RAIS
Jakaya Kikwete amesema uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ulikuwa
ufanyike mwezi Oktoba mwaka huu, huenda ukasogezwa mbele kutokana na
kutokamilika kwa mchakato wa rasimu ya mabadiliko ya Katiba.
Kauli hiyo ameitoa kwenye mkutano wa majumuisho ya ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Tanga.
Alisema
kulingana na hali ilivyo hivi sasa ambapo Bunge la Katiba
halijakamilisha kazi zake, ni dhahiri kwamba uwezekano wa kufanyika kwa
uchaguzi huo kwa kutumia Katiba mpya haupo.
“Kwa
mfano, wabunge endapo wataamua wapitishe kwamba katiba itambue serikali 3
ni lazima kwanza itungwe katiba ya Tanganyika ambayo itaainisha
taratibu zitakazotoa mwongozo wa uchaguzi…hata kama itabaki kama ilivyo
…. bado muda wa kuandaa huo utaratibu wa uchaguzi wa serikali za mitaa
hautatosha kwa sasa”, alisema.
Aidha
aliongeza, “Nimeona niliseme hili japo kwa ufupi kwamba uchaguzi huu
huenda utalazimika kusogezwa mbele kutokana na kutokamilika kwa mchakato
wa Rasimu ya mabadiliko ya Katiba“, alisema.
Katika
hatua nyingine, Rais amewataka Maofisa Kilimo kwenye halmashauri
kujiendeleza kitaaluma na kuwa mabingwa waliojikita katika taaluma ya
mazao yanayostawi kwenye maeneo yao badala ya kuyashughulikia kwa ujumla
mazao yote yanayolimwa na wananchi.
Alisema
utekelezaji wa agizo hilo utaongeza mavuno kwa zao husika, utapanua wigo
wa uzalishaji pamoja na utaalamu katika kushughulikia zao, aina ya zao
na kuleta tija katika sekta ya kilimo.
Alisema
hatua ya maofisa kilimo kuendelea kujishughulisha kwa ujumla na mazao
yote yanayostawi bila kuwa na lengo la kusimamia mazao maalumu,
kunaifanya sekta hiyo kudumaa na hivyo kushindwa kuwakwamua kiuchumi
wananchi.
“Nimegundua
kwamba watu wetu wengi hawana utaalamu uliobobea…hata maofisa kilimo
wetu hawana taaluma maalumu zilizojikita kwenye aina ya mazao mengine
zaidi ya mpunga na mahindi, hatua ambayo inawasababisha washindwe
kusimamia vizuri uzalishaji wa mazao mengine ambayo yangeweza kuwakwamua
kiuchumi wakulima kwenye halmashauri husika,” alisema.
Aliongeza, “Kwa
hiyo ni jukumu lenu viongozi wa halmashauri kuwachukua maofisa kilimo
wenu na kuwapeleka SUA kwa ajili ya ku-specialize (kujikita) kulingana
na vipaumbele vyenu vya mazao kwa sababu sio wote wanao ubingwa katika
kila zao…tukifanikiwa kwenye hilo tutapata mafanikio zaidi”, alisema.
Aidha
aliwataka viongozi kwenye mkoa wa Tanga kuhakikisha shughuli za kilimo
zinajikita kwenye uzalishaji endelevu wa mazao ya matunda na mboga, kwa
kuwa mkoa huo uko katika fursa nzuri kiuzalishaji zaidi ya mazao ya
nafaka.
No comments:
Post a Comment