Songea.
Wakati mazishi ya aliyekuwa mfanyakazi wa kiwanda
cha A to Z kilichopo jijini Arusha,Elias Sixmond Nditi(22) yaliyofanyika mwishoni mwa wiki nyumbani
kwao eneo la Mji Mwema,Songea mjini mkoani Ruvuma ndugu wa marehemu wameapa kuchukua
hatua za kisheria dhidi ya kiwanda hicho.
Mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye ni pacha wa Mama mzazi
wa Elias,Mary Nditi alisema kifo hicho kimewastua mno kutokana na kumfahamu vema marehemu kutokuwa na tabia za ulevi.
“Huyu ni mwanangu niliyemlea baada ya pacha
mwenzangu,Lucia Nditi kufariki dunia mwaka 2001,wakati akiwa hapa hatukuwahi kumuona
akinywa Pombe ,labda alivyofika huko alianza ulevi hatuwezi kufahamu,lakini
muda wa tukio tunaoambiwa alianguka kwenye Bwawa ni saa 9 mchana ni jambo lisiloingia akilini,kwani hakuna uzio au ulinzi,"alisema Mary
Alisema walikuwa wakiwasiliana mara kwa mara na Elias kwa
njia ya simu na kwamba aliwaambia kazi anazozifanya ni ngumu ukilinganisha na
mshahara anaolipwa wa Sh 105,000 kwa mwezi na alikua akipanga kurejea nyumbani
pindi akipata nauli.
Taarifa iliyotolewa na Polisi mkoani Arusha kwa vyombo
vya habari ilisema tukio hilo lilitokea Agosti 12,mwaka huu kwenye kiwanda
hicho baada ya mfanyakazi huyo kukutwa akiwa amefariki dunia kwenye Bwawa la
kuhifadhia maji yanayotumika kiwandani hapo.
“Uchunguzi wetu wa awali unaonesha marehemu alionekana
muda wa saa 9 alasiri akiwa eneo hilo la kiwanda huku akiwa amevua nguo na
kukaa kwenye kingo za shimo hilo la kuhifadhia maji,baadaye hakuonekana lakini nguo zake zikiwa kwenye kingo la Bwawa
ndipo wafanyakazi wenzake waligundua alikuwa amekwishafariki dunia” ilisema
taarifa ya polisi.
Hata hivyo ndugu mwingine wa marehemu aliyejitambulisha
kwa majina ya Fransis Kahimba alisema mwili wa ndugu
yao baada ya kuuchunguza waliona ukiwa na jeraha kwenye jicho lake la kulia
hali inayoonesha aligongwa na kitu chenye ncha kali.
Alisema wakati wakiwa kwenye lango la kuu la kiwanda
hicho wakifatilia kifo cha ndugu yao walishangazwa na kauli zilizokuwa
zikitolewa na wafanyakazi kuwa masuala ya vifo eneo hilo ni jambo la kawaida
sana.
“Unajua hapo kiwandani kuna takribani wafanayakazi 9,000
ambao ukiwasikiliza shuhuda wanazotoa utashangaa kama haya mambo yanafanyika
hapa Tanzania,na kama ni uwekezaji tuu ndio unafanyika au kuna mambo mengine
yakiwamo ya ukiukwaji wa haki za binadamu na hakuna hatua za kisheria
zinazochukuliwa,”alisema Kahimba
No comments:
Post a Comment