Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akimpongeza Mhe. Mansour Yussuf
Himid baada ya kuamua kujiunga na chama hicho na kumkabidhi rasmi kadi
ya CUF katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
Mwanachama
mpya wa CUF Mansour Yussuf Himid akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa
CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, baada ya kujiunga na chama hicho
katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
Mwanachama
mpya wa CUF Mansour Yussuf Himid akizungumza na wanachama wenzake ,
baada ya kujiunga na chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya
Kusini Unguja.
Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia mkutano wa hadhara wa
chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
Wanachama
wa CUF wakionyesha kuunga mkono uamuzi wa Mansour Yussuf Himid kujiunga
rasmi na chama hicho kwenye viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
(Picha na Salmin Said, OMKR).
Na Hassan Hamad (OMKR).
Aliyekuwa
Mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki Mhe. Mansour Yussuf Himid,
amejiunga rasmi na chama cha wananchi CUF.
Mhe. Mansour ambaye amewahi kuitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kwa kushika nyadhifa mbali mbali ikiwemo ya Waziri wa Kilimo, amechukua
uamuzi huo kwenye mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika viwanja vya
Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
Baada
ya kukabidhiwa kadi ya CUF na Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif
Sharif Hamad, Mhe. Mansour amesema ameamua kujiunga na CUF baada ya
kubaini na kuridhika kuwa chama hicho kimebeba matumaini mapya ya
wazanzibari.
Mhe. Mansour ambaye tayari alishateuliwa na chama hicho kuwa mshauri wa
mikakati wa Katibu Mkuu wa CUF, amechukua kadi hiyo akiwa miongoni mwa
wanachama wapya 108 waliojiunga na CUF kwenye mkutano huo.
Mapema
akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif
Hamad, amempongeza Mhe. Mansour kwa kuamua kujiunga na chama hicho
hadharani, na kukiita kitendo hicho kuwa ni cha kijasiri.
Akizungumzia mafanikio ya chama hicho, Maalim Seif amesema kimepata
mafanikio makubwa katika mwaka unaomalizika wa 2014, na kutangaza
maazimia mapya ya chama hicho kwa mwaka 2015.
Ametaja
mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kuendelea kukubalika kwa
chama hicho katika pembe zote za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kuhusu
maazimio ya Chama hicho kwa mwaka 2015, Maalim Seif amesema kimejipanga
kuhakikisha kuwa kinashinda kwa asilimia kubwa katika uchaguzi mkuu
ujao na kuweza kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa.
Hata
hivyo amewataka wanachama wasibetweke kutokana na mafanikio
yaliyopatikana, bali waongeze nguvu kuhakikisha kuwa malengo ya chama
hicho katika uchaguzi mkuu ujao yanafikiwa.
Ameongeza kuwa CUF pia kimejipanga kuimarisha uchumi na kujenga Zanzibar mpya itakayokuwa ya matumaini kwa Wazanzibari wote.
Katika
hatua nyengine, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar amesema katika uchaguzi mkuu ujao hatowazuia vijana kutetea
haki yao iwapo watadhulumiwa.
“Katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 nilifanya kazi kubwa ya kuwazuia vijana
wasifanye vurugu pale hoteli ya Bwawani. Mwanzo niliwatuma wasaidizi
wangu waende kuwaondosha lakini hakuna aliyesikia hadi nilipokwenda
mwenyewe, tena waliondoka kwa shingo upande kabisa. Kwa hivyo uchaguzi
mkuu ujao sina namna yoyote ya kuwazuia vijana kutetea haki yao”,
alifafanua Maalim Seif.
Kabla
ya mkutano huo Maalim Seif alifanya ziara ya kukagua uhai wa chama hicho
katika vijiji vya Michamvi, Bwejuu, Jambiani na Paje ambako aliweka
mawe ya msingi kwenye matawi ya chama hicho, pamoja na kupandisha
bendera kwenye barza ya DAY OUT ya Paje.
No comments:
Post a Comment