Kwa mara ya kwanza, jeshi la anga nchini Cameroon limeshambulia maeneo
yanayotumiwa na kundi la kigaidi la Boko Haram kaskazini mwa nchi hiyo,
baada ya wanamgambo hao kuiteka kambi moja ya kijeshi.
Ni mwenyewe Rais Paul Biya ya Cameroon ndiye aliyeamuru kufanyika kwa
mashambulizi hayo ya jana Jumapili, ambayo yaliwalazimisha wanamgambo
wa Boko Haram kuikimbia kambi ya Assighasia. Mapema jana, wanamgambo wa
Boko Haram waliivamia kambi hiyo ya Assighasia na kuwalazimisha
wanajeshi waliokuwa wakijaribu kuilinda kurejea nyuma kutokana na
kuelemewa na mashambulizi.Kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Issa Tchiroma Bakary, jeshi lilishambulia mara mbili na kusababisha vifo vya wanamgambo 41, kabla ya waliosalia kuamua kukimbia.
Waziri Bakary ameliambia shirika la habari la AFP kwamba awamu hii ya mashambulizi ya anga itafuatiwa na operesheni ya ardhini muda wowote kutokea sasa. Tayari maelfu ya wanajeshi wako njiani kuelekea huko.
Hii ni mara ya kwanza kwa jeshi la Cameroon kutumia ndege zake kuwashambulia moja kwa moja wapiganaji wa Boko Haram, ambao huvuuka mpaka kutokea nchi jirani ya Nigeria.
Mbinu mpya ya Boko Haram
Uvamizi wa karibuni kabisa wa Boko Haram ulishuhudia vijiji na miji mitano ikiangukia mikononi mwa kundi hilo, katika kile ambacho Waziri Bakary alisema ni kubadilika mbinu za kundi hilo, ambalo awali lilitegemea zaidi kushambulia eneo moja na kukimbia.
"Boko Haram ilijigawanya kwa makundi na kushambulia miji ya Makari, Amchide, Limani na Achigachia. Wamebadili mbinu, na hivyo kutaka kuvifanya vikosi vya Cameroon vijigawanye kwenye kukabiliana na matukio tafauti mahala tafauti kwa wakati mmoja, na hivyo kuvifanya viwe rahisi kushambuliwa na pia iwe vigumu kutabiri mashambulizi ya Boko Haram", alisema Waziri Bakary.
Operesheni ya jeshi la Cameroon ya hapo jana ilifanikiwa kuwauwa wanamgambo 34, wakati jeshi lilipoizingira kambi ya Chogori iliyokuwa ikitumiwa na wanamgambo hao, na wengine saba pamoja na mwanajeshi mmoja waliuawa kwenye mji wa Waza.
Msemaji wa jeshi, Luteni Kanali Didier Badjeck, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba hapo kabla, wanamgambo hao walifanikiwa kuiteka na kuikalia kwa muda kambi ya Chogori, ingawa baada ya makabiliano makali na wanajeshi waliotumwa huko, walikimbia jioni ya jana.
Kampeni ya Boko Haram kuunda utawala wa Kiislamu imesambaa kutokea ngome yao kaskazini mashariki mwa Nigeria hadi Cameroon, na hivyo kuongeza wasiwasi uliopo kwenye eneo hilo la magharibi mwa Afrika, ambalo tayari linakabiliwa na wapiganaji wa makundi ya Kiislamu kwenye kanda ya Sahel.
Ndani ya mwaka huu pekee, Boko Haram imeshawauwa wanajeshi 40 wa Cameroon na kutoa mafunzo kwa maelfu ya wanamgambo katika miji ya mpakani mwa Nigeria na Cameroon.
No comments:
Post a Comment