WASOMAJI
na wadau wangu nawasalimu na naimani kuwa Mwenyezi Mungu ametujalia
tumeuona mwaka mpya wa 2015 salama salmini. Nawatakia heri na fanaka
katika mwaka huu pia na karibuni tena katika porojo zangu za ukweli.
IDARA ya
Habari –MAELEZO ndiyo idara ya serikali inayoshughulika na kufanya kazi zake
kama chombo cha usimamizi wa vyombo vya habari na waandishi wake.
Idara
hiyo pia ndio msemaji wa masuala mbalimbali ya serikali lakini pia ndiyo idara yenye
jukumu la kusajili au hata kuyafutia usajili magazeti hapa nchini na vyombo
mbali mbali vya hjabari.
Waandishi
wa habari waajiriwa na wale wa kujitegemea wameanza mchakato wa kujaza fomu
kwaajili ya kupatiwa vitambulisho vipya vya kazi (PRESS CARD) kwa mwaka 2015.
Jambo
hili ni zuri kwa waandishi wa habari maana kitambulisho hicho cha serikali
hutolewa kwa waandishi walio na sifa za uandishi tu na sio wale waparamia fani
za watu maarufu kama kanjanja.
Ndio! Uandishi
wa habari ni taaluma kama taaluma nyingine, kwa hiyo kila mwanahabari anatakiwa
kuwa na Press Card ambacho ndicho kitambulisho cha serikali, kama huna basi
wewe sio muandishi au laa hujakomaa kuwa muandishi.
Nakama
umekomaa lakini sifa za kupata 'Leseni ya Uandishi' huna basi tambua
fika fani ya uandishi wa habari haikufai na unatakiwa kwenda kwenye fani
nyingine, na hii uiache maana utaleta usumbufu tu mitaani.
Vigezo
vya kupewa Press Card kwa mwandishi wa habari ni lazima awe na kiwango cha
elimu ya ngazi ya Stashahada na uzoefu katika kazi hiyo.
Bila
mwandishi wa habari kuwa na kitambulisho kinachotambuliwa na Serikali,
mwandishi huyo anakuwa hatambuliki vyema na huenda katika ofisi nyingine
asipate huduma (taarifa) anazohitaji.
Bunge
linataraji kuanza vikao vyake Januari 27 mwaka huu, lakini waandishi wa habari
wasio na Press Card hawata ruhusiwa kuripoti tukio lolote katika Bunge hilo
mjini Dodoma.
Hili ni
agizo lililotangazwa kwa wanahabari tangu mwaka jana na Mkurugenzi wa Idara ya
Habari Maelezo Assa Mwambene.
Ingawa
utaratibu wa press card umekuwepo kwa miaka, hapakuwa na shuruti kwa waandishi
wa maswala muhimu kama bunge kuwa nayo ilimradi tu watambulike na wawe na barua
kutoka vyombo vyao.
Hili
naliunga mkono, maana pasipo tumika vitambulisho hivyo itakuwa ni shida
kufuatia wingi wa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii iliyopo nchini kwa
sasa.
Leo porojo zangu nazipiga katika huu mtindo wa namna utaratibu unaoutumika wa utoaji huo wa vitambulisho ambapo kila
mwaka waandishi wanatakiwa kujaza fomu maalum za maombi na kulipia.
Idara
hii nyeti ya kuisemea serikali inapaswa
kuendana na mfumo wa Sayansi na teknolojia hasa mfumo wa kidijitali wa utunzaji
wa taarifa za kila mwandishi tofauti na ilivyo sasa.
Hivi
kuna haja gani mimi nipo katika tasnia hii huu mwaka wa 14 sasa kila wakati
naleta picha 3, nakala ya vyeti vyangu vya kitaaluma na kujaza fomu tatu za maombi hayo ya kitambulisho?
Mfumo wa
Dijitali kama ungekuwa unatumika MAELEZO, chini ya Mkurugenzi wake Kijana, Assa
Mwambene, ungeweza kabisa kuweka taarifa zetu waandishi katika mtandao na wao
kuzitumia kuhakiki waombaji wa vitambulisho hivyo.
Ni
makaratasi kiasi gani watakuwa wakiyapokea mwaka hadi mwaka kutokana na utoaji
wa vitambulisho hivyo.
Pia
suala lingine ambalo mimi naliona ni kikwazo na hata waandishi wengine wamekuwa
wakilizungumzia ni haja ya kutoa vitambulisho hivyo kila mwaka.
Kwanini
MAELEZO wasitoe vitambulisho vya walau miaka mitatu au hata mitano kwa
waandishi hawa ambao wameridhia wanavigezo na sifa za kufanya kazi hiyo?
Endapo
mwandishi atakiuka utaratibu wa kazi idara hii ya habari Maelezo inauwezo wa
kumpoka kitambusho hicho mwandishi husika kama ambavyo Polisi usalama
barabarani wanaweza kufanya kwa dereva anaekiuka sheria na kusababisha ajali.
Tunajua
kuwa Press Card kutolewa kila mwaka ni moja ya mradi maana waandishi
wanatozwa fedha, ili kuongeza mapato ya idara husika na
serikali kwa ujumla, lakini wanaweza kutoza malipo ya miaka 3 hadi
mitano basi
lakini waandishi wakaondokana na kero ya kujaza fomu kila mwaka na
kusubiri kwa
muda mrefu kupata vitambulisho hivyo.
Aidha fomu basi zingeweza kuanza kutolewa tangu mwezi Novemba ili ifikapo
Desemba vitambulisho vipya viwe
vimeshatoka kulingana na kumalizika kwa muda wa matumizi ya kitambulisho
cha mwaka uliopita.
Lakini
haya mnatengeneza vya mwaka mmoja moja lakini vipi ubora wake nao, kitambulisho
kinapendeza sana siku unakabidhiwa lakini ikishapita wiki moja ile nembo ya
taifa ya bibi na bwana inafutika.
Ni vyema
sasa wanaosimamia ubora wa vitambulisho hivyo wakaangalia malighafi inayoweza
kudumu kwa kipindi cha mwaka mzima na kubaki na alama zote zinazotakiwa kuwepo.
Pia
kutoa vitambulisho hivyo kwa wakati ili kuepusha usumbufu unaoweza kuwakumba
waandishi ambao kwa sasa wanatumia vitambulisho vilivyopita mudawake.
No comments:
Post a Comment