Moshi. Jeshi la Polisi linamshikilia dereva
mmoja wa pikipiki, maarufu kama bodaboda wilayani Mwanga mkoani
Kilimanjaro baada ya mke wa askari polisi kukutwa amekufa chumbani kwa
dereva huyo.Tukio hilo ambalo limezua
gumzo kubwa wilayani humo lilitokea juzi saa 12:00 jioni katika eneo la
New Mwanga wilayani humo na mtuhumiwa akidaiwa kukutwa akiwa amelewa
chakari.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea.“Hilo
tukio lina ukweli na bahati mbaya sana mumewe ndiyo kwanza amehamishiwa
Geita na alikuwa akaripoti halafu aje kuchukua familia yake,” alisema
Ndemanga.
Mkuu
huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama
ya wilaya hiyo, alisema hadi sasa haijafahamika nini kilitokea na kwamba
hilo ni moja kati ya mambo ambayo polisi inachunguza.“Hayo
yote kwamba ilikuwaje akawa chumbani kwa huyo kijana, nini sababu za
kifo yatajulikana kadiri upelelezi unavyoendelea,” alisema.
Imeelezwa kuwa jana ilikuwa siku ya askari huyo kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi.
“Mpaka
sasa hivi haijajulikana nini hasa kilitokea huko chumbani na ilikuwaje
akawa chumbani kwa huyo dereva,” alisema mmoja wa watu waliokuwapo
katika eneo la tukio ambaye hata hivyo, hakutaka kutaja jina lake na
kuongeza kuwa jana saa sita mchana, mwili wa mwanamke huyo ulichukuliwa
kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mwanga na kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa
ya KCMC kwa uchunguzi.
Taarifa za awali zinasema kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na mikwaruzo shingoni hali inayotia shaka kuwa huenda alinyongwa.
Habari
nyingine zinadai kuwa siku ya tukio, mwanamke huyo alikuwa ameaga kuwa
anakwenda kanisani lakini baadaye simu yake ilipopigwa ilikuwa ikipokewa
na mwanamume.
Ilidaiwa
kuwa mume wa marehemu alipojaribu kupiga simu ya mkewe, ilikuwa
ikipokelewa na mtu aliyeonekana kuwa ni mlevi wa kupindukia hali
iliyomtia wasiwasi na kuamua kuwapigia simu marafiki zake wa karibu ili
wamsaidie kumtafuta ndipo walipopata taarifa kuwa ulikuwapo uhusiano
kati ya shemeji yao na dereva huyo wa bodaboda.
Ilidaiwa
kuwa marafiki hao walikwenda moja kwa moja nyumbani kwa dereva huyo wa
bodaboda ambako walimkuta akiwa amelewa na walipoingia ndani walimkuta
shemeji yao akiwa ameshafariki dunia.”
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert
Boaz hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa alikuwa kwenye
ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda huko Gonja wilayani Same.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment