Pages

May 28, 2014

Membe amlipua Wenje


Dodoma. Wakati Bunge likipitisha bajeti ya makadirio ya matumizi Sh191.91 bilioni ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2014/15 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alitumia nafasi hiyo ‘kumchana’ Ezekiel Wenje na kusema kuwa anatumiwa na mataifa ya nje.
Mbali na hivyo aliwaita watu wanaotoa kauli za uchonganishi kuwa ni wapumbavu na akataka waache tabia za kipumbavu kwani hawatavumiliwa hata kidogo.
Membe alitoa kauli hiyo jana jioni wakati akitoa majumuisho katika michango ya wabunge kwenye hotuba ya mapato na makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka 2014/15.
Wenje ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa jana asubuhi katika hotuba yake, alimshambulia Membe kuwa ni waziri mzigo ambaye hajui wajibu wake.
Sakata hilo liliibuliwa kwenye uhusiano baina ya Tanzania na nchi ya Rwanda ambalo Wenje alilizungumzia zaidi.
Akijibu hoja hizo Membe, alisema: “Kwanza nikubaliane na kauli ya wabunge wengi kuwa uhusiano wa Tanzania na Rwanda siyo mzuri kwani kila upande haumuamini mwenzake,” aliema Membe.
Alisema kinachowaumiza pande zote ni kuwa kila upande unapozungumza na mahasimu wa mwenzake, wanahisi kuwa anataka kuipindua Serikali yao hivyo bado hawajakubaliana kwa jambo lolote lakini akasema yote yatakwisha salama.
“Huwezi kusimama hapa mtu na macho yakakutoka halafu unaanza kulizungumzia taifa lingine ambalo siyo lako, hivi unatoa wapi ujasiri huo au wanakulipa,”alihoji Membe na kuongeza.
“..Mimi naweka rehani uwaziri wangu hapa kwamba ukileta vielelezo kamili mimi nitakuwa tayari kuachia nafasi yangu, je na wewe nikitoa vielelezo utakuwa tayari kuwajibika.”
Alimtaja Wenje kwa jina kuwa alichokifanya hakifai kuwa alitoa kauli ambayo siyo nzuri kwa siri za taifa na akasema mtu kama huyo akipata nafasi hata kama nchi itakuwa vitani, yuko tayari kutoa siri.
Aliyataja makundi ya ya M23 kuwa ni moja ya kundi ambalo linaundwa na Banyamulenge waliokuwa chini ya Roral Nkunda pamoja na kundi la FDRA ambalo liliua watu wengi kwamba linaundwa na Wahutu bila ya ubishi.
Membe alimpongeza mbunge Alli Keissy kuwa alichokizungumza jana asubuhi kuhusu Rwanda na DRC Kongo ni sahihi na ndiyo maana alimshangilia kwa nguvu zote.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...