Pages

January 4, 2015

HADI ZA RAIS KIKWETE ZAITESA CHAMA CHA MAPINDUZI.

Rais Kikwete.

Dar es Salaam. 
Ahadi zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa wananchi katika mikutano mbalimbali nchini wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, huenda zikawa mwiba kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, kutokana na nyingi kutokutekelezwa au kuwa katika hatua za mwanzo. 

Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, kwa nyakati tofauti alitoa ahadi kusaidia kuwakwamua wananchi kutoka kwenye dimbwi la umaskini, maradhi na kuboresha upatikanaji wa elimu nchini. Ahadi hizo zilitarajiwa kukamilika kabla hajatoka madarakani.


Ikiwa imebaki takriban miezi 10 ya uongozi wa kipindi cha pili cha awamu ya nne kufikia ukomo, muda unakwenda haraka na utekelezaji wa ahadi hizo unasuasua jambo linalotia shaka iwapo kila ahadi itatekelezwa kwa wakati.


Kushindwa kutekeleza ahadi hizo ambazo zimo katika kitabu cha ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za urais 2010, kilichondaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, kunaiweka Serikali ya CCM katika wakati mgumu hasa pale itakaporudi kwa wananchi kutoa ahadi nyingine kwenye kampeni za uchaguzi mkuu ujao.

Nape 
Alipoulizwa kuhusu ahadi hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Rais Kikwete ametekeleza ahadi zaidi ya inavyoahidi ilani ya CCM.

“Ukitaka kumtendea haki Rais Kikwete katika utekelezaji wa ahadi zake, lazima uangalie kitabu chote cha ahadi harafu upate ushahidi wa viongozi wawakilishi au kuzunguka kwenye maeneo zilizokotolewa ahadi hizo,” alisema na kuongeza;

“Kwa ufupi tu, Rais huyu amefanikiwa kutekeleza ahadi nyingi ambazo ziko kwenye ilani na zile alizotoa papo kwa papo.”

Hata hivyo Nape alimwahidi mwandishi wa gazeti hili kutoa ufafanuzi wa ahadi zilizotekelezwa na Rais kwa kipindi chote alichokaa madarakani wiki ijayo.

Turuka
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florens Turuka alisema ofisi yake kwa sasa iko kwenye uchambuzi na uandaaji wa kitabu kitakachoeleza utekelezaji wake.

Turuka alisema kazi hiyo itakamilika kwa miezi miwili kuanzia sasa.“Yapo mengi sana aliyoyafanya rais, lakini tutaweka wazi wala siyo siri, kazi zote alizofanya zinaonekana ila kwa sasa itakuwa vigumu kubainisha kiwango cha ahadi alizotekeleza,” alisema Turuka.

Rais Kikwete alipokuwa wilayani Bunda, Mkoa wa Mara aliahidi kutokomeza ugonjwa malaria ifikapo mwaka 2015, lakini mpaka sasa ugonjwa huo umebaki kuwa tishio na ukipoteza maisha ya Watanzania wengi kila mwaka.

Rais Mstaafu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia alisema jana kuwa kwa mujibu wa malengo ya Milenia, Tanzania imepunguza vifo vitokanavyo na malaria licha ya kuendelea kukabiliwa na changamoto kadhaa.

Alisema kwa hali ilivyo hivi sasa nchini, ambapo dawa hazipatikani kwa kiwango kinachotakiwa ni vigumu kufanikiwa kutokomeza ugonjwa huo kwa asilimia 100 mwaka huu.

“Kama tukipata Rais mzuri ambaye ataweka nguvu kwenye sekta ya afya, malaria inaweza kuondoka kwa asilimia 100 baada ya miaka 15,” alisema Dk Saidia.

Akiwa wilayani Nzega mkoani Tabora, Rais Kikwete aliahidi kuwa Serikali yake ingejenga reli mpya kutoka Dar es Salaam mpaka mikoa ya Kanda ya Ziwa, lakini mpaka sasa ahadi hiyo haijakamilika ingawa tayari ameshakutana na Kampuni ya China Railway Group Limited inayotarajiwa kutekeleza mradi huo.

Pia, akiwa Tanga Mjini, Rais Kikwete aliahidi kuhakikisha kuwa mkoa huo unakuwa jiji la viwanda. Ahadi hiyo mpaka sasa haijakamilika ingawa tayari maeneo kwa ajili ya wawekezaji yamekwishatengwa.

Akiwa wilayani Igunga mkoani Tabora, Rais Kikwete aliahidi kuwa wananchi wa Tabora wangeanza kutumia maji kutoka Ziwa Victoria. Ahadi hiyo mpaka sasa haijakamilika japokuwa akijibu swali bungeni, Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge alisema mwaka 2013/14 Serikali ilitenga Sh450 milioni kwa ajili ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni.

Ahadi nyingine za Rais Kikwete ni pamoja na kumaliza migogoro ya ardhi nchini, wakulima kuacha kutumia jembe la mkono na kununua meli kubwa kuliko MV Bukoba iliyozama Mei 21, 1996.

Pia, kiongozi huyo wa nchi aliahidi kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), kwa miaka mitatu, kuanzisha benki ndogondogo kwa ajili ya wajasiriamali na kuimarisha usalama Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa kupeleka kikosi maalumu chenye vifaa vya kupambana na wahalifu.

Katika orodha ya ahadi hizo, pia Rais Kikwete aliahidi kumaliza tatizo la walimu nchini. Hata hivyo, bado walimu wameendelea kuinyooshea kidole Serikali wakilalamikia kushindwa kuwapandisha madaraja, malimbikizo ya madeni na mishahara midogo.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch alisema licha ya kuwa Rais Kikwete amefanya mambo mengi tangu alipoingia madarakani, ataiacha nchi ikiwa njiapanda kielimu.

Alisema Rais Kikwete aliahidi kutatua tatizo la kupandishwa madaraja walimu, lakini mpaka mwisho wa mwaka huu kutakuwa na walimu 120,000 wanaostahili kupandishwa madaraja.

Akifafanua alisema: “Mwaka jana walimu 40,000 hawakupandishwa madaraja, mwaka huu wengine 40,000 walitakiwa kupandishwa na Julai, 2015 wengine tena watahitaji kupandishwa madaraja.”

Oluoch alieleza kuwa Rais Kikwete aliwaahidi walimu kuwa angewaanzishia tume yao, lakini mpaka sasa hakuna hata muswada uliotayarishwa.


Pia, alisema Oktoba 5, 2010 huko Songea mkoani Ruvuma, Rais Kikwete aliwaahidi walimu kuwa angeunda Bodi ya Taaluma ya Walimu, lakini jambo hilo bado halijatekelezwa.


“Hili tunaliona kama ni deni, Rais asiondoke Ikulu bila kutekeleza ahadi hizo,” alisema.


Aliongeza kuwa: “Serikali ya awamu ya nne inaiacha nchi njiapanda kielimu, elimu haikupaswa kusimamiwa na Tamisemi inatakiwa isimamiwe na Wizara ya elimu.”


Vilevile, Rais Kikwete aliahidi kuwajengea nyumba waathirika wa mafuriko ya Kilosa, kununua meli mpya kubwa Ziwa Nyasa na kujenga Bandari Kasanga.


Ahadi zingine ni kufufua Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira, kuzuia hatari ya Kisiwa cha Pangani kuzama, kumaliza tatizo la maji katika Wilaya ya Same, kusambaza walimu 16,000 katika shule za sekondari zenye upungufu mkubwa wa walimu na kununua vyandarua viwili kwa kila kaya.


Rais Kikwete aliahidi kumaliza tatizo la ukosefu wa umeme mkoani Arusha, kukopesha wavuvi zana za kilimo, kuwapatia maji wakazi wa Wilaya ya Longido, kujenga barabara ya lami kupitia pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Seregenti na kusambaza maji nchi nzima.


Kuhakikisha Jimbo la Isimani linapata maji ya uhakika, kuweka lami barabara inayokwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na Serikali kujenga upya Bandari ya Mbambabay.


Aliyekuwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema Rais Kikwete anaweza kutekeleza ahadi zake kwa asilimia zaidi ya 70 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.


“Lazima tuwe wakweli huyu Rais amefanya mengi sana, yaani ukiangalia kuna ahadi nyingi kafanya japokuwa hawezi kumaliza zote kwa muda uliobakia,” alisema Ruhuza.


Hata hivyo, aliongeza kuwa baadhi ya ahadi ambazo hazijatekelezwa mpaka sasa ni pamoja na ujenzi wa barabara za Kigoma-Nyakanazi(km330), Lulenge-Mulungarama(km100),Karagwe-Ngara(km150).


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Watendaji wakuu wa Makampuni nchini(CEOs Roundtable-Tanzania),Ali Mufuruki alisema ahadi alizotekeleza n8i nyingi japokuwa hataweza kumalizia zilizobakia.


“Lakini labda nikupatie mfano, unaweza kuahidi watoto wako zawadi na ukawanunulia wote, inatokea wengine wanakosa kwa hivyo sioni kama ni tatizo hilo,” alisema Mufuruki.MWANANCHI

No comments:

Post a Comment