MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), amepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), baada ya kupata kura 165 kati ya kura 244 na kuwaacha wenzake mbali.
Katika uchaguzi huo, Mdee ambaye sasa amerithi nafasi ya Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo ambaye alimaliza muda wake, alichuana na Lilian Wassira, Mbunge wa Viti Maalumu, Chiku Abwao, Sophia Mwakagenda, Rebeka Mwagisha na Janeth Rith.
Baada ya Mdee kupata zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, ambaye alizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, alimtangaza Mdee kuwa mshindi katika raundi ya kwanza.
Wengine waliomfuatia kwa mbali ni Janeth aliyepata kura 35, Sophia kura 18, Abwao aliyejikuta akiambulia kura 15 huku Lilian akipata kura 11.
Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Bawacha Zanzibar, Makene alisema uchaguzi ulifanyika kwa mizunguko miwili ambapo Amida Abdalah aliibuka mshindi kwa kupata kura 194, akifuatiwa na Maria Msabaha aliyeambulia kura 36.
“Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, mshindi ni Hawa Mwaifunge kwa kura 136 akifuatiwa na Victoria Benedict kwa kura 96,” alisema Makene.
Alisema uchaguzi unaendelea ambapo Kamati Kuu itakaa leo kuandaa ajenda za kikao cha Baraza Kuu, kabla ya kuitisha Mkutano Mkuu wa chama, utakaofanyika kesho kumchagua Mwenyekiti wa Taifa na Makamu wake kwa Zanzibar na Bara.
“Septemba 15, Baraza Kuu litakutana kuchagua Katibu na makamu wake wa Tanzania Bara na Zanzibar na wajumbe wa Kamati Kuu na Septemba 16 Kamati Kuu ya chama, itakaa kufanya majumuisho yote,” alisema.
Akizungumzia ushindi wake, Mdee alisema wanawake wengi wamekuwa waoga kugombea nafasi mbalimbali za kisiasa na ushindi wake huo, ni chachu kwa wasichana wengine kuona kuwa wanaweza na fursa zipo wazi.
“Chaguzi bado zinaendelea na mpaka sasa bado hatujapata timu kamili, hivyo timu ikikamilika tutaweka wazi mikakati mbalimbali ya kumuinua mwanamke,” alisema.
Alisema watafanya ziara ya miezi miwili nchi nzima kuzungumza na wanawake ili wajitambue na kutambua kuwa Chadema ndio chama pekee kitakacholeta maendeleo.HABARILEO
No comments:
Post a Comment