Pages

July 27, 2014

SOMA KISA CHA MTOTO ALIYEIBWA TANDALE AKUTWA KOROGWE


Mama mzazi wa Marylin Repyson (kulia), Elida Fundi, akiwa amembeba mwanawe huku akiomba jana baada ya kuwasili nyumbani kwake Changanyikeni jijini Dar es Salaam. Picha na Fidelis Felix.
HATIMAYE kinara wa wizi wa watoto jijini Dar es Salaam, Amir Juma, amekamatwa na Jeshi la Polisi akiwa mkoani Tanga.

Juma anadaiwa kumuiba mtoto, Merlin Repyson (4) katika eneo la Changanyikeni siku nane

zilizopita.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo akiwa wilayani Korogwe.

“Ni kweli mtuhumiwa huyo amekamatwa huko Korogwe na polisi wetu kwa kushirikiana na wenzao waliotoka Dar es Salaam,” alisema Kamanda Massawe.

Alisema tayari mtuhumiwa alisafirishwa jana asubuhi kupelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

MAMA ASIMULIA
Mama mzazi wa Merlin, Elida Fundi katika mahojiano maalumu na MTANZANIA alianza kwa kusema: “Mungu ni mkubwa nashukuru kwa maombi yenu, Merlin alipotea siku nane zilizopita lakini amepatikana akiwa mzima.

“Ni jambo la kumshukuru Mungu, watoto wengine wakipotea wanakutwa wametobolewa macho, lakini kwa uwezo wa Mungu na maombi yenu mwanangu amepatikana mzima,” alisema Elida.

Alisema mwanaye alipatikana juzi saa 9:30 alasiri na kupigiwa simu na polisi wa kituo cha Oysterbay wakitaka aende Hospitali ya Mnazi Mmoja.

Alisema baada ya kufika Hospitali ya Mnazi Mmoja, alikutana na askari polisi aliyekuwa amevaa nguo za kiraia huku akiwa amembeba Merlin ambaye alikuwa anafanyiwa vipimo kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.

Alisema baada ya kukamilika kwa vipimo vyote, majibu yalipotoka yalionyesha Merlin hana tatizo lolote linalomsumbua.

“Pamoja na kumuona mwanangu akiwa hana ugonjwa wowote, nilishtuka mno kwa sababu alikuwa amelegea kama vile alikuwa na njaa kali,” alisema Elida.

Alisema baada ya kukabidhiwa mtoto wake, aliamua kumbadilisha nguo alizokuwa amevaa kwani siku alipoibwa alikuwa na nguo tofauti na hizo.

“Baada ya kumbadilisha zile nguo niliamua kuzichoma moto pale pale hospitali, nikiamini hazifai kuvaliwa na mwanangu… kama unakumbuka mwanangu aliibwa Julai 15, mwaka huu mpaka nakabidhiwa jana (juzi) Julai 23,” alisema.

MTANZANIA lilifika nyumbani kwa Elida katika eneo la Changanyikeni juzi saa 11:30 jioni baada ya kupata taarifa za tukio hilo na kushuhudia ndugu, jamaa na marafiki wakiwa wamekusanyika.

Ilipofika saa 3:30 usiku msafara wa magari mawili madogo ulionekana ukiingia ndani ya uzio wa nyumba ya mama Merlin, huku shangwe vigelegele vikitawala kwa ndugu na jamaa waliokuwepo nyumbani hapo.

Baada ya muda mfupi, alishuka mama Merlin akiwa na mwanaye ambaye alionekana kuwa katika hali ya kawaida.

Tukio hilo lilipokelewa kwa vigelegele, nderemo na nyimbo za kuabudu zikitawala.

Baada ya kushuka kwenye gari Merlin ndugu na jamaa walimzunguka huku kila mmoja akiwa na shauku kubwa ya kutaka kumbeba na kupiga naye picha.

Baada ya shamra shamra hizo, Elida alishika kitabu cha sala za novena na kuanza kufanya maombi na kuimba nyimbo za mapambio wakishirikiana na wana ndugu.

Baada ya sala ya awali, alifika Mwinjilisti wa Kanisa Katoliki Ubungo, Michael Kobelo na kuanza kusali tena kwa mara ya pili huku akimshika Merlin kichwani na kumuombea.

Akizungumza na gazeti hili baada ya kumalizika shughuli zote, Elida alisema kwa siku nane za kupotea mwanaye aliishi katika maisha magumu.

“Nimeishi katika wakati mgumu mno, sijawahi kupotelewa na mwanangu kiasi hiki…tumesali na kufunga siku zote nane ili Merlin apatikane akiwa katika afya njema.

“Hali ilikuwa mbaya nilisimamisha shughuli zangu zote hakuna aliyekuwa anakula chakula, familia nzima kwa kushirikiana na waumini wenzangu tulifunga novena ya siku tisa na leo (juzi) ni siku ya tano, tutaendelea mpaka zitakapoisha kwa sasa tutakuwa tunamuombea afya na kumuepusha mambo yote mabaya ambayo yataweza kumtokea baada ya hili,” alisema Elida.

Alisema familia kwa kushirikiana na waumini wa Kanisa Katoliki Changanyikeni, walikuwa na utaratibu wa kusali novena kila siku kuanzia saa 2:30 usiku.

Akisimulia kupatikana kwa mtoto wake, anasema: “Nilipigiwa simu na mume wangu ambaye naye alipigiwa na polisi kuwa mtoto amepatikana katika eneo la Tandale kwa Mtogole,” alisema Elida.

“Nilifurahi sana nilivyomuona mwanangu lakini alikuwa amechoka mno, kitu kingine nilichokikuta tofauti ni nywele, alikuwa na nywele fupi lakini sio hizi wamempunguza tena tofauti na ilivyokuwa mwanzo, nilimuuliza ulikuwa wapi akanijibu kuwa alikuwa kwa bibi,” alisema Elida.

Kuhusu Juma ambaye anadaiwa kumuiba mtoto huyo, Elida alisema aliwahi kufanya kazi katika moja ya biashara za mume wake zilizopo eneo la Mwenge.

Alisema Juma alimchukua Merlin na kumpeleka kwa mama aliyekuwa akiishi na mtoto huyo siku zote mpaka polisi walipofanikiwa kumuona.

“Mimi nimeshangaa sana, hivi watu wanaishi dunia gani nasikia uko Tandale muda wote aliokuwepo alikuwa anatoka nje na anacheza na watoto wenzie kama kawaida,” alisema Elida.

Elida alilimwagia sifa MTANZANIA kwa kuandika ukweli wa taarifa hiyo uliosaidia kupatikana kwa mwanaye.

Merlin azungumza

Merlin alipoulizwa na MTANZANIA alikuwa wapi alijibu hivi:

“Nilikuwa nakaa na bibi mbali, nilikuwa nakula chipsi na juisi wakati nipo kwa bibi,” alisema Merlin.

MTUHUMIWA
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zinasema mawasiliano ya simu ndiyo yaliyosaidia alipo mtuhumiwa.

Taarifa hizo zinasema siku ya tukio mawasiliano yalionyesha Juma alikuwa eneo la Changanyikeni na baadaye Tandale kwa Mtogole.

Baada ya hapo mawasiliano yalionyesha Juma alikuwa Manzese kabla ya kupiga simu ambayo ilionyesha yuko Magomeni.

Baada ya kutoka Magomeni, alielekea Mbagala na baadaye Tandika kabla ya kuanza safari ya kwenda Korogwe mkoani Tanga ambako alikamatwa.

MAJIRANI TANDALE
Baadhi ya majirani waliokuwa wanaishi na mama Mwanahamisi aliyekuwa akiishi na Merlin nyumbani kwake Tandale Kwamtogole, wamesema hawakuwa na taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo.

Akizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wanafamilia ambaye ni mtoto wa dada wa mtuhumiwa alisema kipindi chote tangu Merlin alipopelekwa hawakuwa na taarifa yoyote kama ameibwa.

“Kwa kweli huyo mtoto tangu alipoletwa na Juma zimepita kama siku tano hivi na huyo kijana aliomba aishi hapa na sisi na baada ya siku tatu atakuja kumchukua ampeleke kwao Tanga.

“Alituambia Merlin ni mwanaye ambaye alimzaa nje ya ndoa, hivyo endapo angempeleka nyumbani kwake angeweza kusababisha ugomvi mkubwa na mkewe.

“Juma alikuwa anakuja mara moja moja wakati wa usiku kumjulia hali Merlin akiwa na mfuko wa chips, jambo ambalo lilisababisha tuamini ni mwanaye,” alisema.

Alisema siku ya tukio Amir alifika nyumbani kwao jioni akiwa na mtoto huyo na kumkabidhi kwa mama yao mdogo.

Alifafanua kuwa muda wote ambao Merlin alikuwapo nyumbani hapo, alikuwa mchangamfu kwa watu na watoto wenzake.

Alieleza Merlin alikuwa tofauti kimuonekano na watoto wengine wa mtaani hapo kwa kuwa yeye anaonekana kalelewa katika familia ya kifahari.

“Alikuwa tofauti sana na wenzake wakiwa wanacheza utaona kabisa yeye ametokea katika familia ya watu wanaojiweza, wakati mwingine katika maongezi na watoto wenzake alikuwa akisema kuwa anasoma Don Bosco,” alisema dada huyo.

MWENYEKITI
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mtogole, Ramadhani Kabanga, alisema baada ya kupokea taarifa hizo jana jioni, alifanya uchunguzi na kubaini kuwa Juma alikuwa akiishi eneo hilo.

Alisema taarifa alizokuwa nazo ni kwamba, Juma aliamua kumuiba Merlin kwa sababu wazazi wa mtoto huyo walimdhulumu fedha zake wakati akiwafanyia kazi.

“Sijapata taarifa kamili kuwa ni kiasi gani cha fedha ambacho alikuwa anadai huyo kijana hadi ikafikia hatua ya kuamua kumchukua mtoto kinyemela wakati akijua ni kosa,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...