Muhongo ndiye dalali mkuu wa Escrow akaunti
Pinda atakiwa kuachia ngazi kwa kuzembea
Werema kinara wa kufanikisha uchotwaji fedha
Wote watakiwa kung�oka, pia yumo Maswi, Maselle.
Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo
Gharika
la ‘Tegeta Escrow’ limeikumba serikali baada ya Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda na viongozi waandamizi kadhaa wa serikali kubainika kuhusika
katika sakata la uporwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 ya fedha katika
akunti hiyo iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Aidha, imependekezwa kwamba viongozi wa umma waliopata mgawo wa fedha hizo wafilisiwe na kuvuliwa nyadhifa zote mara moja.
Akiwasilisha mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), bungeni jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo
Filikunjombe, alisema uchunguzi umethibitisha kwamba Pinda alikuwa
anaujua mchezo mzima kwa kuwa alikuwa akijulishwa kila hatua iliyokuwa
ikiendelea, lakini hakuchukua hatua.
UHUSIKA WA PINDA
Filikunjombe alisema kamati hiyo ililazimika kupitia kwa umakini Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 iliyoainisha kazi na
mamlaka ya Waziri Mkuu na kubaini kuwa, kwa mujibu wa Ibara ya 52 (1):
Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji
wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya
Muungano.
Alisema Ibara ya 52 (2), inasema; Waziri Mkuu atakuwa
Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni.Alisema baada ya kusoma Ibara
hizo, Kamati ilijiuliza maswali kadhaa ikiwamo (a) Je, Waziri Mkuu
alikuwa anajua sakata la utoaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta
Escrow? (b) Je, Waziri Mkuu alitimiza wajibu wake kwa mujibu wa Ibara ya
52(1)?
(c) Je, Waziri Mkuu wakati akitoa matamshi yake Bungeni alikuwa akitimiza wajibu wake kwa mujibu wa Ibara ya 52 (2)?
(d) Je, nini maana, uzito na ukweli wa matamshi ya mara kwa mara ya Waziri Mkuu ndani na nje ya Bunge kuhusiana na suala hili?
(e) Je, Waziri Mkuu alitoa maamuzi au maelekezo yoyote ya kuzuia jambo hilo lisifanyike?
Mheshimiwa Spika, baada ya kupitia vielelezo vilivyomo kwenye ripoti ya
CAG, kamati imejiridhisha pasipo shaka kuwa, Waziri Mkuu, alikuwa ana
taarifa zote kuhusiana na mchakato mzima wa kuchotwa fedha kutoka katika
akaunti ya Escrow.
Alisema ushahidi uliopelekwa na CAG kwenye
kamati unaonyesha kuwa Waziri Mkuu alikuwa akipata taarifa za jambo hilo
lakini hakuchukua hatua zozote kuzuia muamala huo usifanyike.
Alisema kamati imethibitisha kwamba Waziri Mkuu alikuwa analijua jambo
hilo vizuri na kwamba aliridhia muamala huo ufanyike na ndiyo maana
katika maelezo yake ya bungeni mara kadhaa alithibitisha kuwa fedha za
Escrow hazikuwa fedha za umma.
“Ni wazi kwamba maneno ya Waziri
Mkuu hapa Bungeni yaliuaminisha umma kuwa fedha zile siyo fedha za umma
kiasi kwamba gazeti la Serikali la Daily News la tarehe 1 mwezi Mei,
2014, likachapisha habari yenye kichwa kikubwa cha habari ‘IPTL clean
Deal – Pinda’. Na ofisi ya Waziri Mkuu haikukanusha.”
“Ni jambo
la kushangaza kuona kwamba, jambo kubwa na zito kama hili lingeweza
kufanyika bila ya mamlaka za juu, hususan Waziri Mkuu kufahamu.”
Filikunjombe alisema kutokana na uzito na unyeti wa jambo hilo kwa
vyovyote vile, Waziri Mkuu anapaswa kuwajibika kwa kauli zake na kwa
kutokutekeleza wajibu wake wa kikatiba ipasavyo, ili kurejesha imani ya
wananchi kwa serikali yao na viongozi wao wa kisiasa.
WAZIRI MUHONGO
Filikunjombe alisema Kamati imethibitisha kuwa Waziri wa Nishati na
Madini, Prof. Sospeter Muhongo, ndiye alikuwa dalali mkuu
aliyewakutanisha Harbinder Singh Sethi na James Rugemalira, tena katika
ofisi ya umma.
“Waziri wa Nishati na Madini alifanya udalali
huo akijua dhahiri kuwa Sethi hana uhalali wa kisheria kufanya biashara
kwa jina la IPTL,” alisema Filikunjombe.
Alisema iwapo Waziri
wa Nishati na Madini angetimiza wajibu wake ipasavyo, Fedha za Tegeta
Escrow zisingelipwa kwa watu wasiohusika, na nchi ingeweza kuokoa
mabilioni yaliyopotea kama kodi za VAT, Capital Gain Tax na Ushuru wa
Stempu ambazo ni takribani Sh. bilioni 30.
“Mheshimiwa Spika,
kamati inapendekeza kuwa kamlaka yake ya uteuzi itengue uteuzi wa Waziri
wa Nishati na Madini kutokana sababu hizo zilizoelezwa.”
MASWI
Katika mapendekezo hayo, kamati imetaka Maswi avuliwe wadhiwa wake na
Takukuru imfikishe mahakamani haraka kwa kuikosesha serikali mapato,
matumizi mabaya ya ofisi na kusaidia utakatishaji wa fedha haramu.
Alisema kamati imethibitisha kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini aliingia makubaliano ya kutoa fedha katika Akaunti ya Tegeta
Escrow bila kujiridhisha kikamilifu kuwa maamuzi ya hukumu ya ICSID 2
yalikuwa bado kutolewa na hivyo kusababisha fedha kutolewa bila
kukokotoa upya gharama za ‘capacity charges’, jambo ambalo limesababisha
kupoteza fedha za umma.
“Vile vile, kamati imebaini kuwa,
Katibu Mkuu hakufanya uchunguzi wa kina (due diligence) kujiridhisha
uhalali wa kampuni ya Mechmar kuuzwa kwa Piperlink na baadaye kuuzwa kwa
PAP, na hivyo kusababisha fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kulipwa kwa
asiyestahili na kinyume cha mkataba wa akaunti ya Escrow.”
Filikunjombe aliongeza kuwa: “Kwa maana hiyo, Katibu Mkuu, Wizara ya
Nishati na Madini, pengine kwa uzembe wake ama kwa kukusudia kwa sababu
anazozijua yeye mwenyewe zaidi, amesaidia uchotwaji na hatimaye
utakatishaji wa fedha haramu.”
Alisema kamati pia imethibitisha
uzembe wa hali ya juu uliofanywa na Maswi kushindwa kujiridhisha kama
masharti ya Sheria ya Kodi ya Mapato Sura ya 333, Kifungu cha 90(2)
ambacho kinaitaka mamlaka ya ‘approval’’ ya uhamishaji wa makampuni
kutotambua kampuni mpaka kwanza kodi za uhamishaji ziwe zimelipwa na
hati za malipo ya kodi zimetolewa na mamlaka ya kodi.
BODI YA TANESCO
Alisema kamati imejiridhisha kuwa Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme
Nchini (Tanesco) bila sababu zozote za msingi ilikataa mapendekezo ya
menejimenti ya shirika ya kutoruhusu uchotwaji wa fedha kutoka BoT
akaunti ya Tegeta Escrow na hivyo kusababisha kulikosesha shirika fedha
zake inazohitaji sana kutokana na hali mbaya ya Shirika.
“Kamati inaitaka serikali kuvunja mara moja Bodi ya Tanesco na Takukuru
iwafungulie mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi wajumbe wote
waliohusika kupitisha maamuzi hayo ya kifisadi, ili iwe fundisho kwa
wajumbe wengine wa bodi za mashirika ya umma kwamba watahukumiwa kwa
maamuzi mabovu wanayoyafanya.
STEPHEN MASELE
Kuhusu
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Filikunjombe alisema kamati
imethibitisha kuwa alisema uongo bungeni kwa kutamka kauli ambazo
zilizokuwa na lengo la kupotosha umma kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow,
ikiwamo kauli ambazo zingeweza kusababisha nchi kuingia kwenye mgogoro
wa kidiplomasia na nchi ya Uingereza.
“Kamati inapendekeza kuwa
Naibu Waziri wa Nishati na Madini achukuliwe hatua kali za kinidhamu
ikiwamo kutenguliwa uteuzi wake. Kamati pia inapendekeza kuwa Naibu
Waziri huyu afikishwe mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili ili aadhibiwe
kama Mbunge kwa kusema uwongo bungeni ili liwe fundisho kwa wabunge
wengine kuhusiana na kauli wanazotoa ndani ya Bunge lako tukufu.”
AG JAJI WEREMA
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, ametajwa kuhusika
katika kashfa hiyo kwa kutoa ushauri ulioipotosha BoT kuhusiana na
hukumu ya Jaji Utamwa.
Imebainika pia kuwa Jaji Werema, alitumia
madaraka yake vibaya na kuagiza kodi ya serikali yenye thamani ya Sh. 21
bilioni isilipwe na hivyo kuikosesha serikali mapato adhimu.
“Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kujua na kwa makusudi alilipotosha
Bunge na Taifa kwamba mgogoro uliopelekea kufunguliwa kwa Akaunti ya
Escrow ulikuwa ni mgogoro wa Wanahisa wa IPTL badala ya mgogoro kati ya
Tanesco na IPTL. Kamati inapendekeza kuwa uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali utenguliwe mara moja na kisha afikishwe mahakamani kwa matumizi
mabaya ya Ofisi yaliyopelekea Serikali kupoteza mabilioni ya fedha.
HUKUMU YA JAJI UTUMWA
Kamati hiyo imesema kuwa hukumu ya Jaji Utamwa ya kukabidhi masuala
yote ya IPTL kwa Kampuni ya PAP, ilitafsiriwa vibaya na Harbinder Singh
Sethi mwenyewe na baadaye ikatafsiriwa vibaya pia na viongozi wa Wizara
ya Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hata baadhi ya
viongozi wakuu wa Serikali akiwamo Waziri Mkuu.
Filikunjombe
alisema uchunguzi ulibaini kuwa Kampuni ya PAP haikuwa na uhalali wowote
wa umiliki wa IPTL wakati inalipwa fedha za kutoka Akaunti ya Tegeta
Escrow.
HARBINDER
Kamati imependekeza kuwa Takukuru
na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) wamkamate mfanyabiashara
Harbinder Singh Sethi na kumfikisha mahakamani kwa makosa ya Anti money
laundering, ukwepaji kodi na wizi.
Kamati pia inaelekeza
Serikali kutumia sheria za Nchi, ikiwamo sheria ya ‘Proceeds of Crime
Act’ kuhakikisha kuwa Harbinder Singh Sethi anarejesha fedha zote
alizochota kutoka Benki Kuu ya Tanzania.”
MENGINEYO
Filikunjombe alisema Kamati imethibitisha bila chembe ya mashaka kwamba
mchakato mzima wa kutoa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow uligubikwa
na mchezo mchafu na haramu wenye harufu ya kifisadi ulioambatana na
udanganyifu wa hali ya juu ambao kwa kufuata sheria tu ungeweza
kugundulika na kuzuiwa.
Alisema kutokana na mchezo huo mchafu,
mfumo mzima wa Serikali ni kama ulipata ganzi au uliganzishwa ili
kuwezesha uporwaji huo wa Sh. bilioni 306 na kutakatishwa kupitia Benki
mbili hapa Nchini na baadhi ya mabenki ughaibuni.
Kamati hiyo
pia imependekeza kuwa kutokana na kukua na kukomaa kwa vitendo haramu
vya wizi wa fedha ama mali za umma na kukua ama kukomaa kwa vitendo vya
rushwa kubwa na uhujumu uchumi, inapendekezwa kwamba Bunge lako Tukufu
liridhie kuitaka Serikali kuanzisha kitengo maalumu cha kushughulikia
rushwa kubwa (grand corruption) kitakachokuwa na nguvu ya kuendesha
mashtaka kwa uhuru kamili, na kwamba Bunge lako Tukufu liridhie
kuanzishwa kwa Mahakama Maalum ya kushughulikia Rushwa kubwa
itakayoshughulikia kesi za rushwa zitakazokuwa zikipelekwa kwake na
kitengo maalum cha kushughulikia rushwa kubwa.
KUNA KITU KINAKUJA HAPA MAONI YA WABUNGE
Wabunge wametoa maoni tofauti kuhusu taarifa maaumu ya PAC kufuatia
matokeo ya ukaguzi wa CAG katika akaunti ya Tegeta Escrow, baadhi
wakiiunga mkono na wengine wakisema inahitaji ufafanuzi zaidi.
Walitoa maoni hayo baada taarifa hiyo kuwasilishwa na Mwenyekiti wa PAC,
Zitto Kabwe na Makamu wake, Deo Filikunjiombe, bungeni.
DK. LIMBU
Mbunge wa Magu (CCM), Dk. Festus Limbu, alisema pamoja na kazi ya PAC
kutimiza hadidu rejea walizopewa na Spika wa Bunge, kuna mambo
yanayohitaji kutolewa ufafanuzi, ikiwamo kuelezwa waliopokea fedha hizo
kutoka kwa waliochota kama nao pia waliohojiwa na kamati au la.
LEMBELI
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli, aliunga mkono taarifa ya PAC na
kusema wote waliotajwa kila mmoja abebe msalaba wake kwa kuwa hakuna
kitu anachokichukia duniani kama wizi.
BULAYA
Mbunge
wa Viti Maalumu (CCM), Esther Bulaya, alisema jambo hilo ni zito sana
na kwamba, wabunge bila kujali itikadi zao, walipiganie suala hilo na
hatakubali kuona mwizi akiendelea kuwamo ndani ya Bunge bila kuchukukiwa
hatua.
MASELE
Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Stephen Masele, alisema haoni uhusiano wa mgogoro kati yake na balozi
kuhusishwa na suala la Tegeta Escrow, hivyo ameshangazwa kuona anatajwa
katika taarifa hiyo, ambayo haikuwamo kwenye hadidu za rejea.
NGELEJA
Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, alisema ripoti ipo bungeni
inasubiri kujadiliwa na taarifa itatolewa na makubaliano yatakubaliwa.
MBOWE
Mbunge wa Hai (Chadema), ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema taarifa ya PAC ni nzuri, lakini
akasema ilipaswa kwenda mbali zaidi kwani kuna shinikizo kibwa lilikuwa
likitoka kwa baadhi ya watendaji wa Ikulu katika uchotwaji wa fedha
hizo.
No comments:
Post a Comment