Pages

December 1, 2014

BANDARI YA KASANGA KUANZA KUBORESHWA

Na Saidi Mkabakuli, Sumbawanga

Serikali imeazimia kuanza kuiboresha bandari ya kimkakati ya Kasanga inayohudumia nchi za Burundi, Rwanda na Kongo iliyopo katika Ziwa Tanganyika, mkoani Rukwa.

Ahadi hiyo imetolewa na Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya miundombinu katika Bandari ya Kasanga.

Bibi Mwanri alisema kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania imepanga kuboresha bandari zote ili kuwa malango kuu la biashara kwa soko la ndani na kwa nchi jirani ili kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena kwa ufanisi.

“Tumedhamiria kuendelea kuboresha miundombinu ya bandari hususan miradi iliyoibuliwa katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa ikiwemo Bandari ya Kasanga ili kuweza kukidhi mahitaji ya utoaji wa huduma katika eneo hili,” alisema.

Bibi Mwanri aliongeza kuwa serikali pia imejipanga kuendelea kuboresha miundombinu na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kuhudumia shehena katika bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Kasanga na Kigoma na kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa bandari mpya za Mwambani (Tanga), Mbegani (Bagamoyo) na Bandari Kavu ya Kisarawe.

Akizungumza na ugeni huo, Msimamizi Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa alisema kuwa Bandari hiyo ina fursa nyingi katika kuhudumia shehena na abiria wanaopitia bandarini hapo.

“Bandari yetu ina fursa kubwa za kibiashara kwani tuna wateja wengi kutoka ndani na nje ya nchi wanaotumia bandari yetu kupitishia bidhaa zao, pamoja na abiria wanaosafiri kwenda nje na ndani ya Tanzania,” alisema.

Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha Serikali imedhamiria kuboresha mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kuwekeza katika kujenga miuondombinu na kuboresha usafirishaji wa mizigo katika bandari zote nchini.

Pia, Mpango huo unaweka bayana kuendeleza na ukarabati na ununuzi wa vyombo vya usafiri na usafirishaji katika maziwa.
Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Watatu kushoto) akimsikiliza kwa makini Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kulia) mara walipowasili katika bandari hiyo kujionea shughuli mbalimbali za maendeleo bandari hapo.
Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kushoto) akiwaongoza wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kujionea moja ya meli za kigeni zinazotia nanga katika bandari hiyo. Meli hiyo ni MV Rwegura kutoka nchini Burundi.
Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kushoto) akiongea na wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kuhusu namna ya kuhudumia meli kutoka nje ya nchi.

Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kulia) akitoa ufafanuzi juu ya namna bandari yake inavyohudumia meli kutoka nchi jirani. Wanaomsikiliza ni Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ikiongozwa na Bibi Florence Mwanri (Kushoto aliyevaa fulana nyeusi).
Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kulia) akiwaonesha maghala ya kuhifadhia mizigo katika Bandari ya Kasanga. Maghala hayo yalifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilali tarehe 22 Februari 2012.
Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ikiwa katika picha ya pamoja katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) zilizopo kwenye Bandari ya Kasanga.
Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ikiwa katika picha ya pamoja katika jiwe la msingi la uzinduzi wa maghala ya kuhifadhia mizigo katika Bandari ya Kasanga. Maghala hayo yalifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilali tarehe 22 Februari 2012.
Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kushoto) akimfafanualia jambo Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kulia) wakati akimkabidhi taarifa ya maendeleo ya bandari hiyo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...