Pages

September 6, 2014

NI MSIBA NZITO, WATU 44 WAPOTEZA MAISHA KATIKA AJALI YA BASI LA J4 EXPRESS NA MWANZA COACH BAADA YA KUGONGANA USO KWA USO MUSOMA.

Hali ilikuwa hivi katika eneo la tukio lililotokea ajali ya mabasi kupaata ajali baada ya kigongana.

AJALI za barabarani zimeendelea kugharimu uhai wa Watanzania, baada ya jana watu 44 kufa katika ajali mbili zilizotokea katika mikoa ya Mara na Rukwa. Kati yao, 36 wamekufa katika ajali iliyohusisha mabasi mawili katika eneo la Sabasaba, wilayani Butiama katika mkoa wa Mara wakati wengine wanane wamekufa katika ajali ya lori aina ya Mitsubishi Fuso.

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Phillip Kalanji alithibitisha kutokea kwa ajali mkoani Mara, akisema ilitokea saa 5 asubuhi ikihusisha magari matatu, yakiwemo mabasi yaliyogongana uso kwa uso na gari dogo aina ya Nissan Terrano lililogongwa na kutumbukia mtoni.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Butiama, alisema taarifa ya vifo 36 na majeruhi 79 zilikuwa za awali kwa kuwa walikuwa wanaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo ya mabasi kugongana katikati ya daraja.

Aliyataja mabasi yaliyogongana ni Scania lenye namba za usajili T 736 AWJ mali ya kampuni ya Mwanza Coach lililokuwa linatokea Musoma kwenda Mwanza na jingine aina ya Zoutong, lenye namba za usajili T 677 CYC mali ya kampuni ya J4 Express lililokuwa linatokea Mwanza kwenda Musoma. Gari dogo lililogongwa aina ya Nissan Terrano lina namba za usajili T 332 AKK.

“Kwa ujumla, hizi ni taarifa za awali, tunakwenda kwenye kutambua chanzo cha ajali, idadi ya abiria waliokufa katika kila gari na pia kuwatambua. Kwa ujumla ni ajali mbaya,” alisema Kamanda Kalanji.

Habari kutoka Sumbawanga zinasema kuwa watu wanane wamekufa papo hapo na wengine 11 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria jana kuacha njia na kupinduka katika Mlima Katete kijijini Milumba wilayani Mlele.

Akizungumza na HabariLeo Jumamosi kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema ajali hiyo iliyotokea saa 11 alfajiri ilihusisha lori aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 234 AXK.

Aliongeza kuwa gari hilo likiwa limesheni bidhaa mbalimbali lilikuwa likitokea kijiji cha Kibaoni wilayani Mlele likielekea mjini Sumbawanga mkoani Rukwa likiwa linaendeshwa na Jamal Mohammed (42) Mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam.

Kamanda Kidavashari amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Peter Lusambo (24), Ngelela Shauritanga (29), John Pius (32).

Mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja tu la Linus (30) wote wakiwa wakazi wa kijiji cha Kibaoni Wilaya ya Mlele.

Aliwataja wengine kuwa ni pamoja na Makono Kisumu (23), Elias Mussa (28) wakazi wa wilaya ya Geita Mwanza, Ally (34) mkazi wa Dar es Salaam ambaye alikuwa utingo wa gari hilo na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Abbas (28), mkazi wa Mtaa wa Mpanda Hoteli wilayani Mpanda .

Majeruhi ambao wamelazwa kwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ni pamoja na Kaswagula Linus (25), Peter Mkalala ( 30), Peter Lusambo (20) Castory Kaombwe (23) Nassor Ramadhan (22) wote wakiwa wakazi wa Kata ya Kibaoni Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi.

Wengine ni Salim Hassan (42) mkazi wa mjini Mwanza, Jamari Mohamed (42) Salumu Njomoke (22) wakazi wa Dar es Salaam na John Chambaneje (32) mkazi wa Mtaa wa Mpanda Hoteli mjini Mpanda.

Kamanda Kidavashari alisema chanzo cha ajali hiyo ni kukatika kwa chombo aina ya propela, hivyo kumshinda dereva wa gari hilo na kupinduka.

Kwa mujibu wa Kidavashari dereva wa gari hilo amekamatwa na jeshi la Polisi ambapo anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...