Mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Brazil Geilson Santos “Jaja” jana amewaonyesha wapenzi wa soka nchini nini kazi yake uwanjani baada ya kuisadia Young Africans kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 huku yeye akikwamisha mabao mawili safi mchezo uliofanyika katika dimba la Uwanja wa Taifa jijni Dar es salaam.
Young Africans ambayo ilikua ikicheza mchezo wa Ngao ya Jamii mbele ya mashabiki wake zaidi ya elfu thelathini waliofurika kuwapa morali wachezaji, walitulia na kucheza soka tangu mwanzo wa mchezo mpaka mwisho.
Kocha Mbrazil alianza na mfumo wa 4-5-1 walinzi Juma Abdul Oscar Joshua, Kelvin Yondani na Nadri Haroub “Canavvaro”, mbele yao wakicheza viungo wa Ulinzi Mbuyu Twite na Said Juma “Makapu” wakisaidiwa na Haruna Niyonzima, Mrisho Ngasa na mbrazil Jaja akianza mshambuliaji peke yake.
Kipindi cha kwanza kilianza kwa kasi kwa timu zote kusaka bao la mapema, mipira mirefu ya Mbuyu Twite kwa Mrisho Ngasa haikuwa na madhara sana langoni mwa timu ya Azam katika dakika 10 za mwanzo.
Kiungo Said Juma “Makapu” alikosa nafasi ya kuipatia Young Africans bao la kwanza dakika ya 10 baada ya mpira wa kona uliopigwa na Niyonzima, huku Nizar Khalfani pia akikosa kuifungia pia timu yake bao baada ya shuti la faulo alilopiga kutoka mita chache pembeni mwa lango la Azam.
Young Africans iliendelea kulishambulia lango la Azam FC kupitia kwa washambuliaji wake Geilson Santos “Jaja” Mrisho Ngasa na Nizar Khalfani lakini kutoku makini kulipelekea timu zote kwenda mapumziko zikiwa sare ya kutofungana.
Kipindi cha pili Young Africans ilianza kwa kufanya mabadiliko ambapo kocha aliwaingiza Hassan Dilunga na Saimon Msuva waliochukua nafasi za Said Juma na Nizar Khalfani hali iliyopelekea kikosi cha mbrazil Maximo kutawala eneo la kiungo.
Dakika ya 58 Geilson Santos “Jaja” aliwainua vitini mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu ya Young Africans baada ya kuipatia timu yake bao la kwanza katikati ya walinzi wawili wa Azam FC akiitumia vizuri pasi ya Saimon Msuva.
Geilson Santos “Jaja” dakika ya 66 ya mchezo aliwainua tena vitini washabiki, wapenzi na wanachama baada ya kufunga bao la pili kwa ufundi wa hali juu, baada ya kupenyezewa pasi nzuri na kiungo Hassan Dilunga na Jaja kuukota kwa hatua moja na kisha kumchambua mlinda mlango wa Azam FC Mwandini Ali kwa kuunyanyua kwa ufundi na kuamsha shangwe na nderemo uwanjani.
Huku wapenzi wa soka wakidhania mpira umemalizika, Saimon Msuva alimaliza ndoto za timu ya timu ya Azam kutwaa Ngao ya Jamii baada ya kuipatia timu yake bao la tatu na ushindi na kuifanya Young Africans kuchukua Ngao ya Jamii kwa mara ya nne tangu kuanzishwa kwake huku Simba wakiwa wamechukua mara mbili na Mtibwa Sugar mara moja.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Young Africans 3 – 0 Azam FC.
Mara baada ya mchezo huo kocha mkuu wa Young Africans mbrazili Marcio Maximo amesema anawashukuru wachezaji wake kwa kucheza kwa kufuata maelekezo yake hali iliyoplekea kucheza soka safi la kuburudisha linaloambatana na ushindi.
Aidha Maximo amesema baada ya ushindi wa leo maandaliz ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar yataanza siku ya jumanne ambapo kwa kesho ametoa mapumziko kwa wachezaji wote pamoja na benchi la Ufundi.
Mwisho Maximo amewapongeza vingozi, waachezaji na washabik wa Young Africans kwa sapoti wanayoitoa kwa timu na kuomba wajitokeze kwa wingi pia mjin Morogoro mwishoni mwa wiki katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar.
Young Africans: 1. Deo Munish “Dida”, 2. Juma Abdul, 3.Oscar Joshua, 4. Nadir Haroub “Cananavao” (C), 5.Kelvin Yondani, 6.Mbuyu Twite, 7.Said Juma “Makapu”/Hassan Dilunga, 8.Haruna Niyonzima/Hamis Kizza, 9.Geilson Santos “Jaja”/Hussein Javu, 10.Mrisho Ngasa/Omega Seme, 11.Nizar Khalfani/Saimon Msuva/
Azam FC: 1.Mwadini Ali, 2.Shomari Kapombe, 3.Erasto Nyoni/Gadiel Michael, 4.David Mwantika, 5.Agrrey Morrsi, 6.Kipre Balou, 7.Himid Mao/Kelvin Friday, 8.Salum Abubakar, 9.Didier Kavumbag, 10.Kipre Tchetche/Ismail Diara, 11.Leonel st.Pres/Khamis Mcha
Source: Yanga official website
No comments:
Post a Comment