Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ameeleza
tofauti yake na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akisema
imesababishwa na watu aliowaita wapambe.
Zitto (37), ambaye alikuwa naibu katibu mkuu wa
Chadema, alisema kuwa hata kuvuliwa nyadhifa zake ndani ya chama
kulisababishwa na wapambe hao, lakini akasisitiza kuwa hana kinyongo
tena kwa kuwa alishamwomba Mungu na sasa amesamehe kabisa.
Tofauti za wawili hao hazijawahi kutolewa
hadharani licha ya mitandao mbalimbali kuzungumzia kuharibika kwa
uhusiano wao ikinukuu habari kutoka vikao vya ndani vya Chadema.
Hata hivyo, mapema mwaka huu, Zitto alirushiwa
tuhuma nzito na Chadema kutokana na uhusiano wake na baadhi ya makada wa
CCM, lakini mbunge huyo aliyahusisha maneno hayo na mwenyekiti wake na
aliandika maneno makali dhidi ya Mbowe kwenye ukurasa wake wa facebook.
Lakini katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika
wiki iliyopita nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam, Zitto
alionekana kujutia kuharibika huko kwa uhusiano wao na kusema “wapambe
ndiyo wanatugombanisha”.
“Sina shida yoyote na Mbowe, naamini ipo siku
tutagundua wapambe walituathiri na ndiyo waliotufikisha hapa,”
alisisitiza Zitto bila kutaja ni kina nani hasa.
Zitto alisema yeye na Mbowe wametoka mbali tangu
akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hafurahii uhusiano wao ukiishia
katika hali hiyo.
“Naumia sana, lakini naamini ipo siku ama nikiwa
hai au nimekufa watu wataujua ukweli,” alisema mwanasiasa huyo kijana
aliyepata umaarufu kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja.
Alisema, akiwa mwenyekiti wa Serikali ya wanafunzi
wa Chuo Kikuu (Daruso) yeye na mwenyekiti wake ndiyo waliokijenga chama
wakati huo Mbowe akiwa mbunge wa Hai.
Alisema wakati huo Mbowe alikuwa akienda chumbani
kwake kusuka mikakati ya kuiinua Chadema na kwamba walikuwa wakila chips
pamoja na wakati mwingine kwenye klabu ya usiku ya Bilicanas
inayomilikiwa na Mbowe.
“Wakati mwingine naangalia, naumia sana. Wakati
tunafanya hayo yote wengine walikuwa CCM, wengine walikuwa
wafanyabiashara, lakini sasa ndiyo wana sauti katika chama,” alisema
Zitto.
Zitto alisema kuwa wakati huo walikuwa na kampeni
yao waliyoiita ‘Real Madrid’ ambayo ilikuwa na lengo la kuingiza kila
mwanasiasa bora katika chama chao.
Real Madrid ni klabu ya soka ya Hispania yenye mafanikio makubwa duniani na sera yake ni kusajili wachezaji nyota duniani kwa gharama zozote.
“Na kweli tulifanikiwa na kuongeza wabunge kutoka watano hadi 48 wa sasa,” alisema.
“I real miss that (nakumbuka sana). Naumia sana,
mimi leo sina maelewano na watu ambao tulikuwa nao katika mapambano.
Lakini nasononeshwa zaidi na kitu kinachoendelea ndani ya Chadema.
“Nini kimetokea Chadema? Kwa nini tumejikuta
tumeondoka katika mstari? Tupo wabunge 48 bungeni sasa, lakini
hatusogezi mbele nchi, tumerudi nyuma wakati huo tulikuwa watano lakini
tulikuwa tunaenda vizuri sana.”
Akizungumzia jinsi wapambe walivyoharibu uhusiano
wao, Zitto alisema kuna siku Mbowe alimtuhumu kuwa ameanzisha chama cha
umma, pia akasema ana majina mawili tofauti katika mtandao wa Jamii
forums ambayo anayatumia kuwasema viongozi wa Chadema.
“Kukatokea vurugu, baadaye nikasema naondoka. Ile
nataka kutoka wabunge wakanizuia mlangoni nisipite, waliponizuia
nilikuwa na hasira sana, nikawaambia lazima nitoke. Waliponizuia hasira
zikanipanda nikaanguka chini nikalia sana, yaani sana” alisema
akionekana mwenye hisia huku machozi yakimlengalenga.
Kwa mujibu wa Zitto, jioni ya siku hiyo walijikuta
wamekaa meza moja na Mbowe na baada ya kuzungumza waligundua kuwa
walikuwa wamelishwa maneno.
“Tulizungumza na wote tulilia sana. Wakati kama
huu nikikumbuka nasikia uchungu kwa sababu ni wapambe wametufikisha
hapa,” alisema.
Hata hivyo, Zitto alisema kuwa migogoro ni sehemu
ya maisha na kwamba yeye anachukulia kama changamoto kwa kuwa hakuna
njia inayonyooka moja kwa moja na hiyo ni sehemu ya kuendelea kumkomaza.
“Mmoja wa viongozi ambao ni role model wangu ni
aliyekuwa Waziri Mkuu wa Malaysia, Mahathir Mohamad ambaye kila mwezi
Oktoba huwa nakwenda Malaysia kuonana naye.
Mwaka jana wakati vurugu hizi zimeanza kushika
kasi, watu wakaniambia unaweza vipi kukabili mambo kama haya, ila
Mahathir ambaye alifukuzwa kwenye chama chake akiwa mbunge na baadaye
akaja kuwa Waziri Mkuu, aliniambia hizi ni changamoto ambazo lazima
upite,” alisisitiza Zitto.
Aliongeza kuwa hata Makamu wa Rais wa Kenya, Raila
Odinga, alionana naye mwanzoni mwa mwaka na akamshauri asikate tamaa na
kumweleza kuwa yeye hajafikia hata robo ya changamoto ambazo amepitia.
No comments:
Post a Comment