Akizungumza
kwenye Mahafali ya Chuo cha Uuguzi cha Masista wa Kanisa Katoliki
Kanosa Mugana, Wilaya ya Misenyi, Mkoa wa Kagera jana, Sitta alisema
wengi wa waliotangaza nia hawafai na kwamba wanapiga porojo tu.
Dar es Salaam/Misenyi.
Mjadala wa urais mwaka 2015 unaonekana
kuanza kuitikisa nchi kutokana na vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kuendelea kujitokeza hadharani na kutangaza nia, huku wasomi, viongozi
wa dini, wanaharakati na vyama vya siasa wakitaja sifa za mgombea.
Mmoja wa vigogo
hao wa CCM ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta
ambaye jana alijitokeza na kusema atajitosa kwenye kinyang’anyiro cha
urais iwapo wataendelea kujitokeza wasiokuwa na sifa.
Akizungumza
kwenye Mahafali ya Chuo cha Uuguzi cha Masista wa Kanisa Katoliki
Kanosa Mugana, Wilaya ya Misenyi, Mkoa wa Kagera jana, Sitta alisema
wengi wa waliotangaza nia hawafai na kwamba wanapiga porojo tu.
Sitta
alisema wengine wamejitokeza kwa ‘gia’ ya ajira, lakini hawabainishi
chanzo chake, kwani tatizo hilo limetokana na ufisadi kwa baadhi ya
viongozi.
Aliwataka wananchi kuwapima wagombea kwa makini
kwani wapo baadhi yao wanajinadi kuwa wao ni vijana kitu ambacho siyo
kigezo cha kuwa rais.
“Ndugu zangu Watanzania, tusipowachuja
watu kwa chujio la tabia zao, tutaangukia mtego wa kuwapima watu kama
vile tunafanya mzaha, maana kuna wengine wameanza kusema nichagueni mimi
ni kijana, hivi kwani urais ni mashindano ya ulimbwende, tunatafuta
mzuri?” alihoji.
Awaponda waliotangaza nia
Alisema akiangalia orodha ya waliojitokeza haifai na kwamba, labda watu kama wawili wanaoweza kuungwa mkono lakini hakuwataja.
Waziri
Sitta alitumia hadhara hiyo kuihadharisha jamii kuona suala la uchaguzi
wa rais kama jambo la kawaida, kwani ikicheza nchi itazama.
”Niseme
jingine, kwa kuwa nikitazama hiyo anga ya hawa wanaotafuta ukubwa,
nawaona kama mmoja wawili ndiyo kidogo unaweza kuwaunga mkono. Hali hii
ikiendelea namna hii, eeh itabidi na sisi wazee tujitose manake ikiwa
watu wenyewe hawa ni walaghai, wengine ni waongo, wengine rekodi mbaya,
wengine walishiriki kuhujumu nchi, ndiyo wanakwenda kimbelembele
wanapigana vikumbo.
Wasomi, wanaharakati
Wakati
Sitta akisema hayo, wasomi, wanasiasa na wanaharakati wamesema rais
ajaye anatakiwa kuwa mzalendo, msomi, mwadilifu, mchapakazi, anayejua
matatizo ya nchi na wananchi na akubali kuyatatua, asiwe mbaguzi, mwenye
uamuzi mgumu, anayetanguliza masilahi ya taifa mbele na atakayepambana
na rushwa na ufisadi kwa vitendo.
Kauli za wadau hao
zimekuja kipindi ambacho watu wa kada mbalimbali, hasa kutoka ndani CCM
wakiweka wazi nia zao za kugombea urais mwaka 2015, kufikia hatua ya
chama hicho kuwapa adhabu makada wake sita, kutokana na kuanza kampeni
mapema.
Makada waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa tuhuma za
kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati ni January Makamba,
Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick
Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe. Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu)
Steven Wassira pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini
ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Makamba
takribani siku nane zilizopita akiwa jijini London, Uingereza,
alitangaza nia yake ya kuwania urais mwaka 2015, akisema huu ni wakati
wa fikra mpya ambazo zinahitaji vijana na kwamba wazee wakae kando.
Hata
hivyo, Makamba alipingwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye alisema kuwa
naibu waziri huyo anataka mambo makubwa, kwamba, “asilazimishe” kwa kuwa
wakati ukifika atapata kile anachokitaka. Alhamisi iliyopita Sumaye
akiwa mkoani Mwanza alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari, akisema
kuwa ana nia ya kugombea urais, lakini mpaka atakapoombwa kufanya
hivyo.
Januari mosi mwaka huu, licha ya kutokuweka wazi
Lowassa alitangaza kuanza rasmi kwa safari aliyoiita ya matumaini ya
ndoto zake, ambayo amesema itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu
bure, majisafi na maendeleo ya uhakika.
Hata hivyo, makada
hao huenda wakakumbwa na rungu jingine baada ya siku tatu zilizopita
chama hicho kutoa maagizo kwa Kamati yake ya Usalama na Maadili
kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa adhabu kwa vigogo hao waliotangaza
nia kabla ya wakati.
Wasomi
Profesa wa Chuo
Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema nchi ilipofikia inahitaji
rais mwadilifu atakayekuwa tayari kuchukua uamuzi mgumu bila woga kwa
viongozi wote ambao hawatakuwa waadilifu.
“Umri siyo hoja
wala taabu, tunataka rais anayethubutu kutenda haki na mwenye kuzingatia
maadili, kuwaunganisha Watanzania wote, lakini aweze kuchukua hatua kwa
wasio waadilifu hata kama ni ndugu, jamaa au rafiki yake.
Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Tolly Mbwete alisema,
rais ajaye anatakiwa awe mwelewa wa kiasi kikubwa hasa katika masuala ya
uchumi na mwenye muono wa Tanzania mpya alipoikuta na anakotaka
kuifikisha.
Wanaharakati
Mkurugenzi Mtendaji wa
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba
alisema nchi ilivyo sasa suala la umri isiwe sababu, kwani mtu yeyote
anaweza kuwa rais.
Alisema rais ni lazima awe mtu mwenye upeo mkubwa wa kupokea mabadiliko yatakayojitokeza na kuyafanyia kazi.
“Ujana
haunipi shida, lakini ana uwezo? Kuna vijana wako makini kutuongoza,
hivyo tusiwanyime nafasi kwa umri wao. Tuangalie ni jinsi gani atatatua
changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi,” alisema Dk Bisimba.
Aliyekuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Ussu Mallya
alisema, “Kiongozi tunayemtaka awe anaelewa na awe na msimamo thabiti wa
kuendeleza nchi bila kujali kuwa ni mwanamke, kijana, mwanaume au
mzee.” Aliongeza; “Tunahitaji kumpata kiongozi atakayepambana na rushwa,
uzembe na kipindi hiki mtu wa aina hii ndiyo tunayemtaka.”
Vyama vya Siasa
Mwenyekiti
wa Umoja wa Vijana Chadema (Bavicha), John Heche alisema umri, jinsia
na rangi haijawahi kuwa sifa ya urais hiyo ni kampeni ya kibaguzi.
Alisema
rais anayehitajika ni yule anayejua matatizo ya wananchi, atakayeitoa
nchi iliyo katika matumaini yaliyofifia kwenda mbele zaidi.
Katibu
Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alitaja sifa nne za
rais ajaye na kufafanua kuwa umri ni kigezo cha kibaguzi.
“Rais
lazima awe mzalendo, mwenye maadili, anayejua matatizo ya nchi yake na
Watanzania na awe na majibu yake na asimamie misingi ya utawala bora
iliyoanza kupotea na kuhakikisha kuwa anapambana na rushwa na ufisadi,”
alisema.
Viongozi wa dini
Wakizungumza na gazeti
hili Askofu Furaha Mwambusye wa Kanisa la Haven of Peace, Ammy Mwakitalu
wa Kanisa la TAG-Tabata, David Samson (Jesus Power-Musoma) na Boniphati
Makasi (EAGT-Bunju) na Askofu Mkuu wa Kanisa la Power Miracle, Joachim
Peter walitaja sifa nne za anayefaa kugombea nafasi hiyo.
Akizungumza
kwa niaba ya wenzake, Askofu Peter alitaja sifa ya kwanza kuwa ni
kiongozi mwenye kumcha Mungu, ambaye hatakuwa tayari kufanya jambo bila
kumshirikisha Mungu. “Taifa letu halihitaji viongozi wenye tuhuma za
rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka,” alisema Petre.
Alisema sifa ya tatu ni kuwa na kiongozi ambaye hayupo katika vita, ugomvi na mapambano na viongozi wenzake.
“Ugomvi wa aina hii unaweza kuzaa visasi ambavyo hudumaza amani na maridhiano ya viongozi,” alifafanua.
Alisema
sifa ya nne, kiongozi atakayeweza kukabiliana na changamoto mpya
zinazolikabili taifa, likiwemo suala la elimu, umaskini na
ajira.MWANANCHI
No comments:
Post a Comment