August 8, 2014
KATIBA MPYA !!! CHADEMA YAWACHIMBIA MKWARA MZITO WABUNGE WANAOUNDA UKAWA, AKIWEMO MTOTO WA NYERERE.
Mjumbe wa Bunge la Katiba (Chadema) Said Arfi akisaini karatasi ya mahudhurio bungeni jana, kabla ya kwenda kushiriki mjadala wa kamati yake . Picha na Emmanuel Herman
Dodoma. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama chake hakitavumilia vitendo vya usaliti na kwamba mwanachama yeyote atakayekiuka maagizo ya chama hicho atachukuliwa hatua kali.
“Katika hili hatutakuwa na mchezo na naomba niweke wazi kabisa kwamba usaliti hausameheki. Tuna vikao vya chama vinakuja siku za karibuni mtu yeyote ambaye atabainika kusaliti uamuzi wa chama, uwe wa Kamati Kuu au mwingine wowote, tutachukua hatua hata kama ni kumfukuza uanachama,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo alikuwa akizungumzia taarifa za kuwapo bungeni, Dodoma kwa baadhi ya wanachama wa Chadema, kinyume cha makubaliano ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wabunge hao ni Leticia Nyerere (Viti Maalumu), John Shibuda (Maswa Mashariki) na Said Arfi (Mpanda Mjini) ambaye aliwasili jana na kwenda kushiriki kwenye kikao cha kamati namba 10 kilichokuwa kikifanyika Ukumbi wa Internet, Chuo cha St. Gaspar.
Mbowe alisema baada ya viongozi wakuu wa Ukawa kukubaliana kwamba hawatashiriki katika awamu ya pili ya Bunge Maalumu, kila chama kiliwaelekeza wabunge wake kuhusu msimamo huo ambao pia uliridhiwa na vikao vya vyama husika.
“Sisi suala hili limepitishwa na Kamati Kuu ya Chadema, sasa wewe ni nani kukataa, kupinga au kwenda kinyume cha matakwa ya Kamati Kuu? Ole wake mtu atakayethubutu kushiriki hivyo vikao vya Kamati za Bunge,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Wakati tunagombea ubunge 2010 hakukuwa na ahadi kwamba kutakuwa na Bunge la Katiba, hili limetokea tu, sasa kama sisi kwa masilahi mapana ya umma tunauona mchakato hauko sawa, kwa nini wewe ulazimishe kushiriki, unakwenda Dodoma kumwakilisha nani?”
Vyama vingine vyenye wabunge ambavyo pia wanachama wake wamesusia Bunge Maalumu ni NCCR Mageuzi na CUF. Kadhalika Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila ni miongoni mwa waliosusia vikao hivyo.
Kauli ya Arfi
Akizungumzia uamuzi wa kushiriki Bunge alisema licha ya kwamba yeye ni mwanachama wa Chadema, ameingia bungeni akiwa mwakilishi wa wananchi katika kutunga Katiba na kwamba ndani ya Bunge hakuna vyama, bali wawakilishi wa wananchi.
Alisema anaamini katika muungano wa Serikali tatu na kwamba kama kuna mgongano uliojitokeza lazima uamuliwe ndani ya mkutano wa Bunge na kwamba kutoka nje ya Bunge ni dalili ya woga na yeye siyo mwoga.
“Ndiyo nipo kwenye kikao cha kamati namba 10, hivi sasa hatujamaliza,” alisema Arfi kupitia ujumbe mfupi wa simu yake ya mkononi baada ya mwandishi wetu kumuuliza jana.
Alipoulizwa haoni kwamba kufanya hivyo ni kukiuka maelekezo ya chama chake, Arfi alijibu: “Lakini ipo haki ya uwakilishi, hiyo unaiondoaje? Tutaona itakavyokuwa.”
Hata hivyo, Shibuda na Nyerere licha ya kudaiwa kwamba wamesaini kama ishara ya kuripoti katika Bunge Maalumu la Katiba, hawajaonekana katika vikao vya kamati zinazoendelea.
Shibuda alisema jana kwamba hakuwapo Dodoma huku kukiwa na taarifa kwamba Nyerere tayari ameshaondoka kurejea Mwanza tangu juzi jioni baada ya vyombo vya habari kubaini uwepo wake.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Hamis Hamad alisema jana kwamba wajumbe hao pamoja na yule wa CUF, Clara Mwatuka hawatalipwa posho yoyote hadi pale Bunge litakapojiridhisha kwamba wanahudhuria vikao.
“Tulivyofuatilia attendance (mahudhurio) kwenye kamati, tukakuta kwamba majina yao hayamo, nikafuatilia fedha asubuhi ya leo (jana) na nikagundua kwamba hawakuwahi kulipwa na hawakwenda kuchukua,” alisema Hamad.
Hoja ya posho
Mbowe alisema baadhi ya wajumbe wa Ukawa ambao wamejiandikisha kwamba wanahudhuria vikao vya Bunge lakini hawaonekani kwenye vikao vya kamati, wamefuata posho.
“Huo ni wizi maana kama mtu amekwenda Dodoma halafu akajiandikisha halafu haonekani kwenye vikao, huo ni wizi wa mchana na mtu wa aina hiyo anapaswa kuchukuliwa hatua,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Wana njaa ya fedha na wanafanya hivyo kwa sababu wanaogopa kuhukumiwa na umma kwamba wameusaliti. Kwa hiyo wanaona njia nyepesi ya kupata posho ni kujiandikisha kimyakimya au kwa kificho halafu walipwe ile posho ya kujikimu”.
Alikiri Sh300,000 ni nyingi na kwamba wabunge wangependa kupata fedha hizo lakini akasema mtu yeyote ambaye anaweka mbele masilahi ya posho yake na kuacha misingi ya kuutetea umma na utaifa, hafai kuwa kiongozi.
“Siyo kwamba wabunge wetu hawapendi kupata hizo fedha, hapana, lakini unausalitije umma wa Watanzania kwa sababu ya Sh300,000 kwa siku? Hiyo ndiyo gharama ya kuwa kiongozi tena anayetetea masilahi ya watu.
Kuhusu taarifa kwamba baadhi ya wabunge wamekuwa wakionekana Dodoma, Mbowe alisema lazima ifahamike kwamba mji huo ndiko yaliko makao makuu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano hivyo kuonekana huko siyo dhambi.“Masuala mbalimbali ya kiutawala na kihuduma yanafanyika Dodoma, wabunge wana familia Dodoma na hata ofisi zetu za Kambi ya Upinzani Bungeni zipo hapo, sasa kama mimi nikiamua kuja kwenye ofisi zangu mtasema kwamba nimekuja kujadili Katiba?” alihoji Mbowe.MWANANCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment