi wameanza kuhoji kama kiongozi huyo wa kwanza mweusi wa Marekani
ni Mkristo.
Obama alitoa
kauli hiyo Jumatano wakati wa Siku ya Taifa ya Maombi (National
Breakfast Prayer) alipofananisha Vita vya Msalaba na vitendo vya ugaidi
vinavyofanywa na vikundi vya Kiislamu vyenye imani kali.
“Hadi
tutakapokuwa juu ya farasi na kufikiri kuwa jambo hili ni la pekee kwa
baadhi ya sehemu, kumbuka kwamba wakati wa Vita Vitakatifu (crusades) na
Mahakama ya Kanisa Katoliki (Inquisition), watu walifanya vitendo vya
kutisha kwa Jina la Kristo,” Obama alikaririwa na Shirika la Habari la
AFP akizungumza kwenye hafla hiyo Jumatano.
“Na katika nchi yetu, utumwa na sheria za kibaguzi (Jim Crow), zote pia zilihalalishwa kwa jina la Kristo.”
Obama
alikuwa akitoa hotuba yake kuhusu dini kwenye hafla hiyo iliyofanyika
Washington, D.C. Akitumia maandiko ya dini za Kiislamu, Kiyahudi na
kikristo, Obama alisifu imani yake.
“Utamaduni wa maombi
umetuweka pamoja, ukitupa nafasi ya kukusanyika kwa unyeyekevu mbele ya
Mungu na kutukumbusha nini kinatakiwa kushirikiana kama watoto wa
Mungu,” alisema.
Obama pia aliwageukia magaidi wa kijihadi
aliosema “wanaasi Uislamu”. Alilinyooshea kidole kundi la Islamic State
ambalo alisema “limefanya vitendo visivyoweza kutamkwa vya ukatili “
Mashariki ya Kati pamoja na wanamgambo ambao hivi karibuni waliua watu
kadhaa kwenye ofisi za gazeti la vibonzo la Charlie Hebdo nchini
Ufaransa.
Lakini kauli yake imekosolewa sehemu mbalimbali.
Katibu
wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Saba
Raymond alisema alichozungumzia Obama ni historian a hivyo dunia
inatakiwa ijifunze.
“Kama kimetokea, kimetokea. Tunatakiwa
kujifunza kutokana na kilichotokea. Katika ulimwengu wa sasa ni fursa ya
kujifunza yale yaliyotokea na hayafai na wakati huu yasitokee tena...
wale wanaoyataka, washindwe,” alisema Padri Raymond
Padri
Raymond aliongeza kusema: “Utumwa ulikuwa haufai na Marekani
walijihusisha kwa hili (kuuondoa) na hii ni historia ambayo wanapaswa
kuiacha.”
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho
alisema:” Ni kauli ya kujihami na anaogopa kuwanyooshea kidole moja kwa
moja... Wamarekani wasingependa yatokee kama yaliyowahi kutokea huko
nyuma.
“Hili ni suala nyeti na gumu sana, matuko mengi
yamekuwa yakitoke hivi karibuni ya kuchinja watu kama Nigeria, Misri na
kwingineko... Obama anachukua tahadhari ili akiondoka madarakani
Wamarekani wasianze kumtuhumu kwa kusababisha maafa.”
Mkurugenzi
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba
alisita kidogo kuzungumzia suala hilo moja kwa moja kutokana na kutojua
mazingira ambayo rais huyo wa taifa kubwa duniani aliyotumia kutoa kauli
hiyo.
“Sijajua kwa nini ametoa kauli hiyo na wakati huu
kwani hata hao wanaotekeleza vitendo vya kigaidi ni watu ambao si wa
kawaida... ni kauli ambayo bado sijajua ina maana gani.”
Nchini Marekani, mtangazaji wa kituo cha televisheni cha MSNBC, Joe Scarborough hakuamini kauli hiyo ya Obama.
“Ni
kitu usichoweza kuamini,” alisema mtangazaji Scarborough. “Wakati
mwingine unaweza kusema tu, ‘Hey, unajua? Kuna Waislamu wenye imani kali
ambao ni wabaya, wabaya kweli.’”
Wahafidhina nao walieleza kuchukizwa na kauli ya Obama.
Gavana
wa zamani wa Virginia nchini Marekani, Jim Gilmore alisema kauli ya
Obama ni “ya uchochezi ambayo haijawahi kutokea” maishani mwake.
Na televisheni ya Fox News ilitoa kipande baada ya kipande cha hotuba hiyo na kujadili.
“Mtu
huyu hana maana, mbinafsi na mweye mambo yaliyopita kiasi,” mtangazaji
wa kipindi cha mazungumzo ambaye ni mhafidhina, Mark Levin aliiambia
Fox.
Levin alieleza kuwa kama rais wa zamani wa Marekani, Abraham Lincoln angefuata msimamo wa Obama, angeachia utumwa uendelee.
“Lincoln
angesema, kutokana na hoja ya Obama, Msishuke kwenye farasi wenu. Hili
siyo tishio lililopo,’” aliongeza Levin. “Lincoln angeweza kusema, ‘Kwa
nini natuma duniani maelfu ya watu waende kwenye vifo ili waondoe
utumwa?’Anachosema Obama ni kibaya kuliko vyote.”
Akihojiwa
na ABC News, mwanahistoria wa Chuo Kikuu cha St. Louis, Thomas Madden
alisema: “Sidhani kama rais anaelewa vizuri vita vitakatifu,” alisema.
“Anaonekana
anaelezea kama mfano wa upotoshaji wa Ukristo na kujaribu kulinganisha
na upotoshaji wa Uislamu kutokana na vitendo vya ISIS,” alisema Madden.
“Lengo la awali la vita vitakatifu lilikuwa ni kurejesha kwa Wakristo
ardhi iliyokuwa imetekwa kutokana na ushindi wa Waislamu.”
Vita
vitakatifu, ambavyo vilianza mwaka 1095 kwa wito wa Papa Urban ll wa
kutaka kuirejesha Jerusalem kutoka kwa Waislamu, ilikuwa na matukio
kadhaa yaliyodumu kwa karne mbili.
Ingawa hakuna makadirio yanayoaminika
yaliyosababishwa na vita hivyo, zaidi ya Waislamu 2,700 waliokuwa
wafungwa waliuawa kwa pamoja na Richard the Lionheart nje ya Acre wakati
wa vita ya tatu ya Crusaders na tukio hilo linakumbukwa Mashariki ya
Kati hadi leo.MWANANCHI
No comments:
Post a Comment